Vitendo vya rushwa, ndivyo vinavyochangia kukwamisha shughuli za maendeleo kwa mtu mmoja na jamii kwa ujumla, hivyo ni wazi kwamba rushwa ni adui wa haki, utu na heshima ya binadamu.
Kila mwaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), anapofanya ukaguzi na kutoa taarifa kwa umma, upigaji mwingi wa fedha za umma umekuwa ukidhihirika, katika taasisi za umma.
Kushamiri kwa rushwa, kuna chimbuko lake ambalo ni mmomonyoko wa maadili unaoanzia katika ngazi ya familia hadi taifa. Hivyo, ninadhani vita dhidi yake ingeanzia shuleni kwa wanafunzi kufundishwa somo la maadili.
Mmomonyoko ndiyo unaozaa maovu, ikiwamo kuenea kwa rushwa ambayo imekuwa sugu katika maeneo mbalimbali na kusababisha jamii kukosa haki, huku baadhi ya watoaji na wapokeaji wakiichukulia kama jambo la kawaida.
Wakati jitihada za kupambana nayo zikiendelea, ni wakati mwafaka wa kuwa na mitaala, kwa ajili ya somo la maadili, ambalo linaweza kusaidia wanafunzi kuitambua rushwa wangali wadogo, athari zake na kuiona kama adui wa maendeleo.
Nimaamini kuwa kupitia somo hilo, wanafunzi wanaweza kujua rushwa ni nini, ikiwamo ya ngono, fedha na vitu vingine badala ya kuisikia tu bila kujua maana yake na madhara yake na kujikuta wakijiingiza humo.
Wanafunzi wakipata elimu kuhusu rushwa na madhara yake, watakapokuwa watu wazima wataendelea kuichukia, kutokana na ukweli kwamba inakwamisha maendeleo yao na nchi kwa ujumla.
Hivyo, si vibaya ukawekwa mkakati maalumu wa kuanzisha somo hilo kwa shule za msingi hadi juu ili wanafunzi wapate elimu kuhusu rushwa, kwani ni miongoni mwa mambo ambayo yanachangia mmomonyoko wa maadili.
Ninaunga mkono juhudi mbalimbali ambazo zimekuwa zikifanywa za kupambana na rushwa ikiwamo za kuanzisha klabu za wapinga rushwa shuleni, ili wanafunzi wapate elimu ya madhara ya tatizo hilo.
Hatua hiyo ni nzuri kwa sababu inaweza kuandaa wanafunzi kupinga rushwa wangali wadogo hata pale wanapokuwa watu wazima wanaendelea kupambana nayo kwa manufaa yao na ya taifa kwa ujumla.
Lakini, wakati vita hii ikiendelea, suala la kuwa na somo la maadili ninadhani ni la muhimu, kwani linaweza kusaidia wanafunzi kutambua mambo mbalimbali yanayohusiana na maadili mema.
Kama nilivyoeleza, taarifa za kila mwaka za CAG, zimekuwa zikionyesha ubadhirifu wa fedha za umma, ujenzi wa miradi duni na vilevile kukosekana heshima kwenye matumizi ya fedha za walipakodi ambao wengi wanalalamikia ukosefu na upungufu kwenye huduma, hivyo ni muhimu kuwapo mikakati mbalimbali ya kuwaandaa vyema wanafunzi ikiwamo somo la maadili.
Kwa kawaida, viongozi na watumishi bora wa umma, huandaliwa tangu mwanzo, hivyo kuanzisha somo la maadili shuleni linaweza kusaidia kuandaa viongozi watakaoleta mapinduzi chanya ya maendeleo ya nchi.Utaratibu wa utoaji wa elimu kuhusu madhara ya rushwa kutolewa kuanzisha shule za msingi, ni mtazamo unaolenga kuhakikisha rushwa inaondolewa nchini kuanzia sasa na baadaye.
Maadili na uzalendo ni mambo yanayohitajika sana kujengwa upya na kuimarishwa ndani ya akili na mioyo ya watoto wa taifa hili kwa sababu kilichoziinua nchi kama China, Japan, Korea ni uzalendo na maadili hasa kufanyakazi.