Wanawake NACTVET watoa msaada kwa wafungwa wanaume Segerea

05Mar 2024
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Wanawake NACTVET watoa msaada kwa wafungwa wanaume Segerea

Wafanyakazi Wanawake wa Bazara la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi (NACTVET), leo Machi, 05, 2024, wametembelea Gereza la Segerea,jijini Dar es Salaam, na kuwapatia msaada wafungwa na mahabusu wanaume katika gereza hilo.

Akizungumzia hatua hiyo, Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake NACTVET, Deborah Ngalemwa amesema, tukio hilo ni sehemu ya maadhimisho kuelekea kilele cha Siku ya Wanawake Duniani, ambayo huadhimishwa tarehe 08 Machi kila Mwaka.

“Tumekuja hapa leo kwa niaba ya Wanawake wa NACTVET kutoa msaada kwa Mahabusu na Wafungwa Wanaume kama ishara ya kulikumbuka kundi hili linalosahaulika nyakati kama hizi ili kuwaona na kuwapatia msaada na kufurahi pamoja nao,” amebainisha Debora.

Pia ameongezea kwa kusema, wafungwa na mahabusu, walioko gerezani wanastahili faraja na wanapotembelewa hujihisi ni sehemu ya jamii kama raia wengine walioko huru.

Kwa upande wake, Mkuu wa Gereza la Segerea , ACP Hamisi Alute Lissu ametoa shukrani na kuwapongeza wanawake wa NACTVET kwa msaada huo na kuahidi msaada uliotolewa utatumika kwa ajili ya walengwa kama ilivyokusudiwa.

“Napenda kuwashukuru kwa kuchagua kuja katika Gereza hili la wanaume kuwapa tabasamu kwa kuwaletea mahitaji mbalimbali ," amehitimisha ACP Lissu.

Vitu vilivyotolewa ni pamoja na Sabuni za kufulia/kuogea kandambili, mafuta ya kujipaka , miswaki na dawa za meno.

 Wanawake wa NACTVET kila mwaka wamekua na kawaida ya kutembelea na kutoa msaada kwa watu wenye mahitaji mbalimbali katika jamii,wakati wa kuadhimisha siku ya wanawake duniani.

Habari Kubwa