Janabi aonya unyanyapaa dhidi ya wembamba

05Mar 2024
Christina Mwakangale
Dar es Salaam
Nipashe
Janabi aonya unyanyapaa dhidi ya wembamba

PROFESA Mohamed Janabi amesema mtu kuwa mwembamba haina maana kwamba ni mgonjwa, akionya unyanyapaa dhidi ya kundi hilo ambalo yeye ni sehemu yake.

PROFESA Mohamed Janabi.

Mkurugenzi Mtendaji huyo wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ametoa kauli hiyo wakati wa uzinduzi wa Mradi wa Afua ya Mfumo Jumuishi hospitalini huko.

Ni mradi unaofadhiliwa na Bill & Melinda Gates, ukilenga kuboresha na kuongeza mitaala inayofaa kwenye masomo yanayohusu afya katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS).

Mradi huo wa miaka mitatu unaotarajiwa kugharimu Sh. bilioni 2.347, pia unalenga kupinga unyanyapaa dhidi ya watu wanaoishi na Virusi vya UKIMWI (WAVIU).

Katika uzinduzi huo, Prof. Mohamed Janabi, amesema unyanyapaa upo hata miongoni mwa WAVIU, akieleza alivyoshuhudia hali hiyo wakati anatoa matibabu kwa kundi hilo.

Amesema kuwa alipokuwa anatoa matibabu kwao, wengi wao walimwona anafaa kuwatibu, wakiwakataa madaktari wengi kutokana na yeye (Janabi) kuwa mwembamba, hivyo kudhani naye huenda anaishi na VVU.

“Kilichonisikitisha, kwanini wagonjwa wengi wanaletwa kwangu pale ‘emergency’ (jengo la dharura) wakati huo ugonjwa huu ndio unashamiri nchini.

“Na dhana kuu ya jamii ilikuwa miongoni mwa wanaougua ni watu waliokonda au wembamba. Na mimi wakati huo nilikuwa mwembamba hasa.

“Nikavumilia ila siku nikamwuliza muuguzi mkuu ‘mbona wagonjwa wengi mnawapangia kwangu?’ Akasema wagonjwa wenyewe wanasema ‘wewe ni mwathirika mwenzao, wanakuwa na faraja zaidi ukiwatibu wewe’,” amesema Prof. Janabi.

Amesema unyanyapaa umeendelea kuwa tatizo la duniani licha ya kuwapo lengo la kutokomeza VVU na UKIMWI kufikia mwaka 2030.

“Mfano mwingine ni wa mwaka 2006, nikiwa Daktari Mkuu JKCI (Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete), tulishauriana ‘kwanini tusiende kupima hadharani sisi viongozi ili kuhamasisha wengine?’ Wote tulipima na Rais wakati huo na mkewe walifika.

“Tukaona takwimu zimeongezeka, waliojitokeza kupima kwa siku ni watu 70 na mwaka ule Tanzania ilikuwa na takwimu za idadi kubwa ya walioambukizwa VVU,” amesema Prof. Janabi.

Amesema jamii inapaswa kuendelea kuhamasika na kujitokeza kupima afya ili kufikia malengo ya dunia ya 95:95:95, akisema ripoti zinasema nchi kama vile Botswana, Eswatini, Zimbabwe zimefikia 95:95:95.

Kwa Tanzania changamoto ni katika asilimia 95 ya kwanza ya kutambua wanaougua. “Kisukari au VVU? Siku zote huwa ninawauliza wanafunzi wangu kwamba kati ya hayo magonjwa ukiwekewa mezani utachagua nini?

“Kwa sababu ukibainika una VVU utaanza tiba na masharti ukifuata utaishi, ila kisukari kuna wakati hakisikii chakula, masharti wala dawa, ninajua kama mtaalamu.

“MNH kwa kushirikiana na MUHAS tumeanzisha afua ya miaka mitatu ambayo inalenga kupunguza unyanyapaa na ubaguzi dhidi ya WAVIU, hasa katika maeneo wanayopokea huduma za afya, ikiwamo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili,” amesema.

Prof. Janabi amesema mradi huo utatekelezwa katika nchi tatu ambazo ni Tanzania kupitia taasisi tajwa, Zambia kupitia Taasisi ya ZAMBART na Ghana kupitia Taasisi ya Educational Assessment and Research Centre (EARC) na washauri wao Research and Triangle Institute International (RTI) kutoka Marekani.

Mradi huo utahusisha kuboresha mitaala sita ya vyuo vya afya vya kati nchini pamoja na kuboresha mitaala ya afua ya mfumo jumuishi kwa watumishi walio kwenye vituo vya afya.

Sambamba na uboreshaji wa mitaala, mradi utahusisha mafunzo kwa asilimia 70 ya watumishi walio katika vituo vya afya pamoja na ufuatiliaji na tathmini ya matokeo yatokanayo na afua hiyo.

Mgeni rasmi kati uzinduzi wa mradi huo, Mganga Mkuu wa Serikali, Prof. Tumaini Nagu, katika hotuba yake, iliyosomwa na Mkuu wa Programu kutoka Wizara ya Afya, Dk. Catherine Joachim, amesema “Mradi huu hapa Muhimbili ni fursa ya kuwaleta pamoja wadau mbalimbali nchini pamoja na kuongeza uelewa kuhusu mapambano dhidi ya maambukizi ya VVU.

“Ripoti ya kimataifa iitwayo ‘Njia ya Kumaliza UKIMWI’ inaonesha kuwa kumaliza UKIMWI ni uamuzi wa kisiasa, kifedha na nchi pamoja na viongozi wanaofuata njia hizo tayari wameshaona matokeo makubwa.”