Akikabidhi mashine hiyo juzi kwa niaba ya Rais, Mbunge wa Viti Maalum CCM Mkoa wa Tabora, Aziza Sleyum alisema Rais Samia ametoa msaada huo kufutia adha walizokuwa wakikabiliana nazo hasa wakati wa kuchapa mitihani ya watoto katika vituo vyake.
“Rais Samia ameniagiza niwakabidhi mashine hii ambayo itawasaidia katika shughuli zenu kuandaa mitaala ya kiserikali na hata ya kidini ili watoto hawa ambao ni wajukuu wake wapate huduma katika kituo chenu,” alisema Sleyum.
Aidha, aliwataka wazazi, walezi, walimu pamoja na jamii kwa ujumla kuwafuatilia watoto na kusisitiza kuzishika imani zao na maadili mema wakati wote na popote na kuwasimamia katika kila jambo na kuwawekea mazingira bora na yenye usalama.
Kuhusu gharama za mashine hiyo, Sleyum alisema Rais Samia hakutaka zitajwe na kuwa lengo lake ni kuhakikisha watoto wanapata mahitaji yao staki ya kielimu na kutimiza ndoto zao.
Mwenyekiti wa taasisi hiyo, Mwalimu Amiri Mikombe alisema wana vituo 30 vya malezi na kuwafundisha pia ina watoto 930 na kwamba wanahudumia katika Wilaya za Tabora Mjini, Nzega, Sikonge, Urambo na eneo la Usoke wilayani humo.
Mwalimu Mikombe alisema kuwa awali walipata shida sana kuandaa mitihani ya watoto na nyaraka mbalimbali za kuwafundishia ambapo huduma hiyo waliipata kwa gharama kubwa na wao hawakuwa na uwezo na ndipo walipoamua kumwomba Rais mashine hiyo waliyopokea.
“Kwa sasa tumebaki na uhaba wa viti vya kukalia ambapo tuliwaomba watu wahudhuria hafla hii ili kusaidia kuchangia tupate viti 1,000 ambapo tumefanikiwa kupata mchango wa fedha taslimu Sh.84,400, ahadi Sh.100,000 na ahadi ya viti 212 na wengine waliahidi kuendelea kuunga mkono changizo hili,” alisema Mikombe.
Shekh Mahafudhi Anam aliwataka wazazi na walezi kuhakikisha watoto wanapelekwa katika mafunzo ya dini kulingana na imani zao na kuacha mtindo wa kuwaita walimu majumbani kuwafundisha, kwa kuwa elimu hiyo siyo sahihi kama ile ya darasani.