Akifungua Mkutano Mkuu wa Wafugaji Nyuki wa Mkoa wa Singida ulioandaliwa na Kampuni ya Kijiji cha Nyuki, Pinda amesema chanzo cha sumu ya nyuki kuuzwa ghali ni kutokana na utafiti unaoendelea.
Katika mkutano huo pamoja na mambo mengine, wafugaji walipitisha rasimu ya mwisho ya kuundwa kwa umoja wa wadau wa nyuki Mkoa wa Singida na kugawiwa mizinga 500 na mavazi ya nyuki na kifaa cha kuvuna vumbi la Singida.
“Chanzo cha sumu ya nyuki kuuzwa ghali ni kwamba, kuna tafiti zinaendelea na zinaweza kuleta matunda itatibu kama sio kumaliza ugonjwa wa saratani na pili kuna kila dalili hii sumu ya nyuki ule ugonjwa wa UKIMWI inaweza kuwa kiboko yake,” amesema.
Pinda amesema kutokana na hali hiyo, hawapotezi muda katika kumlinda nyuki ili kunufaika naye kwa kuwa kwa upande wa afya ni chakula kizuri na ni fursa ya uchumi.
“Tumlinde sana mdudu nyuki na wataalamu wanatuambia nyuki wakipotea leo ghafla maisha ya mwanadamu yatabaki ya mwaka mmoja tu. Unabaki unaanguka utafikiri umerogwa ndiyo maana tunashauri tumia angalau kijiko kimoja cha asali kwa kuwa kuna kila aina ya chakula ndani ya asali,” amesema.
Pinda amesema dunia nzima inahangaika na mdudu huyo kwa kuwa vyakula vingi duniani ili kupata mbegu kunatakiwa kufanyike uchavushaji ambao unafanywa na nyuki, kwani kwenye mazao yote asilimia 90 yanamtegemea nyuki.
“Ukienda Ulaya nyuki wakipotea kidogo tu inakuwa kilio kwa maana bila nyuki hakuna chochote ndiyo maana dunia nzima inamwangalia nyuki kwa jicho kali,” amesema.
Ameongeza kuwa kutokana na mazingira mazuri yaliyoko Tanzania, ilistahili kuwa kinara wa uzalishaji wa asali duniani, lakini kiwango kinachozaliswa ni tani 35,000 tu.
Pinda amesema Tanzania imepewa heshima ya kuandaa mkutano mkubwa wa kidunia utaofanyika 2027 ambao utawashirikisha wadau zaidi ya 6,000 wa nyuki kutoka nchi 117.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kijiji cha Nyuki, Philemon Kiemi, amesema katika utafiti alioufanya wa miaka 12 amegundua mazao matano yanayotokana na nyuki tofauti na mwanzo ambapo wafugaji wa nyuki wanafahamu asali na nta tu.
Ametaja mazao ya nyuki mapya kuwa vumbi la Singida ambalo inasaidia nguvu za kiume na inauzwa Sh.laki 3 kwa kilo moja, maziwa ya nyuki yanauzwa Sh.milioni 12 kwa kilo,mkate wa nyuki Sh.300,000,gundi la nyuki Sh.milioni 3 na sumu ya nyuki ambayo inauzwa Sh.milioni 150 kwa kilo.
Kiemi amesema idadi ya makundi ya nyuki yaliyoko katika Mkoa wa Singida inafanana na idadi ya watu mkoani humo, lakini makundi yaliyoweza kukaa kwenye mizinga ni 240 tu na yaliyobaki yanakaa kwenye madari, mashimo, ardhini, magome ya miti, zahanati na shule.
“Niwaombe wananchi kuendelea kuweka mizinga ili kuwanusuru nyuki wasikae kwenye zahanati,shule na pia watu wasikate miti badala yake wapande miti ambayo inapendwa na nyuki.
“Tunaamini kuwa, kama wafugaji wa asili wakipata vifaa vya kisasa kama vile mzinga wa Singida Techno Heifer na kuvuna mazao mapya kama vumbi la Singida pamoja na kupata vifaa vya kujikinga na nyuki wakati wa kulina asali sekta ya nyuki itapaa na kuwainua wananchi wengi nchini kiuchumi,” amesema.
Kiemi amesema jukumu kubwa ambalo Kampuni ya Kijiji cha Nyuki inaendelea kulifanya ni kuwahakikishia wafugaji wa nyuki mkoani humo kuwa, soko la uhakika la asali na bidhaa zake zinapatikana ndani ya kijiji hicho.
Pia amesema lengo la kampuni ni kuwawezesha wafugaji wa nyuki wauze asali na bidhaa zitokanazo na asali kimataifa na wanapaswa kusajiliwa.
Kwa upande wao wafugaji wa nyuki waliiomba serikali kuangalia uwezekano wa kuwakopesha fedha zitakazowawezesha kununua mizinga ya kisasa pamoja na kuwatengea maeneo maalumu kwa ajili ya ufugaji wa nyuki.