Rais huyu aliyeongoza kuanzia 1995 hadi 2005, anakosolewa na kada wa zamani wa CCM aliyejiunga na Chadema, Khamis Mgeja, akisema hastahili kuachwa alivyo kwa kuwa ndiye aliyemliza Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, kwa ubinafsishaji uliosabaisha mali na rasilimali za umma kunufaisha wageni, akimnukuu hayati Baba wa Taifa akimuuliza Mkapa…” kama umeuza kila kitu umebakisha kubinafsisha magereza.”
Mgeja ambaye sasa ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Tanzania Mzalendo Foundation anasema mstaafu Mkapa ndiye muasisi wa sera mbovu ikiwamo mikataba mibovu ya ubinafsishaji , kama ya madini kwa wageni na kutoa rasilimali za taifa kwa wawekezaji wa nje kwa bei chee.
Kadhalika ndiye aliyeuza Benki ya NBC kwa Makaburu kwa bei ya Shilingi bilioni 16, licha ya kwamba ilikuwa na mtandao mkubwa wenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 116 kwa wakati huo.
Mwishoni mwa wiki hii, Chama cha Wananchi (CUF), kimeibuka na kungana na Mgeja kutaka Rais mstaafu Mkapa pamoja na Jakaya Kikwete,w ashtakiwe, Mkapa akijibu mashtaka ya mauaji.
Akizungumza katika Kongamano la Kumuenzi hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere , linalofanyika katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam , Mkapa akiwa Mwenyekiti, mwanahabari mkongwe na wakili kujitegemea Jenerali Ulimwengu, alitaka JK ashitakiwe kwa kulisababishia taifa hasara ya Shilingi bilioni 196 kwa kuvuruga mchakato wa katiba mpya.
Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano ya Umma wa Chama hicho, Salim Bimani, anasema CUF inaunga mkono kushtakiwa JK kwa kuvuruga katiba na kuharibu uchaguzi mkuu wa Zanzibar, lakini Mkapa apandishwe kizimbani kwa kusababisha mauaji watu zaidi ya 45 walioandamana kutaka Tume Huru ya Uchaguzi na kurejewa uchaguzi mkuu mwaka 2000.
Hapa zipo dalili kuwa Watanzania wengi wameumizwa na uongozi wa wakuu hawa, machungu dhidi ya Rais Mkapa ni mengi hasa madini ambayo yanadaiwa kuiingiza nchi kwenye malalamiko yasiyokwisha.
Kuna usiri kwenye mikataba ambayo inadaiwa ukienda kwenye maktaba za nje hasa Ulaya unaweza kuipata lakini huku nyumbani Watanzania hawawezi kuisoma. Watu wamepewa migodi kwa miongo mingi. Pia kuna maelezo kuwa vipo vipengele kisheria vinavyowalinda wasiathirike na mapatio ya mikataba hiyo.
Si hapo kuna madai kuwa wapo Watanzania waliofukiwa kwenye mgodi wa Bulyankhulu ili kutoa nafasi kwa mwekezaji wa kigeni. Si hayo wapo wanaolilia tanzanite kubadilishwa jina na sasa inaonekana kuwa ni mali ya wawekezaji wa Afrika Kusini na Mererani nyumbani kwa madini hayo kuko taabani.
Hilo ni eneo la madini pekee, kiongozi huyu mstaafu anahusishwa kuuza kwa bei ndogo nyumba za serikali ambazo viongozi wakuu wan chi wamezigawana. Nyumba hizo kote nchini zimemilikiwa na wachache jambo ambalo pengine lingetizamwa tena.
Ziko kashfa nyingine nyingi, mfano za Meremeta za madini ambazo zilianzia kwenye serikali yake, kuna ile ya madeni ya nje (EPA), mikataba ya kuzalisha umeme na kampuni za kigeni na pia kauli au maneno ya kejeli, dharau na hata kuwaudhi watu kunakodaiwa kulifanywa na kiongozi huyu.
Pia anadaiwa kuwakejeli wanahabari kuwa ni wajinga na misemo kama hiyo.
Kwa upande wa JK mengi yametajwa ukiwamo ufisadi , upendeleo, uharibifu wa rasilimali za nchi kwenye katiba, kashfa Escrow na sasa matukio ya Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).
Ni wakati wa kuchukua hatua. Kama nchi nyingine ziliwahi kutumia Tume za Usuluhishi kujaribu kutizama na kuyamaliza mambo yaliyotokea nyuma nje ya mahakama, kwanini Tanzania isifikirie kuwa na chombo hicho?
Usuluhishi unaleta na kudumisha uelewano badala ya lawama na kupelekana mahakamani ambako kuna mambo yatakayohitaji gharama kubwa na kuibua mifarakano zaidi kuliko watu wanavyodhani.
Kupitia usuluhishi na maridhiano kila anayehisi hakutendewa haki anaweza kusikilizwa na ikibidi baada ya kuthibitika akafidiwa badala ya kwenda mahakamani ambako hatapewa nafasi.
Kwa njia ya usuluhishi Tanzania itakuwa na upendo na kusameheana ambako kunaweza kukafanyika na kurudisha hali ya udugu na uelewano katika nchi badala ya kukimbizana na askari magereza na ushahidi mahakamani, jambo linaloweza kuongeza chuki na hisia za kuwadhalilisha wale ambao waliongoza taifa kwa siku za nyuma.
Ni wazi kuwa madai kama haya yatawaleta wote waliohusika ama waliowashawishi viongozi hao kuchukua hatua walizofikia na kueleza umma mlolongo mzima ulipoanzia badala ya kuwalaumu marais hawa wastaafu peke yao ambao pengine wanastahili kusikilizwa kwa haki.
Ni vyema kufikiria kuwa na taasisi hiyo ili umma usikie, usamehe na utoe hukumu ya haki ambayo ni kuacha ya zamani na kuanza Tanzania mpya.










