Mbunge anusa harufu ya ufisadi ujenzi wa nyumba za walimu Shinyanga

14Jun 2016
Marco Maduhu
Nipashe
Mbunge anusa harufu ya ufisadi ujenzi wa nyumba za walimu Shinyanga

MOJA ya mikakati ya kukuza kiwango cha elimu nchini ni pamoja na kuboresha mazingira mazuri ya kuishi walimu hasa kuwa karibu na Shule wanazofundishia ili kuwafanya wawe na hali ya kutoa elimu kikamilifu na kuwawezesha wanafunzi kufaulu vizuri na kuzalisha taifa la wasomi.

Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini Steven Masele

Hata hivyo, asilimia kubwa ya walimu nchini huishi mbali na Shule wanazofundishia hata kufikia kilometa nne hadi tano hivyo kusababisha walimu kufika Shuleni wakiwa wamechoka na kutoa elimu kwa kulipua ili kutimiza wajibu tu na sio kujitoa hasa.

Kutokana na adha hiyo wanayoipata walimu ya kuishi umbali mrefu na Shule, halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga imeanza kuondoa changamoto hiyo kwa kuanza kujenga nyumba za walimu katika shule moja baada ya nyingine.Imeanza ujenzi katika shule ya Sekondari Masekelo.

Shule hiyo ilianzishwa mwaka 2007 ambayo ipo takribani kilometa tano kutoka katikati ya Mji wa Shinyanga. Ina walimu 26 kati yao 25 wote wanaishi katika nyumba za kupanga kwenye makazi ya watu hivyo kusababisha wafike Shuleni wakiwa wamechoka pia wakivuka Mto ambao hauna daraja.

Ujenzi wa wa nyumba ya walimu inayojengwa Shuleni hapo itakuwa na ukubwa wa kuhifadhi walimu sita.Ina gharimu Sh.milioni 150. Hata hivyo imebainika kuwa na dalili za kutaka kujengwa chini ya kiwango baada ya mkandarasi kufyatua matofari na kusomba kokoto ambayo yanaelezwa kuwa hayana ubora.

Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini Steven Masele alifanya ziara kwenye Shule hiyo ya kukagua ujenzi wa madarasa mawili, matundu 18 vya vyoo miradi ambayo imekamilika sambamba na ujenzi wa nyumba hiyo ambayo ipo kwenye hatua ya msingi.

Masele alipomaliza kukagua miradi hiyo miwili ya ujenzi wa matundu ya vyoo na madarasa mawili na kujiridhisha kuwa yamekidhi viwango vinavyotakiwa, alielekea kwenye ujenzi wa nyumba hiyo ya walimu sita na kuonyesha mashaka kwenye ubora wa matofari na kokoto zinazotumika kuwa na dalili ya kuwa chini ya kiwango.

Masele baada ya kuonyesha mashaka hayo, alimwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo kumfuatilia kwa karibu mkandarasi huyo ili kuhakikisha nyumba hiyo inajengwa kwa kuzingatia viwango ikiwa pamoja na msingi uliojengwa kama ukibainika kuwa haukidhi viwango ubomolewe na kujengwa mwingine wenye ubora .

“Serikali imekuwa ikijitahidi kukahikisha kuwa inakuza elimu hapa nchini kwa kuboresha miundombinu ya Shule na kuwajengea mazingira rafiki walimu.Lakini baadhi ya wakandarasi hutaka kulipua kazi na kukwamisha juhudi za serikali kumaliza matatizo ya elimu,” amesema Masele

Aliagiza hatua zichukuliwe kuhakikisha kuwa ujenzi bora unafanyika ili kuhakikisha kuwa inakuwa imara ma kuepusha maafa na kuingiza serikali kwenye kashfa nzito na wakandarasi wasiofaa wanapaswa kuangaliwa kwa makini wanapopewa kazi za kufanya.

Kalinjuna Lewis ni Mkurungezi wa Halmashauri hiyo ya Manispaa ya Shinyanga anasema awali kabla ya kuanza kwa ujenzi huo, alibaini matofari yanayotakiwa kujengwa kwenye ujenzi huo kuwa yana kasoro na kumuagiza mkandarasi ayaondoe na kuleta mengine yenye viwango lakini cha ajabu matofari hayohayo ndio yanaendelea kujengewa.

Lewis anasema ana shaka na uadilifu wa mkandarasi huyo katika kuzingatia viwango na kwamba matumzi ya zana za ujenzi zisiszo na viwango zinahatarisha usalama wa walimu watakaoishi katika nyumba hiyo pamoja na kuingizia hasara Serikali kwa kufanya ukarabati wa mara kwa mara.

Hata hivyo Mkurungezi huyo amesema kuwa mkandarasi atakayetekeleza miradi ya maendeleo chini ya kiwango kwenye halmashauri hiyo ndio atakuwa amejifuta mwenyewe kupata kazi tena, maana Serikali inatakiwa kutekeleza miradi mingi na siyo kupoteza fedha kwenye kitu kimoja.

“Nakuhakikishia mbunge kuwa, ujenzi wa nyumba hii ya walimu itajengwa kwa kiwango kinachotakiwa maana na mimi nimebaini kuna dalili ya mchezo mchafu unaotaka kuchezwa hapa maana haiwezekani ninazuia matofari yasitumike kisha nakuta yanatumika tena ,” anasema Lewis

Naye Mhandisi wa halmashauri hiyo Simoni Ngagani amesema wakati walipokuwa wakitangaza tenda ya ujenzi wa nyumba hiyo ya walimu, walijitokeza wakandarasi wengi waliokuwa wanataka pesa zaidi ya hiyo sh. milioni 150 na kupatikana mkadarasi huyo, ambaye yawezekana anajenga kwa shingo upande.

Kwa upande wake Msimamizi wa ujenzi wa nyumba hiyo ambaye alikata jina lake lisitajwe akimwakilisha mkandarasi alikiri kupewa maagizo na Mkurungezi ya kuzuiwa kujengea matofari hayo na kokoto kisha akaomba radhi kwa kosa hilo huku akiahidi kuubomoa msingi na kujengea matofari mengine.

Steven Mihambo ambaye ni mkuu wa Shule hiyo anasema endapo ujenzi huo ulioanza May mwaka huu endapo utakamilika kwa wakati July mwaka huu, utasaidia kuondoa adha ya walimu kutoka umbali mrefu na kuwapunguzia gharama ya usafiri kwani kila siku wanatakiwa watoe Sh. 2,000.

Mihambo pia ameitaka serikali itoa hamasa kwa wananchi wachangie Shughuli za maendeleo ya Shule ikwamo ujenzi wa nyumba za walimu kwani bado zinahitajika kwa wingi.Nyumba hiyo itakapokamilika itaondoa tatizo la walimu sita na kubaki 19 wakiendelea kutembea na umbali huo mrefu kama kawaida.