Waziri ahimiza usimamizi fedha miradi

14Mar 2024
Ibrahim Joseph
DODOMA
Nipashe
Waziri ahimiza usimamizi fedha miradi

WAZIRI wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba, amewasisitiza wasimamizi wa miradi yote ya ujenzi ya serikali inayotumia utaratibu wa ‘force account’ kuimarisha usimamizi ili wazawa wapate nafasi ya kumiliki uchumi.

WAZIRI wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba.

Dk. Nchemba ametoa agizo hilo kwenye hafla ya kuweka jiwe la msingi la Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) Tawi la Dodoma, jijini hapa.

Amewataka wasimamizi hao wa miradi kuimarisha usimamizi wa fedha zote za miradi hiyo zinazotolewa na serikali ili kuwanufaisha wazawa na kukuza uchumi wa nchi.

“Nimepewa taarifa hapa kuwa mnatekeleza ujenzi wa miradi yenu yote kwa kutumia ‘force account’ na imeonyesha mafanikio. Nawataka  wasimamizi wote wa miradi yote nchini kusimamia fedha hizo vizuri ili kuwawezesha wazawa kiuchumi,” alisema.

Pia amesema miradi hiyo inayotekelezwa na chuo hicho kama wangetumia makandarasi, fedha zingetumika nyingi tofauti na zile zilizotumika kujenga majengo hayo.

Chuo hicho, amesema kimeonyesha utaratibu huo unavyoweza kutekelezwa na kuipunguzia serikali gharama za ujenzi. Pia aliwataka wasimamizi hao kuhakikisha majengo yanakuwa na thamani halisi ya fedha za walipakodi zilizotumika.

Awali, Mkuu wa Chuo hicho, Prof. Eliaman Sedoyeka, amesema chuo hicho ambacho makao makuu yake yako Arusha, kina matawi matatu ambayo ni Dodoma, Babati na Dar es Salaam na wanatarajia kufungua tawi lingine mkoani Ruvuma.

Prof. Sedoyeka amesema chuo hicho kilifungua tawi Dodoma mwaka 2021 na wamekuwa wakitumia majengo ya kukodi lakini wameona umefika muda wa kujenga jengo lao ili kupunguza gharama za uendeshaji.

Kwa mujibu wa Prof. Sedoyekam jengo hilo litatumia Sh. bilioni 5.08 na litakuwa na ghorofa sita. Hadi sasa, alisema Sh. bilioni 1.7 zimetumika kugharamia ujenzi huo.

Ameongeza kuwa chuo kimejenga na kinaendelea na ujenzi wa majengo mengine katika kampasi kuu Arusha na tawi la Babati na Sh. bilioni 48 zimetengwa kwa ajili ya kazi hiyo.

Prof. Seoyeka amesema hivi sasa wanakabiliwa na tatizo la kupata eneo la chuo kwa Dar es Salaam ili kujenga majengo ya kudumu na kumwomba waziri kuwasaidia kupata eneo kwa sababu fedha za kujenga zipo.