RC Serukamba: naondoka Singida nikiwa nimeacha alama

10Mar 2024
Thobias Mwanakatwe
SINGIDA
Nipashe Jumapili
RC Serukamba: naondoka Singida nikiwa nimeacha alama

​​​​​​​ALIYEKUWA Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba amewaaga watumishi na wananchi wa mkoa huo na kusema kuwa, anaondoka katika mkoa huo huku akiwa ameacha alama Singida kutokana na kuhamasisha matumizi ya mbolea kutoka tani 2200 zilizokuwa zikitumika mwaka 2022 hadi kufikia tani 7,000.

Peter Serukamba.

Serukamba ambaye amehamishiwa mkoani Iringa, ametumia nafasi ya kuwaaga watumishi na wananchi kwenye kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC), ambapo amesema wakati anateuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Singida mwaka 2022 alikuta wananchi hawaamini katika kutumia mbolea lakini baada ya kuhamasisha mwaka jana zimeletwa tani 7000 za mbolea.

Amesema mipango aliyokuwa amejiwekea ni kuendelea kuwahamasisha wananchi kutumia zaidi mbolea yake hadi kufikia tani 15,000 kwani matumizi ya mbolea yakiongezeka uzalishaji wa mazao utakuwa mkubwa na hivyo wananchi kuondokana na umaskini.

Serukamba amesema alipoletwa Singida alijiwekea malengo ya kufanya kazi kwa bidii ili watu kama ni suala la kumsema wamseme kwa mambo mengine na sio la kufanya kazi kwa ajili ya kuwaletea maendeleo wananchi wa Mkoa wa Singida.

"Mimi nina safari kwa hiyo ukishangilia kuondoka kwangu utakuwa ni ujinga tu sikuwahi kufikiria kwenda Iringa, namshukru Rais Samia Suluhu Hassan ambaye ndiye ameamua kunipeleka Iringa na anazo sababu zake," amesema.