Jenerali Mabeyo amesema ameweka wazi maagizo mawili aliyopewa na Rais Magufuli alipobaini alikuwa anakaribia kufariki dunia; kwanza aliagiza aondolewe Hospitali ya Mzena, iliyoko Makumbusho, Dar es Salaam, ambako alilazwa na arudishwe nyumbani.
Mkuu huyo wa Majeshi mstaafu amebainisha agizo la pili lilikuwa kutoa wito kwa viongozi wa dini, akiwamo Paroko wa Kanisa alilokuwa anaabudu (Hayati Magufuli) pamoja na Kardinali Polycarp Pengo.
“Aliniita 'CDF (Mkuu wa Majeshi) njoo, akaniambia siwezi kupona, waamuru hao madaktari waniruhusu nirudi nyumbani'. Nikamwambia 'Mheshimiwa, sina mamlaka hayo'. Akasema 'yaani CDF unashindwa kuwaamuru wanirudishe nyumbani!'.
“Nikamwambia 'suala la afya, si la CDF, Mheshimiwa, ninaomba ubaki utulie, madaktari watatuambia'. Siku hiyo hiyo alipoona nina msimamo huo, akaniambia niitieni paroko wangu, Paroko wa Oysterbay (St. Peters), Makubi,” amesema Mkuu wa Majeshi mstaafu.
Jenerali Mabeyo aliyasema hayo katika mazungunmzo na chombo cha habari cha serikali cha mtandaoni (Daily News Digital), akisema wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama nchini, akiwamo yeye, walifika kumwona Rais Magufuli mara tatu kila siku chini ya uangalizi wa Prof. Mohamed Janabi, wakati huo akiwa Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI).
Amesema Hayati Magufuli aliagiza waitwe viongozi hao wa dini saa chache kabla ya hali yake kubadilika. Viongozi hao walipofika, walimsalia ibada ya sakramenti ya upako wa magonjwa kwa aliyekuwa na hatari ya kifo.
“Asubuhi yake, aliagiza waitwe paroko wake na Kardinali Pengo, walipofika kwa taratibu za kikatoliki, walimsalia sakramenti ya upako wa magonjwa kwa aliyekuwa na hatari ya kufariki (dunia). Ilipofika mchana wakanipigia simu watu wa hospitalini.
“Wakampigia DGIS (Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa), mimi (Mabeyo), IGP (Mkuu wa Jeshi la Polisi), 'hali ya mheshimiwa si nzuri sana'. Tukamkuta ametulia, lakini alikuwa hawezi kuongea tena, tukawaita madaktari wengine, Prof. Lawrence Museru na Prof. Mohamed Janabi alikuwapo pale muda wote, wakijaribu kumhudumia, tulikaa hadi jioni, ilipofika saa 12 na nusu au moja kasoro, alifariki (dunia),” amesema Mabeyo.
Baada ya madaktari kuthibitisha kifo cha Dk. Magufuli, Jenerali Mabeyo ametaja ulikuwa wakati mwingine mgumu kwake; namna ya kutoa taarifa, kwa familia yake, kwa viongozi wakuu wa nchi akiwamo Makamu wa Rais (wakati huo Samia Suluhu Hassan) akiwa ziarani mkoani Tanga.
“Makamu wa Rais wakati huo hayupo Dar es Salaam, Katibu Mkuu Kiongozi hakuwapo Dar es Salaam, tulikuwapo sisi tu watatu. Tukasema kwa kuwa Makamu wa Rais yuko Tanga, ngoja tumwambie Waziri Mkuu na Katibu Mkuu Kiongozi waje, bila ku-disclose (kufichua).
“Wakaja mapema, mimi kama mwenyekiti wa wakuu wa vyombo, nilitakiwa kufichua, Mheshimiwa Rais ameshatutoka. Tukaanza kushauriana, tufanyeje? Nani anatakiwa kutangaza kwenye vyombo vya habari wananchi wajue?" Jenerali Mabeyo amesimulia.
Katika hilo, Jenerali Mabeyo alisema iliwapasa kurejea kwenye Katiba ili wathibitishe kisheria, ikizingatiwa suala hilo halikuwa na uzoefu nchini - Rais kufariki dunia akiwa madarakani.
"Tukaanza kutafuta Katiba kwanza inasema nini? Mtu pekee anayeweza kutangaza kwenye vyombo vya habari ni Makamu wa Rais, na yeye yuko Tanga. Tunampigia simu au tunamwambia aje? Yakafanyika mawasiliano mengine kumwambia aje.
“Lakini kabla ya kutangaza, tukasema familia (ya Dk. Magufuli) yake haijui. Mke wake yupo hapa Ikulu. Mama yake (Mama wa Dk. Magufuli) anaumwa, yuko Chato (Geita), hajaambiwa, hatuwezi kumwambia kwa simu, nani anayekwenda kumwambia mke wake? Na mwingine wa kwenda Chato? Tukatafuta ndege ‘charter’," amesimulia.
Jenerali Mabeyo alisema hatua hizo zote zilichukua ndani ya takribani saa tano, ikiwamo kuwaita Dar es Salaam viongozi kadhaa akiwamo Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa pamoja na kutoa taarifa kwa familia ya Dk. Magufuli na mama yake aliyekuwa Chato, ndipo kifo chake kikatangazwa rasmi katika vyombo vya habari saa tano usiku (tarehe kama ya jana mwaka 2021).
Kiongozi huyo wa jeshi pia aliweka wazi kwamba kumwapisha Rais mpya lilikuwa jambo lingine gumu kwao. amesema kulikuwa na mawazo ya aina mbili; aapishwe Rais mpya kabla au baada ya maziko.
“Suala lilikuwa Rais aapishwe kabla ya kuzika au aapishwe baada ya kuzika. Tukasema kuna marais watakuja kutoka nje kuja kumzika mwenzao, watapokewa na Rais au Makamu wa Rais? Lazima awapo mwenzao (Rais), ndio maana tukafikia uamuzi Makamu wa Rais aapishwe kuwa Rais.
“Ndio maana zilipita siku mbili, kikatiba haitakiwi. Katiba inaelekeza ni ndani ya saa 24 awe ameshatangazwa Rais. Tarehe 17 na 18, ikapita na 19 (Machi 2021) ndipo akatangazwa Rais.
"Kulikuwa na majadiliano hapo… tunashukuru Mungu… namna ya kumwapisha kulikuwa na mjadala pia. Wengine wakasema isiwe ni sherehe, wengine iwapo sherehe, sasa nilichosema, lazima gwaride liwapo, bendera ya Amiri Jeshi Mkuu lazima ipande. Kulikuwa na mvutano… 'tuko kwenye msiba hakuna gwaride', nikasema huyu ni Amiri Jeshi Mkuu anayeapishwa, asipoapishwa kwa taratibu za kitaifa, jeshi halitamtambua," amesimulia.
Mkuu wa Majeshi mstaafu amesema mjadala mwingine ulikuwapo katika jinsi, kwamba Amiri Jeshi Mkuu aitwe kwa jina gani, kuwatambulisha.
“Sisi katika jeshi hatuwatambui wanawake na wanaume, ndio maana jeshini tuna ofisa na askari, hakuna mwanamume na mwanamke, hata Amiri Jeshi litabaki kuwa hivyo, ni ‘commanding chief’. Amirat ni kiongozi wa dini kwa nchi zinazoongozwa kidini. Tuliwashirikisha pia BAKITA,” Jenerali Mabeyo amesema.
Ameongeza kuwa Rais Magufuli alimteua Makamu wa Rais, akiwa msaidizi wake katika kipindi chote kwenye mamlaka akifuatwa na Waziri Mkuu.
“Rais Samia ameingia madarakani kwa tukio… tunamshukuru Mungu, mpito ulikwenda vizuri. Kwa mujibu wa Katiba, imeelezwa endapo Rais atafariki, au atashindwa kutekeleza majukumu yake kama Rais, atakayeshika madaraka ni Makamu wa Rais.
“Inawezekana watu... Katiba wakawa wameisahau kidogo… ni Rais mzuri kwa sababu anawashirikisha watu, mara nyingine wanaomshauri wanakosea, lakini anashirikisha taasisi, kitaaluma," amesema Jenerali Mabeyo.
Kifo cha Rais Magufuli kilitangazwa usiku na Rais wa sasa, Samia Suluhu Hassan Machi 17, mwaka huu, akieleza kuwa kilitokana na maradhi ya moyo yaliyokuwa yanamsumbua kwa muda mrefu. Siku mbili baadaye, Samia aliapishwa kuwa Rais kwa mujibu wa Katiba ya nchi, toleo la 1977.
KUMKUMBUKA JPM
Katika ibada maalum ya kumwombea Hayati Maguful, Makamu Askofu wa Jimbo Katoliki la Rulenge Ngara, Padri Ovan Mwenge iliyofanyika katika Parokia ya Mtakatifu Yohana Maria Muzeyi Mlimani, Jimbo Katoliki la Rulenge Ngara, wilayani Chato mkoani Geita, alikumbusha jamii kuendelea kumwombea mara kwa mara na kuacha kuhukumu pale alipokosea kama binadamu.
"Kama alikuwa na upungufu, Mungu amsamehe na kumkaribisha katika ufalme wa mbinguni maana huenda yeye kama binadamu kuna mahali alikosea," amesema Padri Mwenge wakati akiongoza ibada hiyo.
Amesema waamini Katoliki na Watanzania kwa ujumla wataendelea kumkumbuka kwa kazi alizolifanyia taifa kwa nyakati tofauti na wala si kazi ya binadamu kuhukumu, bali ni kumwombea, kama kuna watu hawaamini katika kumwombea marehemu, wabaki hivyo hivyo na kama kuna watu wanaamini wafanye hivyo.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko aliyeshiriki ibada hiyo, akimwakilisha Rais Samia, amesema maono yote ya Hayati Magufuli yanafanyiwa kazi ipasavyo.
Amesema Hayati Dk. Magufuli alikuwa na ndoto ya kuunganisha Watanzania kupitia miradi mbalimbali ya maendeleo na sasa Rais Samia anaendeleza miradi hiyo.
"Rais Samia ameendeleza ujenzi wa Bwawa la Umeme la Mwl. Julius Nyerere, reli ya kisasa ambayo majaribio yamefanyika kipande cha Dar es Salaam hadi Morogoro pamoja na ujenzi wa Daraja la Kigongo- Busisi ambalo limefikia asilimia 85 likiunganisha mikoa ya Geita na Mwanza, ninataka niwahakikishie hakuna kitakachosimama," amesema Dk. Biteko.
Amesema kauli ya Rais Samia ya Kazi Iendelee alikusudia kuyaendeleza yale yote yaliyobuniwa na Hayati Dk. Magufuli na kuwahakikishia kwamba yote aliyoyaanzisha Rais Dk. Magufuli anayaendeleza kwa kasi kubwa ili Watanzania wayapate kama walivyoyakusudia kwa Hayati Dk. Magufuli.
MTOTO WA JPM
Akiwasilisha salamu za familia, Mtoto wa Hayati Dk. Magufuli, Jesca Magufuli amesema watamkumbuka kwa kupenda maendeleo na kutanguliza mbele maslahi ya nchi.
Mjane wa Hayati Dk. Magufuli, Janeth Magufuli ameshukuru viongozi wa dini na serikali kwa jinsi wanavyoshirikiana na familia hiyo katika kuyaenzi yote ambayo alikusudia kuyatenda.
Ibada hiyo iliambatana na kumbukizi ya miaka mitatu tangu kifo cha Hayati Dk. Magufuli kilichotokea Machi 17, 2021, iliyofanyika nyumbani kwake na kuhudhuriwa na wanafamilia wakiongozwa na Janeth Magufuli, wananchi, viongozi wa dini na serikali akiwamo Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa na Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martin Shigella.