Kinachowapata wanawake wenye dharau kwa wakwe

19Jun 2023
Flora Wingia
Nipashe
Maisha Ndivyo Yalivyo
Kinachowapata wanawake wenye dharau kwa wakwe

​​​​​​​KARIBU msomaji wangu, leo tunaendeleza mada iliyopita kuhusu wakwe. Nilitaja mambo kadhaa ambayo mke anapaswa kujua kuhusu wakwe. Nikasema ipo misingi na kanuni ambazo tunapaswa kuzingatia ili maisha yawe mazuri na tulivu.

Ndoa nyingi zinapata misukosuko mingi kwa sababu tu wanandoa wenyewe wanakiuka misingi hiyo. Wanawake wengi leo wapo katika sintofahamu nyingi kuhusu ndoa zao. Wengine wamezikimbia, wengine wamejitia nguvu kutegemeana na yale wanayopitia. Wengine wamepoteza maisha kwa sababu tu hawakuzingatia mambo ya msingi.

Leo msomaji wangu nikazie eneo moja nililotaja na kuahidi kutoa mifano hai,  kinamama waliopuuzia wazazi au ndugu wa mume na kupata madhara. Tambua kuwa mume wako ana wazazi wake.

Wanawake wengi wanapoingia katika ndoa, hupuuzia sana eneo hili ndio maana wanapata madhara makubwa katika maisha. Wake wengi huwa wanaishi kana kwamba waume zao walitoka mbinguni na hawana wazazi, huku wao wakiwahudumia wazazi wao.

Hii ni hatari sana! Kama ukishindwa kutambua kuwa mume wako ana wazazi na ndugu zake, na sehemu kubwa bado wanamtegemea, hautoishi kwa utulivu hakika! Ukiwadharau, wanaweza kufikia hatua ya kukutoa katika nyumba ya mtoto wao! Uwe na hekima ya kuwapenda, usiwabague.

Hata kama wazazi hawa wamekufanyia ubaya wa aina gani, mume wako anatarajia uendelee kuwapenda, sawa na vile unavyowapenda wazazi wako. Hebu sikia habari hii ya kusikitisha ikiwa ni madhara ya kudharau wakwe. Usithubutu kuua kuku aliyetaga dhahabu!

Yupo mama mmoja alisimulia tukio lililompata mama, rafiki yake aliyepoteza maisha miaka kadhaa iliyopita, chanzo kikitokana na kuwadharau wakwe na ndugu wengine wa mume wake.

Wanawake hawa wawili wote wameolewa kwa ndoa nzuri na pia wanaume zao wana kazi nzuri katika taasisi kubwa serikalini. Kingine kinachoshabihiana kwao ni waume zao wanatoka mkoa mmoja na kabila moja.

Mama huyu akisimulia mazingira ya kifo cha rafiki yake, akasema kuwa kabla ya kifo alikuwa akimshirikisha mambo mbalimbali anayokutana nayo katika maisha yake ya ndoa. Tayari Mungu alishamjalia watoto wawili, nao walikuwa bado wadogo, mmoja miaka minne na mwingine miaka miwili.

Dada huyu pale alipokuwa anatembelewa na mama mkwe au mawifi alikuwa hapendi. Alikuwa haonyeshi ukarimu, ni kama vile anawaona mzigo nyumbani kwake. Hata kupika alikuwa akiwalazimisha wajipikie na kuwaonea kinyaa hadi waondoke.

Vituko kama hivi viliwaudhi sana ndugu wa mume ikiwamo wazazi wake. Dada huyu akasahau kuwa hawa ni wazazi na ndugu wa mumewe na bado wana wajibu wa kumtembelea kuwajulia hali na kupata misaada midogo midogo. Pia alipaswa kufahamu wakwe zake wanamchunguza, wanamfuatilia.

Vituko vilipozidi, upande wa wakwe wakaona kuwa bibie hawapendi na ndipo wakapanga njama ya kumnyamazisha. Unajua ushirikina bado upo sana katika baadhi ya familia hasa za vijijini.

Siku moja akatumwa wifi toka kijijini kuja kuweka kambi pale nyumbani kwa kaka yake. Mara nyingi mume wa bibie huyu yupo nje ya mkoa kikazi. Dada yake akavizia kaka yupo safarini akaja na kukaa siku kadhaa na wifi yake.

Kumbe alikuja na dawa wanazojua wao. Lengo kumchanganya bibie. Alipomaliza kazi yake, wifi akaondoka. Miezi miwili baadaye bibie akaanza kuumwa vitu visivyoeleweka. Akienda hospitalini madaktari wanasema hawaoni ugonjwa japokuwa walimpatia dawa za kutuliza maumivu.

Miezi mitatu baadaye, bibie huyu alipoteza maisha na kumwachia mumewe watoto wadogo. Ama kweli Maisha ndivyo Yalivyo. Mama huyu mwingine naye akasema yaliyompata rafiki yake yafaa kuyatafakari sana.

Naye ana viashiria vya tatizo kama la rafiki yake. Amekuwa haonyeshi changamko anapotembelewa na wakwe au mawifi zake. Hata mama mkwe anapompigia simu kumwomba fedha kidogo za matumizi kijijini humjibu hana japokuwa kiuhalisia anazo. Mumewe anasomesha baadhi ya watoto wa ndugu zake, jambo ambalo halipendi kabisa. Je, wakwe na ndugu wengine wa mume wakimfanyizia mabaya atamlaumu nani?

Kuwa mwangalifu na jitahidi kutunza nyumba yako kwani wao wanatafuta makosa yako. Usiwape nafasi kukukosoa. Wapende, wavumilie kwani pia ipo siku utakuwa mama mkwe. Wiki ijayo nitakumbushia zaidi uhusiano kati ya mke na mama mkwe, ndoa nyingi zipone! Una kisa? Ujumbe 0715268581.