Utafiti huo wa mwaka 2021, ulihusisha mikoa 26 ya Tanzania bara, shule 650 na wanafunzi 64,465 ambao ripoti yake ilitolewa mnamo Machi mwaka huu, ikielezea hali ya lishe ya wanafunzi wa shule za msingi nchini zilivyo.
Utafiti huo kimsingi, ulilenga kutathmini kiwango cha maambukizi ya malaria na utapiamlo miongoni mwa wanafunzi, ambao katika viashiria vya lishe, utafiti ukabaini kwamba wanafunzi waliopo katika shule za msingi bado wana changamoto nyingi za lishe zinazowakabili.
Mbali na hayo, watafiti hao pia wanaeleza kubaini wanafunzi wengi bado wana lishe duni, uzito uliopungua, uzito uliokithiri na upungufu wa damu kwa kiwango kikubwa.
Aidha wanataja shule nyingi zimezungukwa na maduka na vibanda vya wauzaji wadogo wadogo wa vyakula, lakini bahati mbaya ni kwamba, utafiti huo ulibaini kuwapo kwa vyakula ambavyo si rafiki kwa afya za wanafunzi.
Kwa matokeo hayo, ninadhani ingekuwa ni vyema matokeo ya utafiti huo yakafanyiwa kazi haraka, ili kulinda afya za watoto wa shule, kwani siyo siri, shule nyingi zimezungukwa na maduka na vibanda hivyo.
Pia, si maduka na vibanda pekee, kwani wapo baadhi ya mamalishe wanaokaanga mihogo na viazi katika maeneo ya shule na kuwauzia wanafunzi. Sidhani kama wote wanazingatia kanuni sahihi za afya kwa ujumla.
Kwa kuwa serikali imekuwa ikitoa mafunzo katika maeneo mbalimbali ikiwamo shuleni, ili kukabiliana na tatizo hilo la lishe duni, ninadhani pia ipo haja ya kutumia utafiti huo, ili kusaidia wanafunzi kuwa salama.
Mafunzo hayo yamekuwa yakitolewa kwa walimu wakuu wa shule za msingi na sekondari, kwa lengo la kuwajengea uelewa kuhusu elimu ya lishe bora katika shule zao.
Kwa kuwa mafunzo hayo yanalenga kusaidia walimu na wanafunzi kuwa na uelewa katika umuhimu wa lishe na kuwa mabalozi wazuri katika jamii, ninadhani kupitia ripoti hiyo, maeneo ya shule yanatakiwa kuuzwa vyakula ambavyo ni rafiki kwa afya za wanafunzi.
Ninaunga mkono juhudi hizo za serikali na wadau wake, hasa kutokana na ukweli kwamba lishe duni inasababisha madhara ya udumavu, upungufu wa damu, upungufu wa vitamini A, utapiamlo mkali, kupungua uzito au uzito uliokithiri.
Vilevile inaelezwa kuwa madhara ya lishe kwa wanafunzi ni pamoja na kiwango hafifu cha ufaulu, kutumia muda mrefu kuwafundisha, watoto kushindwa kuhudhuria masomo kila siku na magonjwa.
Hivyo basi, uamuzi huo wa kutoa mafunzo shuleni ni vyema uendelee kusambaa katika shule zote nchini, kwani suala la lishe bora lina changamoto kubwa inayohitaji ufumbuzi wa haraka.