Kichanga hicho kilichozaliwa wiki iliyopita kimeokolewa na mwananchi Ally Hussein, aliyekuwa anapita njiani karibu na choo hicho baada ya kusikia sauti ya mtoto.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi, Kamishna Msaidizi (ACP) Andrew Ngassa, amesema baada ya mwananchi huyo kusikia sauti ya kichanga chooni alitoa taarifa kwa wananchi na kufanikiwa kumwokoa.
“Askari walipofika eneo la tukio walikichukuwa na kukipeleka Hospitali ya Mkoa Sokoine iliyoko mjini Lindi kwa matibabu zaidi,” amesema.
Ngassa amesema askari walipofanya uchunguzi walibaini michirizi ya damu iliyoanzia eneo la choo hadi nyumbani kwa mwanafunzi huyo.
Amesema baada ya mwanafunzi huyo kutekeleza tukio hilo alikwenda shuleni na kuendelea na masomo yake.
“Baada ya kubaini hilo askari walifika shuleni na kumkuta wakamchukua hadi kituoni kwa mahojiano na amekiri kutenda kosa,” amesema ACP Ngassa.
Kaimu Kamanda amesema mama mzazi wa mwanafunzi huyo, Wepi Ibrahimu, alipoulizwa kuhusu mwenendo wa binti yake alijibu hakujua kama ni mjamzito na siku ya tukio alimwona akijiandaa kwenda shule kuendelea na masomo yake.
Amesema baada ya mahojiano na kukiri kosa mwanafunzi huyo amekabidhiwa chini ya uangalizi wa Idara ya Maendeleo ya Jamii,huku taratibu za kisheria zikiendelea kuandaliwa dhidi yake.
Mganga Mfawidhi Hospitali ya Sokoine Mkoa wa Lindi, Dk. Alexanda Makalla, amekiri kumpokea kichanga hicho ambacho afya yake inaendelea kuimarika.
Mwanafunzi huyo amedai kuwa alitekeleza tukio hilo ili aendelee na masomo.