Mwanafunzi ang’atwa nyoka akilima shamba la mwalimu

03Mar 2024
Thobias Mwanakatwe
SINGIDA
Nipashe Jumapili
Mwanafunzi ang’atwa nyoka akilima shamba la mwalimu

MWANAFUNZI wa kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari Minandi, Ikungi mkoani Singida, Felista Charles (16), amelazwa katika Hospitali Teule ya Makiungu kwa zaidi ya mwezi sasa baada ya kung'atwa na nyoka wakati akilima katika shamba la mwalimu mmoja wa shule hiyo.

Akizungumza katika mahojiano na gazeti hili katika wodi namba 14 kwenye hospitali hiyo, mama mzazi wa mwanafunzi huyo, Cecilia Neriko, amesema mtoto wake aling'atwa na nyoka Januari 23, mwaka huu, katika mguu wa kulia wakati akilima kwenye shamba la mwalimu wa shule hiyo aliyefahamika kwa jina la Robert.

Amesema baada ya tukio hilo, walimu wa shule hiyo walimpeleka kwa mganga wa kienyeji, maarufu kama Njoka, ambaye anaaminika anatibu wagonjwa waliong'atwa na nyoka lakini alishindwa kumtibu kwa kuwa sumu ya nyoka ilikuwa imeanza kusambaa na mguu kuvimba.

Neriko amesema baada ya hali ya mwanafunzi kuwa mbaya, ndipo wazazi walijulishwa na baba mzazi, Charles James, alikwenda kwa mganga huyo wa kienyeji kumchukua kwa pikipiki lakini kutokana na hali ya mtoto kuzidi kuwa mbaya na kushindwa kukaa kwenye pikipiki, walilazimika kukodi gari na kumpeleka katika hospitali ya Makiungu.

Amesema mwanafunzi huyo alipelekwa katika hospitali hiyo Januari 24, mwaka huu, na siku iliyofuata (Januari 25) alifanyiwa operesheni ya mguu kuondoa baadhi ya nyama kwenye mguu ili kuzuia sumu ya nyoka kuendelea kusambaa mwilini.

"Hali yake si mbaya sana japo bado hawezi kutembea. Ameshonwa  nyuzi kadhaa imebaki sehemu nyingine hajashonwa wanasubiri ikauke na madaktari wameshauri awe anakula mayai, maziwa machachu na samaki," amesema.

Mzazi huyo amesema licha ya tukio hilo kumpata mwanawe wakati akilima shamba la mwalimu, mkuu wa shule hiyo hajawahi kufika hospitalini kumjulia hali na gharama za matibabu yake zinabebwa na wazazi tangu alipolazwa.

Amesema Mwalimu Robert ambaye mwanafunzi alipata tukio hilo wakati akilima shamba lake, ndiye huwa anakwenda kumjulia hali na Januari 28, 2024 alipofika hospitalini, alitoa Sh. 54,000 kusaidia matumizi ya mgonjwa.

Mkuu wa Shule ya Sekondari Miandi, Juma Maati, alipotafutwa kwa siku tatu kupitia simu yake ya mkononi, alikuwa hapatikani na Mwalimu Robert kila alipotafutwa, simu yake ilikuwa ikiita na kukata na baadaye alituma ujumbe mfupi wa maneno (sms) kwamba ana taarifa za mwanafunzi huyo kung'atwa na nyoka.

Baba huyo wa mwanafunzi, amesema hali ya mtoto wake ilikuwa mbaya na kuna kipindi alilazwa katika chumba maalum cha uangalizi (ICU) na kwamba kama wangechelewa kumwahisha hospitalini, mambo  yangekuwa mengine.