FCC yaonya wananchi wanaokopa kausha damu

12Mar 2024
Faustine Feliciane
Dar es Salaam 
Nipashe
FCC yaonya wananchi wanaokopa kausha damu

​​​​​​​WAKATI wakijiandaa kufanya maadhimisho ya Siku ya Haki kwa Mlaji Duniani, Tume ya Ushindani (FCC), imewaonya wananchi kuacha kuchukua mikopo kwa taasisi au watu binafsi bila kujua masharti ya mkataba.

Akizungumza jijini Dar es Salaam  wakati wa uzinduzi wa maadhimisho hayo ambayo kilele chake ni Machi 15, Mkurugenzi Mkuu wa FCC, William Erio, amesema mikataba yote ya mikopo lazima iandikwe kwa lugha inayoeleweka kwa mkopaji, lakini mhusika anapaswa kuelewa na kukubali vipengele vya mikataba hiyo.

Amesema FCC inawashauri wananchi kuchukua mikopo kwenye taasisi zinazotambulika ili kuepuka kutepeliwa na kuingia makubaliano ya mikopo yenye kuwakandamiza.

"Katika maadhimisho ya siku ya haki ya mlaji duniani, FCC tunaendelea kutoa elimu kwa wananchi kujua haki zao, lakini pia suala la mikopo ya kausha damu tunawashauri wananchi kujua haki zao, suala la mikopo na maamuzi ya mtu mwenyewe hivyo lazima waangalie na kuulewa mkataba wa kukopeshana," amesema Erio.

Amesema katika maadhimisho ya mwaka huu ya siku ya haki ya mlaji, kaulimbiu ni 'matumizi akili mnemba yanayozingatia haki ya mlaji.'

Aidha, amesema kuelekea kwenye maadhimisho hayo, FCC wameandaa kliniki kwa ajili ya kutoa elimu kwa wananchi Machi 13, mwaka huu, pamoja na kusikiliza na kutatua changamoto katika ofisi za mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma, Mbeya na Mwanza.

"Baada ya hapo Machi 15 sasa ndio itakuwa kilele cha maadhimisho haya na tunatarajia Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Ashatu Kijaji, atakuwa mgeni wetu rasmi na atatoa neno kwa wananchi.

"Niwakaribishe wananchi wote kwenye kilele cha maadhimisho haya, lakini niwaombe wananchi kufuatilia taarifa zetu za kuelimisha juu ya haki za mlaji, FCC tunaendelea kutoa elimu kupitia njia ya redio lakini tunaendesha semina kwa wadau ili kujua namna mlaji anapaswa kulindwa," amesema Erio.