Yanga: Ni vigumu nje ndani kwa Gor

26Jul 2018
Faustine Feliciane
DAR ES SALAAM
Nipashe
Yanga: Ni vigumu nje ndani kwa Gor
  • ***Kocha Zahera aanika mbinu za kuchomoa kwa Wakenya hao lakini...

LICHA ya kupitia kwenye kipindi kigumu, benchi la ufundi la Yanga limesema haliwezi kukubali kupigwa nje ndani na wapinzani wao Gor Mahia wanaojiandaa kukutana nao Jumapili kwenye  mchezo wa marudiano wa Kombe la Shirikisho Afrika.

kocha wa timu hiyo Mwinyi Zahera.

Akizungumza na Nipashe jana, kocha wa timu hiyo Mwinyi Zahera, alisema licha ya kufungwa mabao 4-0 na wapinzani wao hao jijini Nairobi, ameona udhaifu wao na atautumia kuipa matokeo mazuri timu yake.

"Halitakuwa jambo zuri kupoteza mchezo wa pili dhidi yao, Gor Mahia ni wazuri lakini pamoja na mambo yote yanayoendelea tutahakikisha tunaondoka na ushindi," alisema Zahera.

Alisema bado ana imani na kikosi chake licha ya kuwa timu hiyo kwa sasa inapitia wakati mgumu huku baadhi ya nyota wake wakiwa kwenye mvutano wa kusaini mkataba mpya baada ya mikataba yao ya awali kufikia mwisho.

"Natumaini mpaka kufikia leo jioni (jana) viongozi watakuwa wamemalizana na wachezaji wenye matatizo ya mkataba na ambao tunawahitaji," alisema Zahera.

Nyota wa timu hiyo wanaosubiri mkataba mpya ni Kelvin Yondani na Andrew Vincet 'Dante' ambao mikataba yao imemalizika na bado hawajaripoti kwenye mazoezi ya timu hiyo.

Dirisha la usajili linafungwa leo saa sita usiku na viongozi wa Yanga wanahangaika kumalizana na wachezaji hao ili warejee kikosini.

Meneja wa timu hiyo, Hafidh Saleh, aliliambia Nipashe jana kuwa nyota hao watamalizana na uongozi leo.

"Sina uhakika sana, lakini nafahamu leo watamalizana na kurejea kikosini," alisema Saleh.

Katika hatua nyingine, baada ya kushindwa kuingia kambini kujiandaa na mchezo dhidi ya Gor Mahia Jumapili ijayo, kocha Zahera, amesema itakuwa jambo zuri kama timu itaingia kambini sehemu tulivu kujiandaa na Ligi Kuu Tanzania Bara.

"Nafahamu muda haukutosha kwa maandalizi ya kuingia kambini kujiandaa na mchezo wetu ujao (dhidi ya Gor Mahia), lakini ningependa baada ya mchezo huo tuingie kambini kwa ajili ya ligi, nimeambiwa ligi inaanza Agosti 22 muda uliopo nataka kuutumia vema kuweka sawa kikosi changu," alisema.

Yanga itafungua pazia la Ligi Kuu kwa kucheza dhidi ya Mtibwa Sugar Agosti 23, mwaka huu kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.