Azam, Yanga ni mechi ya kisasi, ubabe

17Mar 2024
Saada Akida
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Azam, Yanga ni mechi ya kisasi, ubabe
  • Yanga yataka kuendeleza ubabe ikitaka kujidhatiti kileleni, Azam yataka...

​​​​​​​Ni mechi ya kisasi na ya kibabe, ndivyo unavyoweza kusema kwenye mchezo wa leo ambapo Azam FC wataikaribisha Yanga kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa ukiwa mchezo wa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Azizi Ki na Feisal Saloom.

Katika mchezo wa leo ambao Azam ni mwenyeji, anaingia kuumana na Yanga huku akiwa kwenye nafasi ya tatu baada ya kukusanya pointi 44 wakizidiwa kwa pointi nane na Yanga ambao ni vinara wa ligi hiyo.

Ikumbukwe kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza uliochezwa Oktoba 23 mwaka jana, Yanga waliibuka na ushindi wa mabao 3-2 huku kiungo wake, Stephan Aziz Ki akifunga 'Hat Trick'.

Mchezo wa leo ambao utaanza saa 20: 15 usiku, unakuwa wa 36 kukutana kwa timu hizo kwenye mashindano yote ambapo katika michezo hiyo Yanga wameshinda mara 17, Azam wameshinda mara tisa huku wakitoka sare mara 10.

Katika idadi hizo za mechi, Yanga wamecheza nyumbani mara 18 ikishinda mara nane na kutoa sare mara tano huku Azam FC wakicheza michezo 15 wakishinda michezo saba, wametoka sare michezo minne na kupoteza michezo minne.

Vita ya Aziz Ki na Feitoto

Yanga wanaingia uwanjani leo wakiwa juu ya msimamo huku pia nyota wake, Azi Ki akiwa kinara wa upachikaji wa mabao akiwa na mabao 13 ikiwa ni bao moja tu zaidi ya kiungo wa Azam FC, Feisal Salum 'Feitoto' ambaye amepachika mabao 12.

Nyota hao wawili leo watakuwa na vita ya peke yao katika kufumania nyavu kwani kama Azi Ki atafanikiwa kufunga bao ataendelea kuongoza katika orodha ya wachezaji wenye mabao mengi.

Hata hivyo Feitoto naye ana nafasi ya kulingana na Aziz Ki au hata kumpiku kama atafanikiwa kufunga bao zaidi ya moja.

Kuelekea mchezo huo wa leo, Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi amesema itakuwa mechi nzuri kwa kuangalia kwa sababu timu zote zinatumia staili moja ya uchezaji.

Amesema hautakuwa mchezo rahisi kwa sababu kila timu imejiandaa kupata matokeo mazuri, vijana wake wako tayari kwa sababu amewaandaa kiakili na kiufundi licha ya kutoka kucheza mechi mfululizo

“Ni ngumu sana kucheza mechi mfululizo, lakini tupo tayari kwa mchezo wa leo, licha ya kuwepo na majeruhi kwenye kikosi changu lakini nitajitahidi kupanga kikosi imara kitakachofanikiwa kupata matokeo chanya.  Nafahamu Azam FC ni timu nzuri na inapokutana na Yanga wanakuwa wazuri zaidi lakini kikubwa tunaenda kutafuta pointi tatu muhimu,” amesema Gamondi.

Aidha, amesema kwake hapati wakati mgumu kucheza mechi dhidi ya Azam FC, licha ya kuwa na taarifa kuwepo kwa mashushu wa Mamelodi Sundowns watakaoumana nao kwenye mchezo wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

“Kwa sasa tunaangalia mechi iliyopo mbele yetu dhidi ya Azam FC, kila mchezo una mbinu yake, tutakavyocheza na Azam FC ni tofauti na tutakavyocheza na Mamelodi , kwa sasa akili zetu zipo kwenye mchezo na Azam, tunafahamu  ina wachezaji wazuri, wanajua jinsi gani ya kufanya wanapokuwa na mpira , lakini nimewaeleza wachezaji wangu jinsi ya kucheza mchezo huo na niwaombe mashabiki wetu wajitokeze kwa wingi uwanjani kuendelea kusapoti timu yao,” amesema Gamondi.

Kwa upande wake, mshambuliaji wa Yanga, Clement Mzize amesema yeye na wachezaji wenzake wana hali nzuri na wanahamasishana kutafuta matokeo mazuri na kupambana katika mchezo wa leo.

“Tunafahamu ubora wa Azam FC, tunaenda kuyafuata yale yote aliyotuelekeza kocha wetu kupambana kutafuta matokeo, kama nitapata nafasi ya kucheza nitamuonyesha kuwa hajakosea kunipanga katika kikosi cha kwanza,” amesema Mzize.

Pia amekiri kweli wachezaji wanafatiki kutokana na kucheza mechi mfululizo lakini kazi ya mchezaji ni kujituma na kutekeleza majukumu yake kwa weledi na watapambana kwa ajili ya timu.

Kwa upande wake, Kocha Mkuu wa Azam FC, Bruno Ferry amesema maandalizi yao yameenda vizuri na wanafahamu ubora wa Yanga lakini hawaihofii.

Amesema wamesahihisha makosa ya mechi zilizopita na wachezaji wake wapo tayari kwa ajili ya mchezo huo ambao utakuwa wa ushindani mkubwa.

“Hatukuwa na matokeo mazuri katika mechi yetu na Coastal Union, tulifanya makosa mengi, hata hivyo tumefanyia kazi makosa hayo  na tupo tayari kwa mchezo huu wa kesho (leo), hatuna presha yoyote tumejiandaa vizuri,” amesema Bruno.

Nyota wa Azam FC ambaye ameitwa kwenye kikosi cha timu ya taifa kama ilivyo kwa Mzize wa Yanga, Yahya Zaydi  amesema wamejiandaa vizuri na wako tayari kupambana kutafuta alama tatu muhimu dhidi ya Yanga.

“Hizi mechi kubwa kwetu tunazitaka na tumejiandaa , tunataka kulipa kisasi cha kufungwa kwenye mzunguko wa kwanza, tuna waheshimu wapinzani wetu tunafahamu ubora wao lakini pia nao wana mapungufu yao ambayo tutayatumia kupata matokeo mazuri,” amesema Yahya.