Simba yaingia 'chimbo' kuiwinda Al Ahly

17Mar 2024
Adam Fungamwango
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Simba yaingia 'chimbo' kuiwinda Al Ahly

​​​​​​​BAADA ya kuifunga Mashujaa FC mabao 2-0 katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara iliyochezwa juzi kwenye uwanja wa Azam Complex, kikosi cha Simba kinatarajiwa kuingia kambini  leo kujiandaa na mchezo wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly ya Misri.

Simba itaanzia nyumbani Machi 29 kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa kujaribu kusaka tiketi ya kucheza nusu fainali ya michuano hiyo mikubwa zaidi kwa ngazi ya vilabu Barani Afrika.

Akizungumza mara baada ya mchezo wao dhidi ya Mashujaa, Matola amesema wakati kukiwa na mapumziko ya kupisha michezo ya kimataifa ya kalenda ya FIFA, wachezaji wakienda kwenye timu za taifa, kwao hakutakuwa na mapumziko, badala yake wataingia kambini kujiandaa na mchezo huo wa CAF.

"Kuna mapumziko,  lakini sisi Simba hakuna mapumziko kwetu, tunakwenda kujiandaa na mechi ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, wachezaji wetu wanarudi majumbani, lakini kesho (leo), tutaanza rasmi kambi," amesema Matola.

Akizungumzia mchezo wa juzi dhidi ya Mashujaa, Matola amesema haukuwa mchezo mwepesi, iliwabidi kupambana hasa kipindi cha pili na kubadilisha mbinu za mchezo zilizowasaidia kupata mabao hayo mawili.

"Kipindi cha kwanza Mashujaa walikuwa na nidhamu, walirudi nyuma wote, kwetu sisi tulikosa mikimbio kule mbele ili kutengeneza nafasi, lakini kipindi cha pili alipoingia Onana na Saido (Ntibazonkiza) kusisimama kati namba tisa kulitusaidia kuwafungua, tukapata nafasi tukazitumia, kwa hiyo naweza kusema kuwa kipindi cha pili mikimbio yetu ilibadilika," amesema.

Matola pia amefurahi timu yake kutoka uwanjani bila kuruhusu bao na kumfanya kipa Ayoub Lakred kufikisha 'clean sheets' ya tano kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara mpaka sasa.

"Leo tuna furaha hatujaruhusu bao tumetoka na 'clean sheet', kipa wetu Ayoub amefanya kazi kubwa sana pamoja na mabeki wake, tulikuwa tunaumiza sana kichwa kwa sababu mechi tatu mfululizo tunafungwa bao, inaonyesha kile tunachokifanya kwenye uwanja wa mazoezi kimeanza kufanya kazi," amesema kocha kiungo huyo wa zamani wa klabu hiyo.

Aidha mfungaji wa mabao yote ya juzi, Clatous Chama, akiwa sasa amefikisha jumla ya mabao sita, amesema kipindi cha kwanza hawakuwa watulivu mpaka pale kocha wao Abdelhak Benchikha alipowapa maelekezo nini cha kufanya kipindi cha pili.

"Mechi ilikuwa ngumu, kipindi cha kwanza hatukuwa na utulivu kwenye boksi la wapinzani wetu, kipindi cha pili baada ya kocha kutupa maelekezo ya nini cha kufanya, tukafanikiwa," amesema.

Akizungumzia kipigo hicho cha juzi, Kocha Mkuu wa Mashujaa, Mohamed Abdallah 'Bares' amesema mabeki wake walifanya makosa ya kizembe dakika 17 za mwanzo wa kipindi cha pili yaliyobadilisha matokeo ya mchezo mzima.

"Ni makosa tuliyoyafanya tukiwa katika eneo letu la ulinzi, tumecheza na timu yenye wachezaji ambao wanaweza kuamua matokeo wakati wowote. Unapocheza na timu kubwa kama Simba wachezaji wako wanatakiwa kuwa makini wasiruhusu makosa ya kizembe na hicho ndicho tulichokifanya dakika 17 za mwanzo za kipindi cha pili tukaadhibiwa," amesema.

Matokeo hayo ya juzi yanaifanya Simba kufikisha pointi 45 na kupanda mpaka nafasi ya pili kwenye msimamo huku Mashujaa wakibaki katika nafasi ya 12 wakiwa na pointi zao 21.