ambaye wakati akijiuzulu juzi alikabidhi timu hiyo kwa Baraza la Wadhamini.
Ujasiri wa kutamka neno "kumekucha" unatokana na Kamati ya Utendaji ya Yanga, kumteua, Omar Kaaya kuwa Kaimu Katibu Mkuu kuanzia jana huku Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini la klabu hiyo, George Mkuchika, akiwataka wanachama kutulia wakati wakijiandaa kuweka mambo sawa.
Msemaji wa Klabu ya Yanga, Dismas Ten, jana aliwaambia wanahabari kuwa Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo imemteua Kaaya kukaimu nafasi ya Katibu Mkuu wa klabu hiyo kuanzia jana kufuatia Mkwasa kujiuzulu kwa sababu za kiafya.
"Kamati ya Utendaji, imemteua Kaaya (Omar) kukaimu nafasi ya Katibu Mkuu mpaka hapo itakapotangazwa vingenevyo," alisema Ten.
Kwa upande wa Mkuchika, ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, akizungumza na kituo kimoja cha Radio jana, alisema mambo yatakuwa sawa na kwamba kwa sasa wanamaliza kwanza suala la usajili na baadaye watageukia mambo ya utawala.
Dirisha la usajili kuelekea msimu mpya wa Ligi Kuu litafungwa kesho Julai 26.
“Haya yote yatapita, wanachama wa Yanga watulie katika kipindi hiki na sisi tutakutana kuweka mambo sawa,” alisema Mkuchika.
Alisema pindi atakaporejea Dar es Salaam, ataitisha Kikao cha Baraza la Wadhamini la klabu hiyo kujadilia kujiuzulu kwa viongozi wa timu hiyo na mustakabali wake.
Kwa mujibu wa Katiba ya Yanga, baada ya kujiuzulu kwa viongozi wa juu klabu hiyo itakuwa chini ya Baraza la Wadhamini mpaka hapo watakapoitisha uchaguzi kuchagua viongozi wapya wa kuziba nafasi zilizoachwa wazi.
Nafasi zilizoachwa wazi kufuatia kujiuzulu kwa viongozi hao wa juu ni Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti pia nafasi ya wajumbe wanne.
Nafasi ya Katibu Mkuu iliyoachwa wazi na Mkwasa ni ya kuajiriwa hivyo hujazwa baada ya Kamati ya Utendaji kukutana na kumtamfuta mtu mwenye sifa.
Yanga kwa sasa inapitia wakati mgumu wa ‘ukata’ pamoja na kuondokewa na viongozi wake, hali hiyo inatokea huku ikiwa kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika pamoja na maandalizi ya msimu mpya wa Ligi Kuu Bara iliyopangwa kuanza Agosti 22, mwaka huu.
Katika hatua nyingine Msemaji wa Yanga, Dismas, alitangaza viingilio vya mchezo wao wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Gor Mahia utakaopigwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Jumapili.
Alisema kiingilio cha chini kwenye mchezo huo kimepangwa kuwa Sh. 3,000 ili kutoa fursa kwa wanachama na mashabiki wengi wa klabu hiyo kujitokeza.
Viingilio vya juu alitangaza kuwa vitakuwa Sh. 7,000 na 10,000 huku akieleza kuwa kikosi cha timu hiyo kikiendelea na maandalizi ya mchezo huo na kina matumaini yao kufanya vizuri baada ya mechi ya awali kuchapwa mabao 4-0 jijini Nairobi.