Katika mabadiliko hayo yaliyotangazwa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dk. Moses Kusiluka, Rais Samia amewateua Luteni Kanali Patrick Sawala kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Paul Chacha (Tabora) na Daniel Chongolo ambaye aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwa mkuu mpya wa Mkoa wa Songwe.
Kabla ya uteuzi huo, Kanali Sawala alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Tandahimba wakati Chacha alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Misungwi.
Aidha, kutokana na uteuzi huo, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Kaban Thomas, na Dk. Frasic Michael wa Songwe uteuzi wao umetenguliwa. Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Waziri Kindamba, ameteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Mabasi Yaendayo Haraka (UDART).
MAONI YA WADAU
Mchambuzi wa masuala ya uchumi, Prof. Haji Semboja, alisema kitendo cha Rais Samia kufanya uteuzi mara kwa mara, kinaleta tafsiri ya kwamba anafuatilia na ana mfumo mzuri wa ufuatiliaji, kudhibiti na kufanya tathmini.
Alisema kuna wakati Rais anapanga timu yake kama timu ya mpira na huo ni kama mchezo wa kisiasa unaoashiria nia ya kubadilisha mfumo wa utendaji wa kazi.
“Unaweza ukaashiria kusema kuna matayarisho fulani ambayo yapo au kuweka timu ambayo itaweza kutimiza malengo ya kisiasa ambayo yamewekwa katika uchaguzi wa CCM. Ninakumbuka uchaguzi upo karibuni hayo ni mabadiliko ya kisiasa haina maana nyingine zaidi ya hayo,” amesema.
Prof. Semboja amesema wakuu wa wilaya ni marais wa wilaya na wakuu wa mikoa ni marais wa mikoa, hivyo Rais lazima awe na marais wake wa wilaya na mikoa ambao watatengeneza timu nzuri katika ushindi na kutekeleza mipango ambayo imewekwa katika chama.
”Si unaona katika mpira dakika za mwisho huwa wanabadilishana, waliotoka wameshamaliza mchezo wao na wamewaachia wengine kumalizia game (mchezo),” amesema.
Kuhusu uteuzi wa Chongolo kuwa mkuu wa mkoa, amesema bado alikuwa katika mfumo, hajatoka nje na alikuwa katika tawala za mikoa, hivyo ni mtu ambaye anarudi nyumbani kwake.
“Alivyojiondoa kwenye utawala wa kichama aliona kuna masuala mengine mazuri anaweza kuyafanya akiwa serikalini. Amempeleka serikalini atafanya vizuri pia katika hiyo nafasi,” amesema.
Mwanaharakati wa masuala ya kisiasa na kijamii, Bubelwa Kaiza, amesema tangu Rais Samia ameingia madarakani kazi yake kubwa ni kuteua kila wakati.
“Ninachokiona (huu) ni mwendelezo wa teuzi, ukichora chati, ukiangalia utendaji wake wa kazi ukiweka majukumu mbalimbali. Jukumu la uteuzi limekuwa juu zaidi kuliko majukumu mengine ukiangalia kuanzia mwaka 2021 hadi sasa kinachoonekana ni kuteua kila baada ya muda fulani,”amesema.
Kaiza amesema suala la kuteua ni jambo lililozoeleka na tafsiri yake ni kwamba, alivyoingia kwenye uongozi hakuwa amejiimarisha ndani ya chama.
“Aliingia akawakuta aliowakuta akateua. Anapowateua anataka wakatimize majukumu fulani, inaposhindikana anawaondoa ama kuwahamisha. Hili ndilo ninaliona. Angekuwa ameimarika ndani ya chama asingeona shida, angewajua anaowateua au mfumo mzima angekuwa anauelewa vizuri,” amesema.
Amesema kuteua, kutengua tafsiri yake anaowateua ni kwamba hakubaliani na kile wanachokifanya au hawatekelezi kama alivyotarajia.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Uongozi na Maendeleo ya Ujasiriamali (IMED), Dk. Donath Olomi, amesema Kampuni ya Mabasi Yaendayo Haraka (UDART) inatakiwa kuwa na menejimenti nzuri na watu wenye utaalamu wa kusimamia biashara ya usafirishaji.
“Wenye taaluma ya usafirishaji. Taaluma si tu kusomea, lakini kuna maarifa ya kuendesha mashirika ya usafirishaji makubwa. Si biashara ya kumchukua mtu yeyote na kumpeleka huyo aliyepelekwa katika hiyo nafasi sina CV (wasifu) wake simfahamu.
“Kiukweli shirika linahitaji uongozi au usimamizi wake uwe na watu ambao wanauelewa na hiyo biashara na haya mashirika yanahitaji kuwa na bodi. Mabadiliko mengi yanayofanywa na Rais huenda yakawa na sababu yake, labda kuna watu wamekaa sehemu muda mrefu anahitajika kutolewa na jambo jingine ni uchaguzi unaokuja, inawezekana watu wanapangwa katika kusimamia uchaguzi,” amesema.
MA- RC, MA- RAS WAHAMISHWA
Taarifa hiyo ilisema wakuu wa mikoa wanne wamehamishwa vituo vya kazi. Walioguswa na uhamisho huo na vituo vyao kwenye mabano ni Kanali Ahmed Abbas (Mtwara kwenda Ruvuma), Halima Dendego (Iringa kwenda Singida), Peter Serukamba (Singida kwenda Iringa) Dk. Batilda Buriani (Tabora kwenda Tanga).
Makatibu Tawala wa mikoa waliohamishwa ni Msalika Makungu (Mara kwenda Rukwa), Gerald Kusaya (Rukwa kwenda Mara), Albert Msovela (Kigoma kwenda Katavi), Hassan Rugwa (Katavi kwenda Kigoma), Rehema Madenge (Dar es Salaam kwenda Ruvuma), Stephen Ndaki (Ruvuma kwenda Kagera), na Toba Nguvila Kagera kwenda Dar es Salaam.
MA-DC WAPYA
Katika mabadiliko hayo, pia Rais amewateua wakuu wa wilaya watano. Wakuu hao na vituo vyao ni Abdallah Nyundo (Kilwa), Festo Kiswaga (Monduli), Kanali Alfred Mtambi (Mkinga), Almishi Hazali (Hanang’) na Joachim Nyingo (Kilolo)
Mbali na walioteuliwa, pia wamo waliohamishwa vituo ambao ni Deusdedit Katwale (Chato kwenda Tabora), Janeth Mayanja (Hanang’ kwenda Chamwino), Julius Mtatiro (Tunduru kwenda Shinyanga), Johari Samizi (Shinyanga kwenda Misungwi), Hassan Bomboko (Ukerewe kwenda Ubungo), Christopher Ngubiagai (Kilwa kwenda Ukerewe), Veronica Kessy (Iringa kwenda Mbulu), Heri James (Mbulu kwenda Iringa) na Paskasi Muragiri (Singida kwenda Bukombe).
Wengine ni Said Nkumba (Bukombe kwenda Chato), Simon Chacha (Sikonge kwenda Tunduru), Hashim Komba (Ubungo kwenda Geita), Cornel Magembe (Geita kwenda Sikonge), Peres Magiri (Kilolo kwenda Nyasa), Kasare Makori (Moshi kwenda Mbinga), Aziza Mangosongo (Mbinga kwenda Mafia), Zephania Sumaye (Mafia kwenda Moshi) na Luteni Kanali Michael Mtenjele (Tarime kwenda Tandahima).
Wamo pia Kanali Maulid Surumbu (Mkinga kwenda Tarime), Zainab Issa (Pangani kwenda Muheza), Faidha Salim (itilima kwenda Busega), Anna Gidarya (Busega kwenda Itilima) Gift Msuya (Chamwino kwenda Bahi), Godwin Gondwe (Bahi kwenda Singida) na Joshua Nassari (Monduli kwenda Magu).
WAKURUGENZI WAPYA
Rais Samia pia amewateua wakurugenzi wapya 10 wa halmashauri na kuwahamisha vituo wengine 25.
Walioteuliwa ni Dk. Rogers Shemwelekwa (Mji Kibaha), Masoud Kibetu (Manispaa Kahama), Dk. David Mkoga (Karagwe), George Mbilinyi (Bunda), Murtallah Mbuillu (Manispaa Ilemela), Vumilia Simbeye (Mji Kasulu), Jamal Abdul (Mlimba), Mashaka Mfaume (Mufindi) na Fred Milanzi (Uvinza).