Ndivyo ilivyokuwa kwa mwanadada Rose Malle, mkazi wa Moshi mkoani Kilimanjaro ambaye alihukumiwa kunyongwa hadi kufa baada ya kukutwa na hatia ya kumuua dereva wa pikipiki maarufu kama bodaboda.
Kutokana na kukutwa na hatia hiyo, inawezekana watu wengi waliamini kwamba adhabu hiyo itatekelezwa lakini ikawa tofauti baada ya kukata rufani kwa msaada wa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, kabla ya kukata rufani, alikuwa amekaa gerezani miaka sita kusubiri kutekelezwa kwa hukumu hiyo.
Malle anasema ilikuwa mwaka 2012 alipomchukua dereva wa bodaboda aliyekuwa akimtumia kila siku kwa ajili ya kumpeleka chuoni na dereva huyo wakati anaondoka, alichukuliwa na watu wengine waliomjeruhi kisha kumnyang’anya pikipiki.
Siku iliyofuata, anasema alifuatwa na askari polisi chuoni na kupelekwa kituo cha polisi akituhumiwa kujeruhi na kupora pikikipiki kabla hajafariki dunia.
“Nilishtakiwa kwa kesi hiyo nikapelekwa mahakamani lakini baada ya wiki moja nikarudishwa tena polisi nikabadilishiwa kesi na kuwa kesi ya mauaji baada ya majeruhi kufariki dunia. Hapo kesi ikaanza upya nikawa nahudhuria mahakamani mpaka upelelezi ulipokamilika baada ya miaka miwili na nusu. Kesi ilianza kusikilizwa na baadaye kuhukumiwa kunyongwa baada ya kukaa mahabusu kwa miaka minne kesi ikisikilizwa,” anasimulia.
Katika shauri hilo, anasema kabla ya mwendesha pikipiki huyo kufariki dunia, alihojiwa na kutamka kuwa alivamiwa na wanaume wawili lakini kutokana na kuwa binti huyo ndiye aliyemchukua katika kituo chake na kuwa bodaboda wake kila siku, Malle alikuwa mshukiwa wa kwanza hadi kufikia kuhukumiwa.
Anasema alitumikia kifungo hicho kwa muda wa miaka miwili, hivyo kukamilisha miaka sita akiwa gerezani akisubiri siku yake ya kunyongwa na kukatisha ndoto zake za kielimu.
“Siku nahukumiwa, mama yangu alidondoka na kupata mshtuko kisha maradhi ya moyo. Vilevile, nikiwa gerezani baba yangu mzazi alifariki dunia. Sikupata hata nafasi ya kushiriki maziko yake hali iliyozidi kuniumiza zaidi,” anasimulia Malle.
MAMBO YALIVYOGEUKA
Historia ya mwanadada huyo ilibadilika baada ya Waziri Mkuu Majaliwa kutembelea gerezani mwaka 2016 kwa ajili ya kusikiliza na kutatua kero za wafungwa. Hapo ndipo alipopokewa na kilio cha Malle cha kufungwa bila kosa huku rufani yake ikicheleweshwa.
“Nilihamishwa kutoka Gereza kuu la Karanga na kuhamishiwa Gereza la Isanga mkoani Dodoma. Huko nilikaa kwa mwaka mmoja na nusu na wakati huo nilikuwa bado sijaandika sababu za rufani yangu kutokana na kukosa mwenendo mzima wa kesi yangu,” anabainisha.
“Mara ya kwanza alikuja aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba. Nililalamika juu ya kufungwa bila hatia na kucheleweshwa kwa rufani yangu na kipindi hicho gerezani nilikuwa mdogo kuliko wote, hivyo akaagiza jambo hilo lishughulikiwe lakini hakuna kilichofanyika,” anasimulia.
Baada ya hapo, anasema maisha yaliendelea gerezani lakini baada ya muda, Waziri Mkuu Majaliwa alifanya ziara gerezani hapo, hivyo kutoa kilio chake kwake kisha (Waziri Mkuu) akatoa siku tatu jambo hilo lishughulikiwe haraka.
“Hapo Waziri Mkuu ndiye alikuja kuwa mkombozi wangu kwani ndani ya wiki, nililetewa mwenendo mzima wa kesi yangu na kuandika sababu za rufani kwa mwanasheria wa magereza zikaenda Arusha. Baada ya wiki moja, nikaletewa tarehe ya kwenda kusikiliza rufani yangu,” anasema.
Pia anasema baada ya hapo, alihamishiwa gereza la Arusha na kupata nafasi ya kwenda kusikiliza rufani yake. Siku ya kwanza na ya pili alirudishwa kwa ajili ya kusikiliza hukumu na Wakili wa Jamuhuri alisema hana pingamizi na sababu na mrufani (Malle), hivyo akashinda rufani yake na hatimaye kuachiwa huru.
“Kutokana na madhila niliyopata gerezani, kuambiwa niko huru ilitosha kwangu. Sikuwa na haja hata ya kuanza kushitaki wala kutaka fidia,” anasisitiza.
Pia anasema licha kumshukuru Waziri Mkuu kupitia vyombo vya habari kwa kuhimiza jambo lake kushughulikiwa haraka na hatimaye kunusurika adhabu ya kunyongwa hadi kufa, ana shauku ya kukutana naye uso kwa uso ili amshukuru kwa kuwa bila yeye ama angalikuwa bado gerezani au ameshanyongwa.
“Nimeomba nafasi ya kukutana naye nimshukuru kwani bila yeye ningekuwa bado nasubiria siku yangu ya kunyongwa au bado naendelea tu kusota gerezani bila matumaini,” anasema.
ALIVYOPATA MUME GEREZANI
Malle anasema alikutana kwa mara ya kwanza na Mohamed Ulotu akiwa bado mahabusu gerezani Moshi ambaye kwa wakati huo alikuwa akitumikia kifungo cha miaka 30 jela na wakati huo akiwa kiongozi wa wafungwa (nyapara).
Mwanzo wa yote hayo ni wakati alipoomba ruhusa kwa askari wazungumze wakati Ulotu akipeleka wafungwa kupata matibabu katika Zahanati iliyokuwa karibu na gereza la wanawake, hivyo wakabadilishana mawazo na kupeana moyo.
“Mimi niliolewa 2019 kwa kufunga ndoa na ni mama wa watoto wawili kwa sasa,” anasema.
Naye Ulotu anasema kwa kipindi hicho ilikuwa vigumu kuwa na uhusiano wakiwa gerezani lakini walizidi kujuliana hali kila walipopata nafasi ya kukutana kwa kuwa si ruhusa kuonekana mfungwa wa kiume na wa kike wakiwa pamoja.
Anasema baada ya kumaliza kifungo chake, aliendelea kumfuatilia Malle akiwa gerezani hadi siku ya rufani yake alikuwapo na kumpa moyo kuwa atashinda. Baada ya kushinda rufani hiyo, safari ya uchumba wao ilianza rasmi kutokana na wote kuwa na nafasi ya kuonana na kuzungumza bila kipingamizi hadi walipofunga ndoa mwaka 2019.
Wawili hao mpaka sasa wamefanikiwa kupata watoto wawili katika ndoa yao na kuendelea na maisha wakijihusisha na harakati za kuwasaidia wafungwa waliomaliza vifungo vyao, wasirejee kwenye uhalifu kisha kurejeshwa gerezani.
KUSAIDIA WAFUNGWA
Male anasema kutokana na wito huo, waliamua kuanzisha taasisi inayojulikana kama Tanzania Ex-Prisoners Foundation. Lengo kuu la taasisi hiyo ni kuwasaidia wafungwa waliomaliza vifungo ili kuanza maisha ya uraiani kwa kutumia ujuzi walioupata gerezani na kuwaepusha kurudia makosa hatimaye kurudishwa gerezani.
“Idadi kubwa ya mahabusu na wafungwa wanajirudia, hivyo hali hii imetufanya tuanzishe taasisi hii ili kuwasaidia wafungwa kuwa na maisha mapya wanapokuwa uraiani. Tunawawezesha katika mbinu za ufundi na mambo mengine, hivyo tunaomba serikali kupitia wizara husika watusaidie kuinua taasisi yetu kwa hali yoyote ile,” anaomba.
Taasisi hiyo inaongozwa na Malle akiwa mkurugenzi na mumewe akiwa katibu.