Naam! Wewe sasa ni jemedari wetu, tunakutegemea utuvushe pale tulipo kwenda sehemu nyingine kimaendeleo, kiuchumi, biashara na mengine,tuko nyuma yako tukifuata nyayo.
Mkoa wa Mwanza una fursa nyingi hujawahi kuona,mfano kuna madini ya dhahabu,uvuvi wa samaki Ziwa Victoria, tuna ardhi yenye rutuba ya kutosha kwa kila aina ya kilimo cha mazao ya chakula na biashara.
Mfano ni kilimo cha pamba, mahindi, njugumawe, alizeti, choroko, kunde, mtama, viazi vitamu, nyanya, miwa, dengu, mpunga, mihogo na mengine mengi. Tatizo kubwa linalozorotesha shughuli za maendeleo na uzalishaji, ni usimamizi duni wa baadhi ya watendaji wetu, ambao wanasubiri mpaka wasukumwe.
Kuna haja ya watendaji kubadilika tabia, wajitume bila kusukumwa, kwa sababu kila mtu anatakiwa kuipenda kazi aliyoichagua,siyo ubabaishaji wakati wanalipwa mishahara itokanayo na kodi za wananchi. Kama ulichagua kazi hiyo, inapaswa uitendee haki.
Kwa ujumla, ni mkoa wa wafanyakazi, wakulima, wafanyabiashara, wafugaji, wavuvi, viwanda mbalimbali vilivyosheheni rasilimali za kutosha, zikiwamo vivutio vya visiwa, Hifadhi ya Taifa ya Saanane, iliyoko ndani ya Ziwa Victoria, milima na shughuli za uwekezaji.
Hakuna shaka wananchi wanaamini sasa fursa hizo zitawanufaisha zaidi, kwa usimamizi wako uliotukuka,wewe ni dhamana kwa kuwa serikali imekuamini, kwamba uje hapa kuwatumikia wananchi, ikiwamo kusikiliza shida za masikini. Tunaamini ofisi yako itakuwa wazi kwa ajili ya kuwahudumia wana Mwanza wote bila ubaguzi wa matabaka.
Mwanza imesheheni utajiri. Wapo watu wengine huenda wanaitamani kuwa ingekuwa kwao, sasa msamiati wa ‘mgeni njoo wenyeji tupone’unao ofisini kwako, tofauti na hapo itabadilika kuwa ‘mgeni njoo wenyeji tuumie.’ Tunajua ndiyo umeanza kufanya kazi mwishoni mwa mwezi ulioisha juzi.
Hili ni jiji maarufu Tanzania katika ukanda wa Kanda ya Ziwa na Afrika Mashariki kwa ujumla. Wengi wanatamani waje kujionea fursa zilizopo, kujua historia yake ya utalii uliopo ndani na mandhari zinazovutia kila kukicha.
Makalla wewe ndiye umeshika makali, ukitangulia vitani kupambana na majukumu,kero za mkoa zote ni zako. Mafanikio ya vyote vitakupa sifa, yetu ni macho na masikio tunakusubiri utekelezaji wako ututangulie na usituangushe kwa dhamana kubwa uliyopewa.
Zipo changamoto zinazowaumiza wananchi, ambazo zinatakiwa kusimamiwa,mfano ujenzi miradi ya barabara, masoko, kudhibiti ufujaji fedha za umma kwenye miradi, ambayo kimsingi ni kero kubwa kwa wananchi.
Yawezekana, mkuu wetu ukawa umekuja na mpango mkakati kabambe ambao utaibadilisha Mwanza kiuchumi, ikiwamo usafi wa mazingira, kumaliza kero ya machinga katika kuboresha masoko yao wanakofanyia biashara.
Tufahamu kila mahali hapakosi changamoto, misukosuko, migongano, lakini wewe kiongozi wetu umejaa hekima na busara, tunaamini utatuvusha tulipo, hatuna shaka wananchi wataungana nawe kusukuma zigo la maendeleo.
Pia, tunakukumbusha wana Mwanza kuwa kwenye ofisi yako usisahau kuwahamisha watumishi waliokaa muda mrefu bila kuhama, wengine wakiwa na zaidi ya miaka 10, ambao wameshajenga mazoea ya kimaslahi yao binafsi.
Wananchi hawahitaji mpaka wawanyoshee vidole kwamba watumishi hao wamewachoka, wanahitaji kubadilishwa vituo vya kazi, ili kama wamezoea kwenda kinyume na maadili ya kazi, ukiwamo ‘upigaji’ waende huko kwingine wakaumbuke, hata Waswahili wananena mazoea hujenga tabia.
Unafahamu binadamu hapendi kuambiwa ukweli. Katika hilo tunaikosoa serikali kuacha watumishi wa umma wakikaa miaka mingi wakilinda maslahi yao binafsi au maslahi ya nani? Wanawaumiza wananchi wengi ,kwanini hawahamishwi? Au wako pale mahsusi kwa ajili ya watu flani kulinda maslahi yao.
Makalla, jambo hilo limekuwa likilalamikiwa na wananchi hivyo hao waliokaa miaka mingi wachunguzwe kuna nini nyuma ya pazia?.