Maxime ajivika taji kocha bora wa miaka mitano

19Jun 2016
Lasteck Alfred
Lete Raha
Maxime ajivika taji kocha bora wa miaka mitano

KOCHA wa Mtibwa Sugar, Mecky Maxime amedai kuwa kwa miaka mitano sasa yeye ndiye kocha bora nchini.

Sababu? Anasema kuwa amezalisha wachezaji bora wengi zaidi ya kocha wote na kwamba usajili wa nyota wengi kutoka Mtibwa unapaswa kumvika taji la kocha bora.

Lakini umeshawahi kujiuliza ni wachezaji gani wa zamani ambao wakati wanacheza soka walinyakua ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania bara na baada ya kustaafu soka wakatwaa pia taji hilo kama makocha? Basi, majibu ni mawili tu -- Charles Boniface Mkwasa na Fred Felix Minziro, wote wakiwa na Yanga. Sasa anayetaka kuwamo kwenye orodha hiyo kwasasa ni kocha Maxime ambaye amesema kuwa hataondoka Mtibwa hadi aweke rekodi ya kutwaa taji la Ligi Kuu Bara na timu hiyo akiwa kama kocha.

Kocha huyo alikuwapo katika kikosi cha Mtibwa kilichotwaa ubingwa wa Ligi Kuu 2000 na 2001, hivyo akifanikiwa kutwaa taji la ligi kwa sasa atakuwa kocha wa kwanza anayefundisha timu nje ya Dar es Salaam kuwa na rekodi ya kutwaa akiwa mchezaji kisha kama kocha.

Maxime anasema angependa kuiona rekodi hiyo ikitimia msimu huu au misimu minne ijayo. “Kama kocha napenda kuona ninaweka rekodi hiyo, najua inawezekana licha ya kwamba kuna changamoto kubwa za hapa na pale kubwa zaidi ikiwa ni usajili kwa maana ya kuondokewa na wachezaji wengi kila kipindi cha usajili kinapofika."

Katika mahojiano maalum na Lete Raha, kocha huyo ameelezea anavyosajili na jinsi nyota wanavyoondoka kwenye timu hiyo.

Anavyowauza wachezaji

Kwanza anasema, “Ninajiona kama kocha bora kwani mimi ndiye ninayezalisha mastaa wengi kwenye Ligi Kuu. Pia mimi ndiye ninayetengeneza kikosi cha timu ya taifa (Taifa Stars) kwa kutafuta wachezaji, kuwatengeneza na kuwafanya wahitajike na timu nyingine.
“Kwanini ninajiita kocha bora?

Kwasababu mimi ni kama mwalimu, ninafaulisha wanafunzi wengi na kuwafaulisha wengi. Ndiyo maana Mtibwa ndiyo timu inayouza wachezaji wengi zaidi katika kila dirisha la usajili.

“Kwa misimu mitano wachezaji wetu 45 wakiwa kwenye viwango vya juu walihama Mtibwa na kujiunga na timu nyingine na siamini kama kuna klabu inafikia rekodi hii. Unafikiri inatokana na nini? Jibu ni kuwatunza na kuwapa maelekezo mazuri,”anasema huku akisema kuwa kazi anayofanya si ya kulinganishwa na kocha mwingine.

Anawatengenezaje?

Beki huyo wa zamani wa Mtibwa anasema, “Mimi ninafanya kazi yangu kwa juhudi na kwa kuwaelewa wachezaji. Pia ninaishi nao vyema kwa kuwasimamia vyema. Ninawapa uhuru pale inapohitajika na ndiyo maana wanakuwa tayari wakati wanapoitajika kupambana.”

Wakishindwa wanarudi
Anasema kuwa kwanza wachezaji wake wanapoenda kwenye timu nyingine wanakutana na changamoto kuu mbili ambazo ni wao kutojitambua kwenye baadhi ya mambo, lakini pia wanaowachukua hawawaelewi wachezaji wa Kitanzania wanavyotakiwa kuongozwa.

“Aina ya ufundishaji wa makocha wengine ni changamoto, lakini wachezaji wenyewe wakati mwingine hawajitambui na wale wanaowafundisha hawatambui hilo, hivyo wanashindwa kuwasaidia,” anasema.

Usajili wa kuwanufaisha

Anasema, “Hatuwezi kumzuia mchezaji kwenda popote kama ana uwezo wa kwenda kupata kitu kizuri aendako. Nina maana ya fedha. Tunamruhusu kwani maisha ya sasa yanahitaji fedha kujiendesha.

“Zamani tulisajiliwa kwa Sh. milioni 10, sasa wachezaji wanapata hadi Sh. milioni 40. Fedha ndizo zitakazowapa mwelekeo wa maisha ya baadaye.”

Anaibua mchangani

Kocha huyo anasema kuwa mbali na kuchukua wachezaji walioachwa na timu nyingine, wachezaji wengine huwa anawapata kwenye soka la mchangani.

“Kuna vipaji vingi, makocha wengi VPL ni wavivu na wanataka wachezaji ambao tayari wameshatengenezwa. Tofauti yangu na wengi ni kuwa mimi na benchi langu la ufundi huwa tunaenda hadi mtaani kusaka vipaji. Wakati mwingine tunafuatilia wachezaji wa Ligi Daraja la Pili.

“Angalia mchezaji aliyesajiliwa Yanga, Andrew Vincent ‘Dante’, anacheza michuano ya kimataifa sasa, lakini misimu miwili iliyopita nilimtoa kwenye Ligi Daraja la Pili. Wengine ni kama Shiza Kichuya ambaye kwasasa yuko sokoni akihitajika na Simba pamoja na Azam.

“Kiukweli kama kila kocha angekuwa anaingia mtaani na kutafuta wachezaji, timu yetu ya taifa na soka letu kiujumla vingefika mbali,” anasema.

Aliumia kuondoka Luizio, Awadh Juma

Anasema kuwa alifurahi kuwa wachezaji hao walipoondoka kusaka maisha mazuri, lakini kiufundi kama kocha aliumia kwani alikuwa akiwategemea na kwa uwezo waliokuwa nao imekuwa ni ngumu kupata wachezaji wa aina hiyo.

“Wapo wengi ambao sikupenda waondoke lakini Juma Luizio aliyeenda Zesco United ya Zambia aliniumiza kiasi fulani kutokana na umahiri wake. Pia uwezo wa kiungo Awadh Juma wa kucheza nafasi tofauti kwa kiwango cha juu ulinifanya niumie baada ya Simba kumsaini.

Kocha huyo pia alibainisha kuwa hakufurahi wakati ule alipomuachia straika Hussein Javu ambaye alitua Yanga na kutoweza kudumu kwa kipindi kirefu ndani ya kikosi hicho.

Nidhamu ya wachezaji wake

Katika msimu uliomalizika, hakuna mchezaji wa timu hiyo aliyeadhibiwa kwa kadi nyekundu, lakini katika msimu wa 2014/15, kiungo Henry Joseph ‘Shindika’ pekee ndiye aliyepata kasi nyekundu iliyotokana.

Maxime anasema, “Nidhamu bora ya wachezaji inatokana na jinsi kocha unavyowataka wachezaji wawe. Mimi huwa naamini nidhamu ndiyo inayotupa mafanikio hivyo wachezaji wangu huwa ninawahimiza kuheshimu kazi yao ndani na nje ya uwanja.”

Rushwa na upangaji matokeo

Baada ya kuwapo maneno ya hapa na pale kuwa Mtibwa huwa wanasaka pointi nyingi mwanzoni mwa msimu kisha kwenye hatua za lala salama wamekuwa wakipanga matokeo kwa kufungwa, Maxime anasema, “Mwanzoni mwa msimu timu zote hucheza kwa kushinda au kupoteza kwa haki kwasababu ni mwanzo wa msimu, lakini mzunguko wa pili unapoanza huwa timu nyingine hazichezi mpira wa haki.

“Sina uhakika, bali ninahisi baadhi ya timu huwa zinahonga nyingine wakati waamuzi nao wakipewa kitu kidogo. Kimsingi timu bora huwa inaonekana mwanzoni mwa msimu na kwamba mechi za mwisho za ligi hutumika zaidi na timu zenye fedha kwa kupanga matokeo,” anadai.

Waliopo sokoni sasa

Maxime anasema kuwa baada ya kuondoka kwa Dante, wengine ambao ofa zao ziko mezani ni kiungo Mudhamir Yasin, winga Shiza Kichuya, mlinzi wa pembeni Ally Shomari na beki Salum Mbonde ambaye kwasasa amemaliza mkataba wake.

Kagera Sugar?

Kocha Mexime anasema amesikia tetesi kwamba anatakiwa na Kagera Sugar lakini amesema mipango yake ni kuendelea kuitumikia Mtibwa kwani hajatimiza malengo yake ya kupata mataji na klabu hiyo kama kocha.

Uongozi unasemaje?

Msemaji wa klabu hiyo, Thobias Kifaru anasema, “Tumecheza kwa mafanikio makubwa kwa miaka 21 sasa katika ligi kuu ya bara, niseme kwamba jambo kubwa linalofanya klabu hii iwetengeneze nyota wengi wa uhakika ni kutokana na uongozi bora uliopo katika mfumo wa kampuni.”

“Tumekuwa tukiwalea vizuri wachezaji wetu vijana. Mtibwa ni chuo kizuri ambacho kimekuwa kikizalisha vipaji vingi katika soka la Tanzania na tutaendelea kufanya hivyo kutokana na misingi mizuri tuliyoijenga. Tunafurahi kuzalisha vipaji bora ambavyo vimekuwa lulu,” anasema Kifaru.

Rekodi miaka ya karibuni

Klabu ya Yanga kwa miaka ya hivi karibuni iliwasajili kutoka Mtibwa wachezaji; Said Bahanunzi, Juma Abdul, Shaaban Kado, Hussein Javu. Wakati Simba waliwahi kuwasajili Shaaban Nditti, Shaban Kisiga, Hassan Kessy, Musa Hassan ‘Mgosi’, Abdulhalim Humud, Hussein Shariff ‘Cassilas’, Issa Rashid ‘Baba Ubaya’, Paul Ngalema na wengineo.