Mfanyakazi kampuni ujenzi afia gesti akiwa na mpenzi wake

17Mar 2024
Said Hamdani
LINDI
Nipashe Jumapili
Mfanyakazi kampuni ujenzi afia gesti akiwa na mpenzi wake

​​​​​​​MFANYAKAZI wa Kampuni Lujuni Construction Ltd inayojihusisha na ujenzi wa barabara, Mahamudu Mbwana (44), amefariki dunia katika nyumba ya kulala wageni wakati akifanya mapenzi.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi, Kamishna Msaidizi (ACP) Andrew Ngassa, amesema kuwa Mbwana alikutwa amefariki dunia katika nyumba ya kulala wageni ya Another Coast iliyoko Kata ya Mikumbi, akiwa na rafiki yake wa kike aliyefahamika kwa jina la Gemina.

Amesema Mbwana ambaye ni mkazi Mbezi mkoani Dar es Salaam, alikutwa na umauti huo majira ya alfajiri baada ya kuanza kujihisi kuishiwa nguvu na kukoroma, ndipo mpenzi wake alipotoa taarifa kwa mhudumu wa gesti ambaye aliliarifu Jeshi la Polisi.

Baada  ya askari kufika eneo la tukio, amesema walikuta tayari ameshafariki dunia na katika suruali yake walikuta dawa za kulevya aina ya bangi.

“Baada ya kukamilisha taratibu za kiuchunguzi, mwili wa Mbwana umekabidhiwa kwa mwajiri wake, Lufurano Ludovick (64), kwa utaratibu zingine,” amesema.

Kamanda Ngassa amesema watu wengine wawili wamekufa katika matukio mawili tofauti, kwa kushambuliwa na wananchi kutokana na tabia za udokozi na mwingine kunywa sumu kwa madai ya hali ngumu za maisha.

Amesema matukio hayo yametokea Februari 27, mwaka huu na lingine Machi 4, mwaka huu.

Ngassa amewataja marehemu hao, Erick Kilonzo (19) na aliyefahamika kwa jina la Bwanga (53), wakazi wa Kata za Mpilipil na Mlandege Manispaa ya Lindi.