Yanga kuendeleza ubabe leo Ligi Kuu?

14Mar 2024
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Yanga kuendeleza ubabe leo Ligi Kuu?

​​​​​​​KIKOSI cha Yanga leo kinatarajiwa kushuka kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi kukabiliana na Geita Goldi kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi.

Mchezo huo umepangwa kuanza saa 2:00 usiku huku macho ya mashabiki na wadau wakitaka kuona kama mabingwa hao watetezi wataendeleza kasi ya ushindi kwenye michezo ya Ligi Kuu.

Yanga itakabiliana na Geita Gold siku chache ikitoka kupata ushindi mnono wa mabao 5-0 dhidi ya Ihefu kwenye uwanja huo huo huku Geita ikitoka kupata ushindi wa bao 1-0 ugenini dhidi ya Dodoma Jiji FC katika uwanja wa Jamhuri, Dodoma.

Kuelekea mchezo huo Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi  amesema wamefanya maandalizi mazuri kuwakabili Geita Gold katika mchezo huo muhimu.

Amesema haijalishi watapata ushindi wa idadi gani ya mabao kikubwa wanahitaja pointi tatu.

“Bado sina uhakika wa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu licha ya timu yangu kuendelea kupata alama tatu, baada ya mchezo na Ihefu mara moja tukaanza kujiandaa na mchezo huu, naamini tutafanya vizuri," amesema Gamondi.

Wakati Gamondi akisema hivyo, Kocha wa Geita Gold, Denis Kitambi amesema wameifuatilia Yanga kwenye michezo yao ya hivi karibuni na kujiandaa kuwakabili.

Amesema wamefanya maandalizi ya namna gani ya kuweza kujilinda na kushambulia katika mchezo wa leo kulingana na namna wapinzani wao watakavyokuja.

“Kwa jinsi ambavyo Yanga wanavyocheza Aziz Ki (Stephane) ndio tatizo la kwanza tuliloaanza kulifanyia kazi wakati wa maandalizi yetu,  lakini pia kuna Mudathiri (Yahya) ambaye mara nyingi amekuwa akitokea nyuma, anacheza kiungo lakini anajukumu kubwa la kushambulia, hawa wote tunatakiwa kuwachunga," amesema Kitambi.

Anasema wamejiandaa kukabiliana na wapinzani wao hao na kuhakikisha wanaondoka na pointi.