Pwani inang’aa miradi yote  kukubaliwa na Mwenge

31May 2023
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Pwani inang’aa miradi yote  kukubaliwa na Mwenge

HIVI karibuni, Mwenge wa Uhuru ulihitimisha mbio zake mkoani Pwani, ukiwa umepitia miradi 99 yenye thamani ya Shilingi trilioni 4.46 huku kukiwa hakuna hata mradi mmoja uliokataliwa.

Mkuu wa Mkoa huo, Alhaji Abubakari Kunenge, alitoa taarifa hiyo wakati akikabidhi Mwenge kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, ambaye alisema mkoani kwake, Mwenge ulitarajiwa kutembelea miradi 32 yenye thamani ya Shilingi bilioni 23.4. 

Ingawa inawezekana ipo mikoa ambayo Mwenge huo umepita na kukubali miradi yote ya maeneo hayo, lakini kwa mkoa wa Pwani ambao nimefanikiwa kusikia taarifa, unaweza kuwa ni wa kutolea mfano. 

Kwa nini? Kwa sababu imekuwa ni kama jambo la kawaida kuona kila mwaka Mwenge ukikataa baadhi ya miradi inayotekelezwa chini ya kiwango kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo rushwa. 

Labda nikumbushie kidogo kwa miaka iliyopita nikianzisha mbio za Mwenge huo za mwaka 2021 ambapo miradi 49 ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 65.3, ilikataliwa baada ya kutiliwa shaka kutokana na sababu mbalimbali zikiwamo ujenzi chini ya kiwango na kukosekana ukweli wa thamani halisi ya pesa. 

Hayo ni kwa mujibu wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Jenista Mhagama, katika kilele cha mbio hizo kilichofanyika Chato mkoani Geita mwaka huo. 

Katika taarifa yake, akafafanua kuwa miradi hiyo ni kwenye wilaya 38 katika ya wilaya 150 zilizotembelewa na mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huo wa 2021. 

Ukija katika hitimisho la mbio hizo mwaka jana mkoani Kagera, ilitolewa taarifa kuwa miradi 65 ya thamani ya Shilingi  bilioni 12 ilikataliwa baada ya kugubikwa na dosari ikiwamo, rushwa, uzembe na ubadhirifu. 

Taarifa iliotolewa mbele Rais Samia Suluhu Hassan na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Prof. Joyce Ndalichako, ilionyesha miradi 1,263 yenye thamani ya Shilingi bilioni 650 ilipitiwa na Mwenge huo mwaka jana. 

Kwa mazingira hayo, ni wazi kuna haja ya kujifunza jambo kutoka katika mkoa wa Pwani ili kuepuka kutumia vibaya fedha za walipa kodi na kukwamisha maendeleo ya nchi yao. 

Lakini pia ninadhani ipo haja ya kuwachukulia hatua za kisheria wanaohujumu miradi ya maendeleo, kwani bila kufanya hivyo, inawezekana maendeleo ya nchi yakazidi kusuasua. 

Itakumbukwa  Rais Samia Suluhu Hassan,  aliwahi kutoa maelekezo kwa Taasisi ya Kupambana na Kudhibiti Rushwa (TAKUKURU) na Mamlaka ya Kuzuia Rushwa Zanzibar ( ZAECA) kufanya uchunguzi na kuchukua hatua stahiki kwa wote waliobainika kufanya ubadhirifu wa fedha za umma kwenye miradi 65 iliyokataliwa na Mwenge. 

Rais pia alielekeza kila kiongozi kusimamia matumizi sahihi ya fedha zinazotolewa, kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa kuhakikisha inafanyika kuzingatia ubora kulingana na thamani ya fedha. 

Lakini akawataka Watanzania kuyaenzi mema yaliyoachwa na hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ikiwamo kukataa rushwa, uzembe na ubadhirifu wa fedha za umma.

Aidha, Rais aliwapongeza viongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kwa uaminifu na uzalendo walioonyesha, ikiwa ni pamoja na kuikataa miradi yenye mashaka na dosari mbalimbali.Mwaka jana, Mwenge wa Uhuru ulikimbizwa kwa siku 195 kwenye halmashauri 195 na kuweka mawe ya msingi na kuzindua miradi 1,263 yenye thamani ya Shilingi bilioni 650.