Majanga soka la Nigeria

13Jun 2016
Somoe Ng'itu
Nipashe
Majanga soka la Nigeria

Siku tatu baada ya kifo cha Kocha Stephen Keshi, Nigeria ilipata msiba mwingine katika medani ya soka.

Si, mwingine ni Mkurugenzi wa Ufundi wa Chama cha Soka cha nchi hiyo, Amodu Shaibu (58).
Amodu naye aliwahi kuwa kocha wa timu ya Taifa ya Nigeria (Super Eagles).

Kama ilivyokuwa kwa Keshi, Amodu naye aliwahi kuiongoza Nigeria kufuzu fainali za Kombe la Dunia mwaka 2002 na 2010, hata hivyo alitumuliwa kazi hiyo ya ukocha.

Amodu aliwahi pia kuifundisha klabu ya Orlando Pirates ya Afrika Kusini kati ya mwaka 1996 na 1997.
Kufuatia kifo cha Amodu, kilichotokea Jumamosi iliyopita, mashabiki wa soka, wachezaji wa zamani na Wanigeria kwa ujumla walishtushwa na kifo hicho na kuandika kwenye akaunti zao mbalimbali mitandaoni.

Baadhi ya walioguswa na msiba huo ni mchezaji na kocha wa zamani wa Super Eagles, Sunday Oliseh; Senator Shehu Sani, wakili Festus Keyamo na mtangazaji, Funmi Iyanda.

Jumatano wiki iliyopita, Nigeria ilimpoteza aliyekuwa nahodha na kocha wake wa timu ya soka ya Taifa (Super Eagles), Stephen Keshi (54), kutokana na tatizo la moyo, taarifa ya familia yake ilisema.

Kocha huyo aliyekuwa mahiri aliyejulkana kwa jina la 'Big Boss', alifariki katika mji wa Benin ulioko Kusini mwa Nigeria.
Kaka na meneja wake, Emmanuel Ado, alithibitisha kifo cha mkongwe huyo.

"Ni kweli, kaka yangu amefariki. Amekwenda kukutana na mkewe," Ado alisema, akimkumbuka Kate (35), aliyekuwa mke wa Keshi ambaye alifariki mwaka jana kwa kansa ya ufizi.

"Hakuwa anaumwa, hakuonyesha dalili zozote za ugonjwa, lakini tunadhani hakuwa katika hali ya kawaida tangu kufariki kwa mke wake," alisema mmoja wa marafiki wa Keshi kwa majonzi.

RAIS BUHARI AMLILIA
Rais wa Nigeria, Muhammadu Buhari alituma salamu za masikitiko kufuatia kifo cha kocha huyo.
"Leo (Jumatano), Nigeria imepoteza mwanamichezo mkubwa, mcheza soka, kocha na raia," Buhari aliandika katika ukurasa wake rasmi wa akaunti ya Twitter. Aliongeza: "Soka la Nigeria halitakuwa sawa bila ya Stephen Keshi.
"Aliitumikia nchi yake kikamilifu. Apumzike kwa amani."

HISTORIA YAKE
Keshi aliiongoza nchi yake kutwaa ubingwa wa Kombe la Afrika (AFCON).
Mwaka mmoja baadaye, aliisaidia Nigeria kufika hatua ya 16 Bora ya mashindano ya Kombe la Dunia yaliyofanyika Brazil.

Keshi pia aliwahi kuzifundisha timu za soka za Taifa za Togo ambayo mwaka 2006 ilifuzu kucheza Kombe la Dunia. Pia aliinoa Mali.1985 alijiunga na klabu kongwe ya Anderlecht iliyoko nchini Ubelgiji.

Pia aliwahi kuzichezea klabu za Strasbourg ya Ufaransa na Stade Abidjan ya Ivory Coast. Pia aliwahi kucheza soka la kulipwa nchini Malaysia na Marekani.

Akiwa na miaka 52 (mwaka juzi), Septemba 6, aliiongoza Nigeria katika mechi yake ya 52 kusaka tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Afrika 2015 dhidi ya Congo (Red Devils) kwenye Uwanja wa U.J Esuene mjini Calabar na kufuzu.

Keshi alijiuzulu kuifundisha Super Eagles Novemba 11, 2011 baada ya sare ya bila kufungana dhidi ya Botswana kwenye mchezo uliofanyika Ogbemudia, Benin. Kabla ya hapo, kati ya mechi 51, alishinda michezo 23, sare 19 na alipoteza mechi 9 wakati timu hiyo ikiwa imefunga mabao 80 na ikifungwa magoli 47.

Chini ya Keshi, Nigeria ilishinda ubingwa wa Afrika 2013 nchini Afrika Kusini kwa mara ya kwanza baada ya mara ya mwisho kuchukua kikombe hicho Tunisia 1994, Keshi alikuwa nahodha wa timu hiyo, akiwa ni mtu wa pili kuchukua kikombe kama mchezaji na baadaye kocha. Mmisri Mahmoud El-Gohary, ndiye wa kwanza kuweka rekodi hiyo.

Nigeria pia ilifika raundi ya pili kwa mara ya kwanza tangu 1998 wakati wa Fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika Brazil 2014, lakini ilifungwa mabao 2-0 na Ufaransa ikiwa ndiyo mchezo wa 51 wa kocha huyo.

Oktoba 2014 alitimuliwa baada ya timu kuonyesha kiwango kibovu, lakini Rais Goodluck Jonathan alibatilisha uamuzi huo.
Februari 2015, Keshi alikataa kusaini mkataba aliouita wa ''Mkataba wa Kitumwa" kabla baadaye Julai mwaka jana hajatimuliwa kufuatia kukiri kuomba kazi ya kuifundisha Ivory Coast.

Hiyo ilitokana pia baada ya Super Eagles kukosa tiketi ya kushiriki fainali zilizopita za Afrika nchini Equatorial Guinea.