Bashiru amekuwa ni kivutio kwa kushangiliwa kuliko wachezaji wengine kila anapogusa mpira katika mashindano haya yanayoendelea kwa kuonyesha kiwango cha juu.
Akizungumza na gazeti hili jana, mmoja wa viongozi wa timu hiyo, Contact Kazungu, alisema tayari mmiliki wa timu hiyo ameridhishwa na kiwango cha Bashiru na ameahidi ataanza mchakato wa kumsajili nyota huyo.
Kazungu alisema wanaamini wakimpata mchezaji huyo, timu yao itaendelea kufanya vizuri katika ligi na mashindano mengine ya ndani ya Rwanda wanayoshiriki.
"Kiwango cha yule mchezaji ni kizuri, tunamhitaji katika timu yetu, naamini sasa soka la wanawake linazidi kukua katika ukanda wetu," alisema kiongozi huyo.
Bashiru aliingia akitokea benchi katika mechi ya kwanza dhidi ya Rwanda ambayo Kilimanjaro Queens ilifungwa, lakini akacheza dakika zote kwenye michezo iliyofuata dhidi ya Kenya na Uganda.
Wachezaji wengine ambao nyota zao zimeng'ara na wanatakiwa ni Mwanahamisi Omary "Gaucho" na Amina Ally ambao wamewavutia viongozi wa mabingwa wa Ligi Kuu ya Wanawake Rwanda, AS Kigali.