Simulizi ‘mchongo’ mabinti wa kazi wanaopokewa mijini

17Mar 2024
Na Waandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Simulizi ‘mchongo’ mabinti wa kazi wanaopokewa mijini
  • Wakimbia kuozeshwa, waangukia ukatili wa mabosi...

SHERIA ya Mtoto Na. 21 ya Mwaka 2009 inazuia utumikishaji wa watoto lakini mabinti wengi wa kazi mijini ni watoto na namna ya kuwapata ni ‘michongo’ mitupu.

Wadau wa eneo hilo waliozungumza na Nipashe wakiwamo mabinti wenyewe, wameeleza kwa kina namna ilivyo biashara hiyo, mtoto anavyoondolewa mikononi mwa wazazi wake hadi anapotumikishwa.

Serikali nayo haiko nyuma katika hilo imesema inatambua na imekuwa ikipambana na tatizo hilo na wapo baadhi ya watu wamefikishwa mahakamani.

SIMULIZI ZA MABINTI

Zawadi (si jina lake halisi) mwenye umri wa miaka 13, mwenyeji wa mkoa wa Kagera, aliingia Dar es Salaam Februari 26, mwaka huu, kwa ajili ya kufanya kazi za ndani baada ya bosi wake kutuma kijijini Sh. 150,000 kwa wakala wa biashara hiyo ili kutafutiwa msichana.

Katika mahojiano, mtoto huyo anasimulia kuwa mwaka jana aliacha shule akiwa darasa la sita baada ya viboko kuwa vingi kutoka kwa walimu wake, hivyo akaanza kutumikishwa kazi mbalimbali ikiwamo ya uyaya.

“Nilipoacha shule nikawa ninakaa nyumbani kwa mama wakati mwingine kwa bibi. Tumezaliwa  watoto wanane, mimi ni wa sita kuzaliwa, nina wadogo zangu wawili mmoja anasoma.

“Ninakaa na mama. Wazazi wangu hawaishi pamoja waliachana. Tunaishi kijiji kingine na baba anaishi kingine na wake wengine. Kabla ya kuja hapa (Dar) nilikuwa ninafanya kazi ya uyaya kwa dada (anamtaja jina). Yeye  anafanya kazi ya kudanga ana mtoto wa mwaka mmoja.

“Akienda katika madanga yake, anamwomba mama nikakae na mtoto wake. Akirudi  alikuwa ananipa Sh. 1,000 ambayo nilikuwa ninanunua vitu vidogo au siku nyingine ninampelekea mama. Mama anafanya biashara ndogo sokoni,” anasimulia.

Anasema maisha ya nyumbani kwao ni ya kawaida yakitegemea mlo mmoja au miwili kwa siku huku mama yake ambaye ndiye kila kitu, wakati mwingine hujishughulisha pia na kilimo.

“Mama ndiye anayenilea pamoja na wadogo wangu. Wakubwa wangu wengine wameolewa, kuoa na wengine wako na maisha yao. Umri wa mtoto wa kwanza sifahamu.

“Mama aliniambia nije huku (Dar) kwa ajili ya kufanya kazi za ndani. Mshahara sijui ni shilingi ngapi, sikuambiwa. Ninapenda kusoma lakini bado sijajua kusoma vizuri,” anabainisha.

Bosi wa mtoto huyo ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, mkazi wa Mwenge, anasema baada ya kumpokea na kumhoji alibaini changamoto ni ugumu wa maisha na ndicho chanzo cha usafirishaji na utumikishaji watoto.

“Kama unavyomwona amelingana na watoto wangu. Nimejiuliza ni kazi gani ya kumpa afanye? Watoto wangu wanaamka asubuhi kwenda shuleni, je, yeye atabaki nyumbani kucheza au kuangalia TV? Hapana.

“Nimewasiliana na aliyenitumia ili amjulishe mzazi wake kuwa mtoto anarejeshwa anastahili kuwa shuleni, hivyo anaondoka usiku wa kuamkia kesho (Jumamosi iliyopita) kurudi nyumbani. Nimechelewa kumrudisha kwa sababu nilikuwa ninajikusanya kutafuta nauli yake,” anasema.

Simulizi yake haitofautiani na ya Ninawajali (si jina halisi) aliyepelekwa Dar es Salaam mwaka 2022 akitokea mkoani Iringa akiwa na umri wa miaka 14.

Ninawajali ambaye anatokea kijiji cha Mgowelo, Kata ya Nyanzwa, Wilaya ya Kilolo, anasimulia kuwa alifika Dar es Salaam baada ya shangazi yake kutuma nauli kwa mama yake akitaka aende  kuuza duka. Hata hivyo, alipofika alipelekwa kwa mtu maeneo ya Sinza Madukani kufanya kazi za ndani.

“Nikawa nafanya kazi ya kufua, kupika na kuwapeleka na kuwachukua watoto shuleni. Baadaye nikawa naenda kukata majani ya ng’ombe. Ilifika hatua nikawa sipewi mshahara ndipo nilipoacha na kurudi kwa shangazi. Kwa sasa ninauza chakula kwa mtu,” anasimulia binti huyo ambaye anasema alifeli darasa la saba.

Mama mzazi wa binti huyo, akizungumza na Nipashe kwa njia ya simu mwishoni mwa wiki, alisema mtoto wake alimweleza mateso anayopata na kitendo cha kutopewa mshahara.

“Nilimwambia arudi nyumbani, akasema nimtumie nauli hajalipwa mshahara. Nilimwambia aende kwa shangazi yake wakati ninajipanga kutafuta nauli, arudi aje aolewe,” anasimulia .

Simulizi nyingine ni ya Sarafina (si jina halisi) mwenye umri wa miaka (15), mkazi ya Nagulo Bahi, mkoani Dodoma. Anasema hofu ya kuozeshwa katika umri mdogo ndiyo inayowakimbiza nyumbani kwenda mijini kutafuta kazi za ndani au kwenye migahawa.

Binti mwingine anayefanya kazi za ndani jijini Arusha (jina limehifadhiwa), anasema  mbali na kutumikishwa kazi ngumu, hupigwa na mwajiri wake amewahi kumchoma na pasi kisa alikuwa hajafua nguo vizuri.

SAFARI KWENDA MIJINI

Baadhi ya watoa huduma za usafiri wa mabasi ya mikoani, wamefunguka ugumu waupatao pindi wanapokabidhiwa watoto wadogo wenye umri kati ya miaka 13 hadi 17 kuwasafirisha kwenda mijini.

Richard Goodluck, kondakta wa mabasi ya Tilisho, anafunguka mbinu ambayo baadhi ya wazazi au madalali hutumia wanapowasafirisha watoto ni ya kukata tiketi mapema .Baada ya kufika, humkabidhi kwa kondakta na kumlipa fedha kidogo ili asishuke njiani.

“Changamoto ni pale umekubali unafika mjini, anayetakiwa kumpokea hujamwona, unalazimika kuzunguka naye mpaka achukuliwe. Kinyume cha hapo kesi umeinunua. “Wako ambao unakabidhiwa hajapewa fedha za kujikimu njiani, inabidi uingie mfukoni mnunulie japo kitu kidogo kupoza njaa,” anasema.

Dereva wa basi la Kampuni ya Masalu, Abdahallah Kazinza, anasema: "Kuna wakati tunalazimika kurudi nao walikotoka kutokana na kutowaona wenyeji wa kuwapokea au wakati mwingine hulala kwenye gari.”

WAKALA AFUNGUKA

Mmoja wa mawakala wa mabasi ya Kandahar, yanayofanya safari kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa na Singida, ambaye hakutaka jina lake liandikwe, anasema mabinti wengi wadogo kutoka mikoa ya Mwanza, Singida, Shinyanga na Simiyu wamekuwa wakisafirishwa kwenda mijini kufanya kazi za ndani.

“Wengine wanatelekezwa stendi za mabasi. Kijana akiona anamlaghai wengine wanaishia kwenda kuwafanyisha biashara za ngono,"anasema.

Msafirishaji mwingine katika stendi ya mabasi Shinyanga (jina linahifadhiwa), anasema amekuwa akisafirisha mabinti baada ya kukabidhiwa na mwanamke ambaye hakumtaja jina.

“Huwa tunawasiliana kwa simu anawapakia katika gari wakifika hapa ndipo ninawasafirisha kwenda Dodoma au Dar es Salaam. Kwa  wiki ingawa si zote, huwa ninasafirisha hadi watoto watatu. Kwa mwaka huu, nimewasafirisha 10 umri wao ni ule wa kuwa shuleni,” anasema.

MABOSI

Rehema Renatus, mkazi wa Moshi, Kilimanjaro anasema: “Nimewahi kutuma Sh. 100,000 nikaambiwa binti anatoka Mwanza Vijijini na ni mkubwa, kumbe alikuwa Pasua (Moshi).

“Alikaa kwangu kwa siku 14 tu, akaomba kuondoka akisema wazazi wake ni wagonjwa. Nilibaini baada ya muda kwamba ulikuwa mchezo. Hii ni biashara ya mtu anachukua nauli na kuwauza, halafu wanafundishwa wakifika kazini baada ya muda wafanye ukorofi ili warudi,”anasimulia.

Mkazi wa Mwanza, Gladness Godfrey, anasema baadhi ya watoto vijijini hawapendi kwenda shule kwa sababu mbalimbali ikiwamo umbali wa shule, ugumu wa maisha nyumbani, makundi rika huku wazazi wao wakishindwa kumudu gharama za shule za bweni.

“Tunajua haki ya mtoto ni kupata elimu. Wako  wanaolazimishwa kuolewa katika umri mdogo, wengine wanalazimika kutoroka nyumbani au kutoroshwa na kuletwa mijini kutumikishwa wakisahau nayo ni ukiukwaji wa haki ya mtoto,” anasema.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Karume, Kata ya Mnadani jijini Dodoma, Matwiga Kyatya, anasema amewahi kupokea kesi ya mtu kuletewa binti mwenye umri wa miaka 13 kutoka Kagera kwa ajili ya kufanya kazi za ndani kwa mshahara wa Sh. 50,000 kwa mwezi na hatua zilizochukuliwa ni pamoja na mzazi wake kuitwa, kuonywa na kukabidhiwa mtoto.

KAULI YA SERIKALI

Katibu wa Sekretarieri ya Kuzuia na Kupambana na Usafirishaji Haramu wa Binadamu, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Separatus Fella, anasema tatizo la usafirishaji haramu binadamu lipo.

Anasema hivi karibuni lilikuwapo mkoani Kigoma ambako watoto husafirishwa kutoka  Burundi kwenda kutumikishwa kazi mbalimbali zikiwamo za ndani.

“Wengine wanatumikishwa majumbani au mitaani. Tatizo hili limevuka hadi kwenye miji mikubwa kama Dar es Salaam. Wengine wanawachukua watoto wenye ulemavu kuwatumikisha mitaani,” anasema.

Fella anataja takwimu za kuzuia usafirishaji haramu binadamu kipindi cha Julai hadi Desemba, 2023 ambazo zinaonyesha wahalifu 11 miongoni mwao waliosafirisha watoto walikamatwa na kesi tatu zilifunguliwa na zinaendelea kusikilizwa.

“Waathirika 99 waliokuwa chini ya umri wa miaka 18 waliokolewa. Waathirika hawa waliokolewa mikoa mbali mbali ikiwa ni pamoja na Dar es Salaam, Arusha, Mwanza, Kigoma na Zanzibar. Hawa walikuwa wakitumikishwa kazi za majumbani, biashara ya ngono, kuchunga mifugo, kulima mashambani na kuomba mitaani,” anasema.

Anasema mtu yeyote akipatikana na hatia ya kusafirisha mtoto au mtu mwenye ulemavu, atafungwa kifungo kisichopungua miaka 30 na kadri mahakama itakavyoona inafaa atalipa faini isiyopungua milioni 50, lakini isizidi milioni 300.

Fella alisema mwaka 2008 Tanzania baada ya kuridhia mikataba ya kimataifa, ilitungwa Sheria ya mwaka 2008 ya Kuzuia Biashara Haramu ya Usafirishaji Binadamu ambayo katika kudhibiti vitendo vyote vya usafirishaji haramu wa binadamu.

“Baada ya kutungwa iliwekwa adhabu kwamba mtu akipatikana na hatia anaweza kufungwa kifungo au kulipa faini au vyote kwa pamoja.

“Hii faini ilikuwa kwa makosa ya usafirishaji watoto ilifikia hadi zaidi ya Sh. milioni 150 na kifungo hadi miaka 10, lakini mwaka juzi serikali iliona haitoshi ikafanya mabadiliko, ikaondoa faini kwa kuwa, watu walipokutwa na hatia walikuwa na uwezo wa kuilipa.

“Kwa sasa mtu akipatikana na hatia ni kifungo na faini inakuwa ni nyongeza endapo mahakama ikiamua kufanya hivyo,” anafafanua.

Alitaja mikoa mingine yenye changamoto ya kusafirisha watoto mijini ni Simiyu, Kahama na Shinyanga ambao hupelekwa kwenda kutumikishwa katika shughuli mbalimbali.

CHANGAMOTO

Fella anasema; “Changamoto ya makosa hayo ni namna ya kudhibitisha kosa lililotendeka. Ukimkuta mtu mfano, yupo na watoto 30 ili udhibitishe ni unyonyaji wanakwenda kutumikishwa kidogo inakuwa ngumu.

“Sasa hivi tumefanya mabadiliko ya sheria yapo mapendekezo mengine yanakuja lengo ni kama mtu atakutwa na watoto wadogo hatutasubiri kudhibitisha hilo tendo la unyonyaji, tutaonyesha umejaribu kutenda kosa hilo.”

Anasema jambo lingine ni uelewa na ushahidi kwa kuwa watoto wanapookolewa hawawezi kupelekwa mahakamani na kesi kuisha siku moja, hivyo kesi ikiendelea  katikati kunakuwa na uvurugaji wa kesi.

“Kwa kuwa vitendo hivi huwa vya kimtandao, baadhi hujaribu kuvuruga ushahidi kwa kutishia mashahidi kuwa watawaua endapo watakwenda mahakamani kutoa ushahidi,” anaongeza na kubainisha kuwa changamoto hizo zinafanyiwa kazi ili kusaidia kudhibiti vitendo hivyo na wahusika kupata haki.