Dendego ambaye amehamishiwa mkoani hapa kutoka Iringa, amesema hayo alipokuwa akizungumza na watumishi baada ya kukabidhiwa ofisi na mtangulizi wake, Peter Serukamba, ambaye amehamishiwa Iringa.
Amesema ni lazima kazi zifanyike na majibu yapatikane kupitia utumishi huku akisisitiza atakuwa msikivu, mnyenyekevu na mtulivu katika kuongoza na kusimamia shughuli za maendeleo ya mkoa.
Awali, Serukamba amezishukuru kada mbalimbali za uongozi tangu alipowasili mkoani Singida mwaka mmoja na miezi saba iliyopita na kusema amejifunza mengi ya maendeleo atakayoyaendeleza alikohamishiwa.
Amesema akiwa Singida anajivunia kupandisha matumizi ya mbolea ikilinganishwa na hali aliyoikuta, huku pia akifanikisha upatikanaji wa mbegu ya ruzuku ya alizeti.
Serukamba amesema anajivunia kumaliza tatizo la mauaji lililoikabili wilaya ya Manyoni ambalo lilikithiri nyakati za usiku kwa ufukuaji wa makaburi kutokana na imani za kishirikina.
Akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Singida, Katibu Mwenezi wa CCM Mkoa, Eliphas Lwanji, ameahidi kuwa chama CCM na serikali ya mkoa kumpa ushirikiano wa kutosha mkuu huyo mpya wa mkoa ili atekeleze majukumu yake kwa ufanisi.