Mgonjwa kuchagua daktari Muhimbili

17Mar 2024
Beatrice Shayo
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Mgonjwa kuchagua daktari Muhimbili

​​​​​​​HOSPITALI ya Taifa ya Muhimbili (MNH) imetangaza huduma mpya ambayo mgonjwa atakuwa na uwezo wa kumchagua daktari amtakaye kwa kujisajili kwa njia ya mtandao na kupanga naye muda wa matibabu.

​​​​​​​HOSPITALI ya Taifa ya Muhimbili.

Ofisa wa Kitengo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) Hospitali ya Muhimbili, Chindemba Lingwana, amesema huduma hiyo ni katika kuendana na kasi ya sayansi na teknolojia.

“Mfumo huu utamwezesha mgonjwa kufanya usajili na kumchagua daktari anayemtaka, kliniki anayotoka, huduma anayoitaka na kwa muda anaoutaka. Mfumo ni rahisi na ni rafiki kuutumia unaweza kuomba ukiwa hata nyumbani.

“Hii inasaidia kumpunguzia mgonjwa usumbufu wa kuja kusimama hospitalini. Mfumo huu ni salama na wa siri kumbukumbu zote za mgonjwa zinatunzwa kwa usalama, hataweza kuuona mtu mwingine,” amesema Lingwana.

Amesema ili mtu kupata huduma hiyo anatakiwa kutumia simu au kompyuta mpakato (laptop) na kufungua kivinjari (browser) na kuingia kwenye tovuti ya Hospitali ya Muhimbili.

“Ukiingia hapo kulia utaona Appointment utabonyeza itafunguka na njia ya pili ukiwa umefungua browser yako utaandika www.appointment.mnh.or.tz mfumo utafunguka na utaanza kujaza taarifa zako kwa kuandika jina lako la kwanza na la pili.

“Utaandika namba ya simu, utajaza email yako na kuchagua kliniki unayokwenda na kumchagua daktari na muda unaotaka kuonana naye kisha kutatuma,” amesema Lingwana.

Amesema baada ya hatua hizo mhusika (mgonjwa) atapokea ujumbe katika simu yake au kwenye email yake kumtaarifu kuwa taarifa zake zimepokewa.