Aliongeza kwamba, kwa kuwa madini muhimu ni rasilimali zisizoweza kujadidishwa, ni muhimu sekta ya umma na binafsi kuungana na kufanya kazi kwa karibu ili pande zote ziweze kunufaika kikamilifu.
Mbibo aliyasema hayo jana Machi 5, 2024 wakati akitoa wasilisho kwenye Mkutano wa Wadau wa Madini Mkakati wa Asia na Afrika ulioandaliwa na Institute of Geoscience and Mineral Resources (KIGAM) ya nchini Korea Kusini na ambapo mkutano huo unaofanyika kwa Siku Mbili.
Alisema kwamba nchi ya Tanzania imebarikiwa utajiri wa kijiolojia unaobeba madini muhimu ya aina mbalimbali ikiwemo ya kimkakati ya nikeli, colbati, lithium, Shaba, niobioum, graphite pamoja na mengine muhimu ambayo yanahitajika duniani hivi sasa.
Alieleza kuwa, katika kuhakikisha kwamba Ukanda unanufaika ipasavyo na rasilimali za madini hususan mkakati katika uzalishaji wa nishati safi, Serikali ya Tanzania chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, imechukua hatua za makusudi kuwezesha shughuli za uwekezaji nchini na kuzitaja baadhi kuwa ni pamoja na kuvutia uwekezaji wa umma na kampuni binafsi kufanya shughuli za utafiti wa madini ili kuibua vyanzo vipya vya madini mkakati, kuvutia wawekezaji wa kimataifa kushirikiana kuendeleza miradi ya kimaendeleo inayokwenda sambamba na vipaumbele vya taifa.
Alisema hatua nyingine ni pamoja na kuongeza uwazi na kujenga mazingira ya ushindani katika mnyororo mzima wa shughuli za madini muhimu na mkakati, kuongeza ushirikiano wa kimataifa na kuweka mazingira yanayokwenda sambamba na Sera za nchi pamoja na kuboresha usimamizi wa rasilimali madini ili kuwezesha ukuaji endelevu wa uchumi na kupunguza umaskini.
Vilevile, alisema kuwa, mbali na hayo, jiografia ya Tanzania inayounganisha nchi mbalimbali ni sababu tosha inayoifanya nchi hiyo kuwa sahihi kwa uwekezaji ikiwemo uwepo wa miundombinu inayoiunganisha na maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na uwepo wa bandari kubwa katika maeneo tofauti, amani na ukarimu wa watanzania.
Aliongeza kwamba, ushirikiano na Korea Kusini na nchi husika utapelekea kuwepo maendeleo endelevu kiuchumi kupitia Sekta ya Madini na hivyo kuwezesha uzalishaji wa ajira kwenye nchi ya Tanzania na duniani kiujumla na kutumia fursa hiyo kuipongeza KIGAM kufuatia jukumu kubwa inalofanya la kukuza ushirikiano na kuendeleza ustawi katika tasnia ya uzinduaji pamoja na kuonyesha maendeleo katika undelezaji wa madini mkakati.
Alipongeza taasisi hiyo kwa kuandaa hafla hiyo inayofanyika kila mwaka ambapo huwakutanisha watafiti wengi, wabunifu katika nyanja nyingi ikiwemo TV za betri za umeme na kueleza ni utaratibu ambao haupaswi kuachwa kwa mutskabali wa maendeleo wa madini mkakati duniani na bila kuathiri maendeleo ya pande zozote.
Katika hatua nyingine, Mbibo alifanya mazungumzo na Rais wa KIGAM, Pyeong –Koo Lee ambapo wamejadili maeneo ambayo Korea Kusini inaweza kushirikiana na Tanzania kupitia taasisi ya GST. Masuala mengine yalizungumzwa yanahusu uwekezano wa KIGAM kuendesha utafiti wa pamoja na GST, ikiwezo ujenzi wa smelter na kuanzisha program maalum ya kuongeza ujuzi.
Aidha, akiwa nchini humo Mbibo alipata nafasi ya kuweka saini kitabu cha wageni cha maombelezo ya Rais Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Pili Hayati Ali Hassan Mwinyi ambaye alifariki dunia hivi karibuni.
Wengine wanaoshiriki katika mkutano huo ni Kamishna wa Madini Dk. AbdulRahman Mwanga na Mkurugenzi wa Huduma za Jiolojia kutoka GST Dk. Ronald Massawe.