Baadhi ya mambo yaliyoibuka katika mjadala huo wabunge kupinga kikatwa asilimia tano ya kodi kwenye kiinua mgongo baada ya miaka mitano, waliligomea pia ongezeko la tozo la pikipiki, kupunguziwa fedha kwa Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na kuhitaji kuongezewa fedha maeneo mengine.
Yapo pia masuala ya tozo katika huduma za utalii ambazo kwa kiasi kikubwa zitachangia kupunguza idadi ya watalii na kuruhusu nchi jirani kutumia mwanya huo kujipatia fedha kwa kutumia vivutio vya Tanzania huku zikijipatia watalii wengi zaidi.
Sehemu nyingine ambayo imegusa moja kwa moja maslahi ya Watanzania na ambayo wabunge waliipa msisitizo na hata kamati ya bajeti kusisitiza huku serikali ikiogopa kwa madai ya kukwepo mfumuko wa bei ni ongezeko la Shilingi 50 kwenye mafuta ili zielekezwe kwenye mfuko wa maji vijijini.
Wabunge hao walisema wananchi vijijini wanateseka kwa kukosa huduma muhimu ya maji huku serikali ikiwa imejiwekea malengo kuwa ifikapo 2020 kila mwananchi atapata huduma hiyo umbali usiozidi mita 400.
Waheshimiwa walitumia muda mrefu kufafanua hoja hiyo, walisema wana hakika haitakuwa na madhara wala mfumuko wa bei kwa kuwa umepungua kutoka asilimia sita hadi tano, na watawaelewesha wapiga kura wao kwa kuwa kinachofanyika ni kwa faida yao.
Katika bajeti ya mwaka 2015/17 Bunge liliridhia nyongeza ya Sh 100 kwa kila lita ya petroli na deseli pamoja na Sh 150 kwenye mafuta ya taa ili fedha ambazo serikali iliahidi kuzihifadhi kwa ajili ya kusambaza umeme vijijini zipatikane.
Malalamiko ya wabunge kwa sasa ni kuwa serikali ilimega fedha hizo na kusambaza maji mijini na hivyo umeme haukufika maeneo yote kama ulivyotarajiwa.
Wakati wa mjadala wa bajeti hiyo baadhi ya wabunge wa chama hicho walipinga vikali kwa kueleza kuwa itachangia mfumuko wa bei na kuwaacha wananchi katika mateso makubwa huku wengine wakidai itasaidia wapate umeme ili kurahisisha shughuli zao.
Mwananchi huyu ambaye ni pamoja na mimi amejikuta akisemewa mengi na mengine ambayo ni maumivu kwake lakini kwa vile tu kuna mwakilishi wake ambaye hukumu yake husubiriwa kutolewa miaka mitano baadaye kwa aidha kuchagua mbunge mwingine au kumuacha aliyepo aendelee.
Wabunge hawa hawa wameguswa kwenye mafao yao wamekuwa wakali sana kwa madai kuwa wao ni kama mashine za kutolea pesa -ATM kwenye majimbo yao, kwa siku anapokea zaidi ya simu 30 za wapiga kura zikiomba fedha za mahitaji mbalimbali, na fedha hiyo ni sawa na posho tu na kumtaka Waziri wa Fedha na Mipango kugombea jimboni 2020 ili kuona machungu ya jimbo.
Wakati wanajitetea kwa hoja hiyo inapokaribia uchaguzi mkuu wengi hukaribia kutoana roho kwenye majimbo, sasa ‘Nawaza kwa Sauti’ ni kweli wote wana nia ya dhati ya kufanya kazi ya kujitolea kama wanavyadai, kwanini mpambano kwenye majimbo unakuwa mkali kiasi cha kutishiana maisha kama ni kutaka kutumikia umma pekee kwa kujitolea?
Nakubaliana nao kuwa wananchi wa mijini na vijijini kuna shida ya maji, maeneo ya mijini yanaonekana yana afadhali kubwa kwa kuwa kuna baadhi ya miradi ya maji lakini taabu ipo na inaathiri wananchi kiasi cha kutumia maji ambayo hushirikiana na wanyama wa kufuga na wa porini.
Mathalani, Jiji la Dar es Salaam lina shida kubwa ya maji ambayo kwa kiasi kikubwa imekwaza maendeleo ya kiuchumi, na maji yanayotumika ni ya visima ambayo si salama.
Vijijini wengi wanatumia maji ya chemchem na visima wanayafuata umbali mrefu, hivyo kama nia ya kuwasaidia wananchi wa kawaida ni lazima wabunge nao wakubali kuvuja jasho na siyo wananchi pekee, kama ni kujitolea waanze sasa.
Ningefurahi zaidi kusikia wamekubali kukatwa kodi hiyo ambayo itaipatia serikali Shilingi bilioni 4.5 kwa ajili ya kupeleka huduma ya maji kwenye kata au vijiji, na ndipo kuwepo ongezeko la Shilingi 50 kwenye lita ya mafuta kusaidia jitihada zao.
Lakini , za kwao hawataki ziguswe ila zigo liwaangukie wananchi ambao athari zake zitaonekana kwenye usafiri wa umma na kusafirisha mazao kwa kuwa hakuna mfanyabiashara ambaye atakubali kupata hasara bali kupandisha bei ili aweze kufidia faida anayotarajia.
Hata kama, mfumuko wa bei kwa sasa uko asilimia tano, lakini bado mafuta yana athari ya moja kwa moja kwa mwananchi wa kawaida, hivyo wawakilishi hao wafike mahali waache ubinafsi, kuwa jambo likiwagusa wanakuwa wakali na kupinga kwa kuwa wako kwenye nafasi ya kujitetea na hata kuigomea bajeti ya serikali, lakini wananchi wasioweza kugoma kwa sasa wanarushiwa mzigo huo.
Waiunge mkono serikali ambayo imejinasibu kuwa inatumikia wanyonge na itahakikisha maskini anafurahia mgao wa keki ya taifa.
Tutafakari
Kwa maoni kitomari.salome@guardian.co.tz










