Marekani kuhamisha raia wake Haiti kisa vurugu

18Mar 2024
Nipashe
Marekani kuhamisha raia wake Haiti kisa vurugu

MAREKANI imetangaza kuwa imepanga kuwahamisha raia wake kutoka Haiti, kufuatia wiki kadhaa za ghasia za magenge ya uhalifu ambazo zimelikumba taifa hilo la Caribbean.

Hakuna tarehe rasmi iliyotolewa na haijulikani ni wamarekani wangapi watakaoweza kuhamishwa kutoka Haiti.

VOA imeripoti kuwa, Ubalozi wa Marekani nchini Haiti umesema raia hao watahamishwa kutoka mji wa pili kwa ukubwa wa Cap-Haitien, wakati uwanja mkuu wa ndege katika mji mkuu wa Port-au-Prince ukiendelea kufungwa kutokana na machafuko hayo.

Serikali ya Guatemala imesema ofisi za ubalozi wake nchini Haiti zilivamiwa na magenge hayo ya wahalifu ambayo yamekuwa yakishinikiza Waziri Mkuu Ariel Henry kuachia madaraka. Kiongozi huyo ametangaza siku ya Jumatatu kuwa atajiuzulu mara baada ya kuundwa kwa baraza la mpito.