Mbokomu mna shida gani lakini?

03Mar 2024
Godfrey Mushi
Nipashe Jumapili
WARAKA WA NDANI
Mbokomu mna shida gani lakini?

UKIENDA katika Mahakama za Mwanzo katika ukanda wa juu wa Old Moshi, mkoani Kilimanjaro, nusu ya wahalifu wanaopandishwa kizimbani wanatoka Mbokomu.

Ukienda Mbokomu, mahame ni mengi (magofu ya nyumba). 

Ni kwa nini wanahama!Jibu ni rahisi tu kwamba,hakuna huduma muhimu za kijamii.

Hakuna hoteli, daladala zinazoanzia katikati ya mji, yaani kituo kikuu cha mabasi cha Moshi Mjini, migahawa, wala nyumba za kulala wageni hakuna.

Hiyo hiyo ni Mbokomu, ambayo imetoa vigogo serikalini wenye mchango mkubwa kwa taifa letu. 

Wako wale wanaoitwa 'business tycoons' wametelekeza kwao. 

Wafanyabiashara wakubwa wenye majina, wadau wa sekta ya michezo nchini, wenye majina na utajiri wa kufuru, wamejaa Dar es Salaam na majiji yetu mengine matano, wameipiga mgongo Mbokomu.

Lakini hadi leo, miaka 60 ya Uhuru, Mbokomu haina kituo cha afya, haina barabara ya lami au ya kiwango cha changarawe inayopitika kwa uhakika. 

Leo hii ndio wamepata Kituo Kidogo cha Polisi, tena baada ya wazawa kujichangisha huko mikoani.

Ukienda Mbokomu, hizo nyumba utakazoziona barabarani, miaka ya nyuma yalikuwa ni maduka, kulikuwa na soko, kulikuwa na mabasi ya SHIMATSO, sasa hivi hakuna.

Vijana wakimaliza shule wakiondoka harudi. 

Akijitokeza mzawa kutafuta mwarobaini wa maendeleo ya Mbokomu mnamuita mpinzani, mwanaharakati, mna nini lakini?

Labda shida ya Mbokomu ilianzia hapa. Nawaza tu kwa sauti! 

Wenyeji wanakuambia kila uchao, lori lililobeba pombe aina ya bia, lenye mzigo wa kati ya milioni saba mpaka 10, linapita Mbokomu na bia zinaisha kila siku.

Lakini nyama ya ng’ombe, ukichinja katika vijiji vinne vya Kata ya Mbokomu, ambavyo ni Korini Juu, Korini Kati, Korini Kusini na Tema, anzia pale lilipo soko la zamani la mitumba la Kiborloni.

Acha mguu wa nyuma wa nyama ya ng'ombe, nenda Saoni acha kichwa, Fukeni acha mguu wa nyuma, Tema acha mguu wa mbele, Kiwalaa, acha mguu wa mbele, hiyo nyama haitanunuliwa yote. Kifupi haitaisha.

Mbokomu ni Kata ya mwisho kwa maendeleo katika Jimbo la Moshi Vijijini, kwa sababu ya unafiki uliopo. 

Wenyeji wenyewe kwa wenyewe, wanaambiana mnafiki anazaa mtoto mnafiki na mjukuu mnafiki.

Wana Mbokomu, hebu tubadilike, tujipende na tuache mauzauza, tukumbuke kuwekeza kwetu. Nyumbani kwanza.

Halafu mambo ya kuitana wapinzani yanatoka wapi? Ndio maana mnapitwa na kata jirani, kwa sababu ya haya mambo haya!

Ni aibu. Leo ukienda Mbokomu na shilingi milioni moja, unaweza kulala na njaa.

Labda urudi Kiborloni. Hakuna mahali pa kufanyia matumizi, bar ya ukweli, mgahawa wa kisasa, lodge na kumbi za harusi au mikutano.

Mbokomu kuna ulevi wa kupitiliza, ulevi wa kupindukia. 

Tengenezeni sheria ndogo za kudhibiti muda wa kunywa pombe.

Gongo, pombe za vibobo huko ndiko nyumbani kwake, zimelala.

Wanaoijua Mbokomu ya sasa, wanasema afadhali ya yale mambo yaliyokuwa yakizungumzwa kipindi kile kuwaathiri wanaume wa Wilaya ya Rombo.

Haiingii akilini, asubuhi kijana anaonekana amelewa, kijana mdogo anaonekana ana umri mkubwa. 

Amezeeka kuliko hata wazee. Kumbe ni matumizi ya hovyo ya gongo na pombe za vibobo.

Kuna wazee na akina mama wazawa, ambao ni waasisi wa New Mbokomu Development Group, mnawabeza lakini wanaweza kuwa ‘taa’ kwenu.

Nyie nyie wazawa wa Mbokomu, rudishenu nguvu nyumbani, acheni kupigana vita isiyopiganiwa na Mungu. Changamkieni fursa za uwekezaji kwenye Kata yenu.

Utalii utawabeba nyumbani kwenu mmepakana na Hifadhi ya Taifa ya Kilimanjaro (KINAPA), mnao mti mrefu kuliko yote Afrika, uko nafasi ya tatu duniani, mnafeli wapi?

Jengeni basi hoteli na nyumba za kisasa za kulaza wageni, hapa ni karibu sana na Mji wa Moshi.

 Kili Marathon ni mashindano yenye hadhi ya kimataifa, yanavuta mamia kwa maelfu ya watu, wakiwamo raia wa kigeni kuja kukimbia kila mwezi Februari.

Kili Marathon ya majuzi, iliweka rekodi kwa mara kwanza ya kuingiza zaidi ya watu 11,000 katika Mji wa Moshi.

Wageni walifurika wakakosa nafasi za kulala, wakakimbilia miji ya jirani, hasa Wilaya ya Hai.

Nyie mnayo ardhi ambayo haijaendelezwa zaidi ya migomba na kahawa. 

Mngekuwa na lodge za kisasa, pesa zingependezesha mji wenu, vijana wangepata ajira, wazee wangeongeza umri wa kuishi aisee!

Godfrey Mushi, ni Mwandishi Mwandamizi wa Nipashe, Kanda ya Kaskazini. Anapatikana kwa simu namba 0715 545 490 au barua pepe: [email protected]