Mfukumuko wa bei waleta ahueni mwezi Februari

14Mar 2024
Rahma Kisilwa
ZANZIBAR
Nipashe
Mfukumuko wa bei waleta ahueni mwezi Februari

KASI ya kiwango cha mfumko wa bei kwa mwaka ulioishia Februari 2024, imeshuka hadi asilimia 5.10 kutoka asilimia 5.26 iliyorekodiwa Januari 2024.

KASI ya kiwango cha mfumko wa bei kwa mwaka ulioishia Februari 2024, imeshuka hadi asilimia 5.10 kutoka asilimia 5.26 iliyorekodiwa Januari 2024.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Kitengo cha Takwimu za Bei Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Salma Saleh Ali, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, Mazizini jana.

Amesema, kushuka kwa kiwango cha mfumko kulichangiwa zaidi na kushuka kwa bei za bidhaa za vyakula na vinywaji visivyo na vileo kwa asilimia 8.66 Februari 2024 ikilinganishwa na asilimia 8.98 mwezi Januari.

Amesema, faharisi za bei zimeongezeka kufikia 109.53 mwezi Februari 2024 ikilinganishwa 104.22 Februari, 2023.

Aidha, mfumko wa bei wa bidhaa za chakula wa mwaka ulioshia Februari 2024 umepungua na kufikia asilimia 8.88 ikilinganishwa na asilimia 9.21 iliyorikodiwa mwezi Januari 2024.

Amesema, faharisi za bei za chakula kwa mwezi Februari 2024 ziliongezeka na kufikia 116.83 kutoka 107.30 katika mwezi Januari 2023.

Mfumuko wa bei wa bidhaa zisizo za chakula kwa mwaka umepungua na kufikia asilimia 2.40 kwa mwezi Februari 2024 ikilinganishwa na asilimia 2.46 katika mwezi wa Januari 2024.

“Faharisi za bei za bidhaa zisizo za chakula zimeongezeka na kufikia 104.56 kwa mwezi Februari 2024 ikilinganishwa na asilimia 102.11 katika mwezi Februari 2023.

Amezitaja bidhaa zilizosababisha kupungua kwa mfumuko wa bei ni pamoja na mchele wa Mbeya (11.0%), unga wa ngano (4.2%), unga wa sembe (5.5%), ndizi za mtwike (25.5%), na mafuta ya kula (6.7%).

Meneja Msaidizi, Uchumi Benki Kuu, tawi la Zanzibar, Shami Chamicha, amesema kupungua kwa kasi ya mfumuko wa bei ni hatua nzuri ya kiuchumi na malengo yaliyopo ni kubakia kwenye tarakimu moja.

"Ni ahueni kwa wananchi na hii inatokana na kuwapo kwa bidhaa za kutosha kwenye masoko. Lakini kwa ujumla hali ya uchumi imeendelea kubakia vizuri na hata upatikanaji wa dola hivi sasa upo vizuri," amesema.

Mchumi Mkufunzi Mwandamizi Skuli ya Biashara, Dk. Estella Ngoma Hassan, amesema kushuka huko kwa kiwango cha mfumuko ni hali ya kawaida kulingana na mwenendo wa kibiashara.

Aidha, amesema kuwapo kwenye tarakimu moja ni njia bora ya kuwavutia wawekezaji kwa ajili ya kuwekeza nchini kwa maendeleo ya taifa.

Mfumuko wa bei wa Zanzibar ni kipimo kinachotumika kupima mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma mbalimbali zinazokusanywa katika masoko ya miji ya Zanzibar.