Manara atoa neno Yanga

25Jul 2018
Faustine Feliciane
DAR ES SALAAM
Nipashe
Manara atoa neno Yanga

AFISA Habari wa Klabu ya Simba, Hajji Manara, amesema kinachotokea sasa kwa wapinzani wao, Yanga ni jambo la kujifunza kwa klabu nyingine za Ligi Kuu nchini zisizotaka mabadiliko ya uendeshwaji.

AFISA Habari wa Klabu ya Simba, Hajji Manara.

Manara, alisema jana kuwa wao kama Simba wanasikitishwa na hali mbaya inayoendelea kwa wapinzani wao na kuwaomba wakae pamoja na kutatua changamoto zinazowakabili ili kuifanya timu yao kuwa imara na pindi watakapoifunga wasipate kisingizio.

Kauli hiyo ya Manara, imekuja siku moja tu baada ya aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga, kutangaza kujizulu nafasi zote ndani ya klabu hiyo.

“Unajua kinachotokea sasa kwa watani zetu hata sisi tuliwahi kukipitia japo hatukufika hapa walipofika wenzetu, na hili ni funzo kwa klabu zingine zisizotaka mabadiliko ya uendeshwaji wa klabu zetu,” alisema Manara.

Alisema ni lazima klabu zikubali mabadiliko kwa kuwa uendeshwaji wa soka kwa sasa umebadilika.

“Sisi tunaamini bila kuwapo kwa Yanga imara hakuna Simba imara…, tunaomba wamalize mambo yao na timu irudi kwenye hali yake ili hata tutakapokutana Septemba 30 tukiwafunga wasiwe na visingizio…, hivi kwa hali hii waliyonayo tukikutana nao tukawafunga mabao 5-0 tutajisifia? Hapana watakuwa na kisingizio, tunawaombea mambo yao yaende sawa,” alisema Manara.

Aidha, Manara alisema soka si uadui wala uhasama bali ni sehemu ya burudani na kuwataka mashabiki wenye mawazo mabaya wabadilike.

“Nimesikitika kusikia Sanga ameachia ngazi kutokana na vitisho kutoka kwa mashabiki na wanachama wa klabu yake, mimi niseme tu kwa wanafamilia ya mpira, hatupaswi kufika huko, mpira si vita,” alisema Manara.

Wakati Sanga akitangaza kujiuzulu juzi, alisema moja ya sababu zilizomfanya kufikia uamuzi huo ni kutokana na kutishiwa maisha na baadhi ya wanachaama wa klabu hiyo kutokana na Yanga kutofanya vizuri.