Rubani ATCL asimulia alivyoamua kuzima injini na kurejesha ndege Dar

01Mar 2024
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Rubani ATCL asimulia alivyoamua kuzima injini na kurejesha ndege Dar

RUBANI wa ndege ya Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) Airbus A220-300 iliyopata hitilafu ya injini angani ikiwa njiani kwenda  Mbeya, William Zelothe, ameelezea alivyochukua uamuzi wa kugeuza ndege na kurejea Dar es Salaam.

Februari 24, mwaka huu, majira yaa saa 12:00 asubuhi, ndege hiyo iliruka kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam kwenda  Mbeya. Nusu  saa badaye ,ikiwa usawa wa Mbuga ya Taifa ya Mikumi mkoani Morogoro,  moja ya injini zake ilipata hitilafu.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Zelothe alisema hatua za kiusalama alizochukua na wahudumu wa ndege, kutokana na hitilafu hiyo, ni matunda ya mafunzo waliyopewa na shirika hilo.

Siku  hiyo, alisema injini ilipata joto na kuanza kutoa moshi ambao uliingia kwenye mfumo wa kiyoyozi (air condition) hali ambayo ilisababisha woga kwa baadhi ya abiria ingawa hakukuwa na taharuki kubwa.

“Moshi uliendelea kwa dakika tano tu ukaisha na wahudumu wetu ndani ya ndege walichukua hatua za kwanza za kiusalama ikiwamo kuwapa taarifa abiria kinachoendelea,” alisema.

Zelothe alisema hatua ya kwanza aliyochukua ni kuzima injini iliyokuwa na hitilafu ili kuepusha madhara ambayo yangetokea iwapo hali hiyo ingeendelea kwa muda.

“Kwa kawaida ndege hiyo ingeweza kuendelea na safari hadi Mbeya kwa kutumia injini moja bila shida yoyote lakini kwa kuzingatia zaidi suala la usalama, mimi rubani kiongozi niliona ni busara kuirudisha ndege Dar es Salaam,” alisema.

Alisema marubani, wahudumu na wahandisi wa ndege wa ATCL wamekuwa wakipewa mafunzo ndani na nje ya nchi namna ya kukabiliana na dharura wakati wa safari.

“Ndege zote huwa zinatengenezwa na kitu kinaitwa ‘redundancy’ ndiyo maana zinatengenezwa injini mbili. Moja  ikifa nyingine inakuwa na uwezo wa kumaliza safari iliyobaki salama. Kwa  hiyo wananchi wafahamu kwamba ndege zetu za Airbus ziko salama, hivyo  hakuna haja ya kuwa na hofu,” alisema.

Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL, Ladislaus Matindi, alisema moja ya injini za ndege hiyo ilikuwa imetoka kwenye matengenezo Ujerumani na ilipata hitilafu ya kiufundi angani ikiwa na abiria 122 na hakuna madhara yoyote yaliyotokea.

Alisema ndege hiyo ilipaa Ferbruari 24, saa 12:00 asubuhi na baada ya nusu saa, ilisikika harufu ya moshi ambao baadaye ulitanda ndani ya ndege kutokana na hitilafu kwenye moja ya injini.

Kutokana na hitilafu hiyo, alisema rubani aliamua kurudi Dar es Salaam na baada ya ndege hiyo kufika, abiria 104 walikubali kusafiri kwa kutumia ndege nyingine ya shirika lakini wengine 18 waliomba kubadilishiwa siku ya safari.

Mkuu wa Usalama wa ATCL, Emmanuel Twai, alisema hitilafu ni jambo linalotarajiwa kwenye chombo chochote lakini cha msingi ni tahadhari za kiusalama kuzingatiwa muda wote wa safari.

Alisema hatua ya kwanza ya kiusalama aliyochukua rubani ni kurejesha ndege Dar es Salaam ili wahandisi wa ndege wakague tatizo na kulifanyia kazi kabla ya kuanza safari nyingine.

“Hatua aliyochukua rubani ni sahihi kabisa kwa sababu kama wangekwenda Mbeya, huenda isingepata huduma za haraka kama ambavyo ilipata ikiwa hapa Dar es Salaam ambako kuna wahandisi na wataalamu wote,” alisema.

Twai alisema si kila hitilafu inayotokea wakati wa safari ya ndege angani inatolewa taaarifa kwa umma na hilo limekuwa likifanyika ili kuondoa taharuki inayoweza kutokea kwenye jamii kuhusu usafiri wa anga.

Aliyekuwa kiongozi wa wahudumu waliokuwa ndani ya ndege hiyo, Mwanaidi Mwanga, alishukuru mafunzo ambayo ATCL wanawapa ndiyo sababu ilipotokea hitilafu hiyo, walitimiza wajibu wao kitaalamu na bila kutetereka.

“Tunamshukuru pia rubani alitwambia tusiwe na wasiwasi atakabiliana na hali hiyo akasema tuendelee na taratibu zetu za kazi ndani ya ndege na kauli hiyo ilitupa moyo wa kufanya kazi kwa weledi na kuwatuliza abiria ambao walianza kupata hofu kubwa,” alisema.