Mabadiliko ya uongozi yaliyotokea Machi mwaka 2021 yakifunguka tena kwa shughuli za kisiasa huku vyama vya siasa, vikiwa vimepata nafasi kushiriki kwa dhati.
Ni mambo yaliyomgusa Rais Samia Suluhu Hassan, akaamua kuwatuliza wanasiasa wenzake katika nyendo zao.Kwa kazi yangu ya uandishi, ilinikutanisha na wadau wengi.
Kimsingi, matumaini ya wananchi wa pande zote za kisiasa yalikuwa kuona Rais Samia anafanya wepesi kurudisha mikutano hiyo.
Nakumbuka Rais Samia alimaliza mwaka huo , ikionyesha kipimo chake kingine cha kisiasa, alivyokuwa anatakiwa kukivuka.
Kilikuwa kipimo ambacho Rais Samia alidhihirisha, huku maelfu ya wananchi wa Tanzania wakisubiri tamko la Rais Samia kuhusu shughuli za kisiasa.
Tamko hilo lilikuwa muhimu, huku Katiba ya nchi nayo ikiruhusu kufanya uamuzi kadri anavyoona inafaa kwa maslahi ya nchi.
Rais Samia alivuka wakati na kufanya uamuzi, akihakikisha tamko lake kuhusu shughuli za kisiasa linakuja wakati ambao ameridhishwa na kile alichokipanga.
Uthibitisho wa hilo ni hotuba yake iliyosema “nasimamisha na kufungua nchi” akiwa amelenga kutekeleza kwanza mikakati iliyokuwa mezani kwake kuhusu marekebisho kadhaa ya masuala ya uongozi nchini.
Alianzia shughuli za diplomasia, afya, uchumi na ziara kadhaa katika nchi za Afrika na nje ya Afrika. Rais Samia akiendelea na shughuli hizo, huku akichora ramani yake ya kisiasa kuhusu namna anavyotaka nchi iendeshwe na wanasiasa wanapaswa kufanya nini kwa maslahi ya wananchi.
Kana kwamba haitoshi, akaadhimisha Siku ya Demokrasia nchini, akiandika makala mazuri ambayo ikaonyesha ramani yake kwenye siasa.
Akafafanua, anahitaji siasa za kistaarabu na wanasiasa wanaweza kuendesha mikutano bila matusi, kuvunjiana heshima na kutupiana kashfa.
Baada ya hapo Rais Samia, akafanya mazungumzo na viongozi wa vyama vya siasa mbalimbali pamoja na kukutana nao kwenye Jukwaa la Vyama, huku akishauriwa kuendelea kuongoza vizuri nchi yetu.
Awamu nyingine, akakutana na Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, wakiwa na ajenda kuu ya maridhiano. Katika mikutano yao viongozi hao wawili walikubaliana na kuendesha siasa za kistaarabu kwa maslahi ya nchi.
Katika kipindi hicho ndipo Rais Samia alileta falsafa yake ya R4 yenye kulenga Maridhiano, Amani na Ustaarabu miongoni mwa wadau na viongozi wa kisiasa bila kuwasahau wananchi.
Haijalishi mafanikio ya R4 yamefikia kiasi gani, lakini furaha iliyopo sasa katika mikutano ya hadhara na maandamano yanayofanyika sehemu mbalimbali nchini ni matokeo ya maono ya Rais Samia, kuwaachia watu uhuru wa kujieleza pasipo kutweza haki za wengine.
Kama kiongozi mkuu wa nchi, alijaribu kulinda taswira ya serikali ya Tanzania, kisha akajenga taswira ya hali ya demokrasia. Kwa kipindi cha miaka mitatu, Serikali ya Awamu ya Sita imefanikiwa kuwaachia uhuru wa kujieleza hali ambayo inawapa furaha wanasiasa na manazi wao.
Baadhi ya vyama hivyo vimekuwa kwenye mchakamchaka wa kisiasa na kuitengeneza taswira ya kidemokrasia kuwa yenye kulinda haki na kuheshimu uhuru wa watu wengine.
Samia naye akafanya hayo, akiruhusu wasaidizi wake ndani ya chama kuhakikisha wanafanya siasa za kistaarabu.
Mambo yanaiva, Paul Makonda wa CCM akizunguka sehemu mbalimbali kuwahutubia wananchi na kusikiliza kero zao na kukiuza vizuri chama chake, hali kadhalika kina Benson Kigaila na wezake wa CHADEMA nao wapo kwenye mikutano na maandamano ya amani kwa kila mkoa. Wako katika majiji wakianzia na Dar es Salaam kisha Mwanza, Mbeya na wiki hii, Arusha.
Hiyo inamuachia Rais Samia taswira kuwa mjenzi wa nuru ya kisiasa inayoendelea nchini. Anaweza kuzungumziwa kwa namna yoyote, lakini walau katika hilo asinyimwe maua yake, kwani ametenda katika siasa za nchini.
Kimsingi ameelekeza, amesimamia, ameonyesha dira, amewapa uhuru wasaidizi wake ndani ya chama huru wa kupambana kisiasa na wanasiasa wa vyama vya upinzani.
Ligine nalitazama, amejaribu kutenganisha shughuli za chama na serikali. Kwamba CCM wanaweza kuendesha hekaheka za siasa kwa ‘kunyukana’ na wapinzani wao bila serikali kutia mkono wake.
Leo tukianza kumhesabia siku kufikia stendi ya miaka mitatu.