Ukerewe yapiga mbiu ipelekewe walimu wanawake

14Jun 2016
Rose Jacob
Nipashe
Ukerewe yapiga mbiu ipelekewe walimu wanawake

Wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza inakabiliwa na changamoto lukuki ikiwamo uhaba mkubwa wa walimu wanawake na kuathiri malezi hasa kwa wanafunzi wasichana,

madawati na wanafunzi kulazimika kusafiri kwa kutumia mitumbwi na maboti ili kuvuka kwenda kuzifuata shule zilizo mbali na maeneo yao.

Upungufu wa walimu wa kike unasababisha changamoto kubwa ya kimalezi hasa kwa wanafunzi wasichana wanaopevuka ambao hukosa miongozo sahihi na kuathiri safari yao ya kutafuta elimu

Ofisa Elimu Msingi wilaya ya Ukerewe, Reginald Richard alikiri kuwapo tatizo hilo“Pamoja na changamoto hizo wilaya imeendelea kufanya vizuri katika mitihani ya kuhitimu elimu ya msingi mfano mwaka 2014 wilaya ilishika nafasi ya kwanza kimkoa na nafasi ya kumi na tatu Kitaifa na mwaka 2015 ilishika nafasi ya kwanza kimkoa na nafasi ya tano Kitaifa”.

Mwanza ni mkoa unaounganishwa na wilaya saba, halmashauri nane zilizo na rasilimali nyingi zinazoliingizia Taifa mapato na jamii kwa ujumla.

Unatajwa kuwa ni wa pili katika kuchangia mapato ya taifa.Hata hivyo, katika baadhi ya wilaya zake, kunakabiliwa na chagamoto kubwa ya upatikanaji wa elimu kutokana na hali halisi ya mazingira yake.

Wilaya ya Ukerewe ni miongoni mwa wilaya saba za mkoa huu.Una jumla ya visiwa 38 katika Ziwa Victoria.Visiwa 15 vinatumika kwa ajili ya makazi ya kudumu na 23 vinatumika kwa makazi ya muda mfupi kama kambi za uvuvi. Makao makuu ya wilaya niNansio.

Halmashauri ya wilaya hiyo ina shule za msingi 124 kati ya hizo moja ni ya binafsi.Shule za sekondari ni 25 kati yaketatu ni za binafsi Idadi ya walimu katika shule za msingi ni 1,616 na upungufu wa walimu 1,400.Mahitaji halisi ya walimu ni3,016. Kuhusu uandikishaji wa wanafunzi wa darasa la kwanza matarajio yalikuwa ni kuandikisha watoto 12,498 lakini lengo lilivuka na kuwaandikisha wanafunzi 22,212 ambao ni sawa na asilimia 177.7.

Idadi hiyo imesababisha halmashauri kukabiliwa na changamoto nyingi ikiwamo kuweka mazingira rafiki ya kusomea, kukabiliwa na uhaba wa madawati na usafiri wa mitumbwi kuwawezesha wanafunzi kwenda na kurudi shuleni.Baadhi ya shule za Sekondari na msingi hazifikiki kwa urahisi.

Kama hiyo haitoshi, wilaya hiyo inakabiliwa na changamoto kubwa ya uhaba wa walimu wa kike hata kusababisha watoto wengi wa kike katika shule nyingi zilizopo katika visiwa vidogo vya wilaya hiyo kukosa malezi yanayojitosheleza toka kwa walimu wanaume na wanawake hivyo kukosa huduma ya makuzi ya kijinsia.

Shule ya Msingi Busumba katika kata ya Bwiro ni moja ya shule zilizopo katika visiwa hiyo inayokabiliwa na uhaba mkubwa wa walimu wa kike tangu ianzishwe mwaka 2004 hadi sasa haijawahi kuwa na walimu wa jinsia hiyo
Mazingira hayo yamechangia kusababisha wanafunzi wa kike katika shule hiyo kuiomba Serikali iwasaidie kuwapatia walimu hao ili malezi yao yaweze kukamilika hata kuwaepushia changamoto zinazowakabali katika ukuaji wao ambazo walimu wakiume hawawezi kuzitatua kwa ukamilifu.

Wanafunzi wazungumza

Wanafunzi wa shule hiyo wakizungumziachangamoto zao hivi karibuni walitaja kwamba ni pamoja na uhaba wa madawati, ukosefu wa walimu wa kike hata kusababisha mapungufu katika malezi yao hasa changamoto za ukuaji kwa wasichana Waliiomba Serikali ilione suala hilo na kulitafutia ufumbuzi haraka ili kuboresha malezi ya wanafunzi wa kike katika wilaya hiyo.

“Tunachangamoto nyingi sana,hasa wanafunzi wa kike tunakumbana na vishawishi vingi na kushindwa kuviepuka kikamilifu kwa sababu ya ukosefu wa elimu ya kutosha ya kujisimamia, walimu wa kiume wanatufundisha lakini sio kwa undani ingekuwa vizuri kama tungepata walimu wa kike. Na tukipatiwa madawati yatatusaidia kufanya vizuri maana watoto wa kike baadhi yetu tukishapevuka tunaona kusomea chini ni
fedheha na kuamua kuacha shule,”walisema wanafunzi hao.

Suala jingine waliloligusia ni usafiri kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari zilizopo visiwani, kwa sababu ya ukosefu wa shule za sekondari inawalazimu kusafiri kwa kutumia mitumbwi hata kuhatarisha kwa maisha yao na kuchangia vishawishi kwa watoto wa kike hasa kutoka kwa waendeshaji wa vyombo hivyo.

Wazazi wanena
Daudi Magesa ni mzazi wa mwanafunzi wa darasa la saba shuleni hapo, alisema tatizo la ukosefu wa walimu wa kike linampa wasiwasi sana kuhusu usalama wa watoto wao mabinti ili wapatiwe elimu ya kujitambua hata kuchangia ongezeko la wasichana wengi kukata tamaa ya masomo kwa kushindwa kuhimili mikikimikiki ya maisha.
Kwa upande wake, Suzana Phinias alisema tatizo hilo ni kubwalicha ya kwamba wazazi wanajitahidi kuwaelimisha watoto nyumbani kwao lakini hawana uelewa wa kutosha kwa sababu ya kiwango cha chini cha elimu kwa wazazi wengi kisiwani humo
“Mfano mimi nilikomea darasa la tatu.Wakati mwingine tunaogopa kuwafunza watoto mambo yote kwa kuwa hata sisi tuliishia njiani.Tunaamini huko wanakokwenda kujifunza watafunzwa kila kitu, lakini kumbe inakuwa sivyo. Wazazi tunapata ugumu kuwafundisha watoto wetu pamoja na mambo mengine ni majukumu ya kutafuta riziki.

“Ukerewe inawalimu wengi waliozaliwa katika visiwa hivyo ambao wana uzoefu mkubwa katika masuala ya maji, hivyo wanamudu kuishi katika visiwa kikamilifu endapo tu wataboreshewa mazingira na kuwafanya wasikate tamaa kwamba wametelekezwa,”alisema Suzana.

Mkurugenzi azungumza

Mkurugenzi wa halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe, Jumanne Mwasamila alisema tatizo la ukosefu wa walimu linatokana na umbali uliopo kati ya visiwa hivyo na vingine, hata kusababisha walimu kushindwa kwenda kuishi huko.
“Changamoto kubwa inatokana na walimu wa kike wanaotoka mikoa isiyo na ziwa ama bahari wengi wao hushindwa kumudu maisha ya huku ya kusafiri kwa meli,boti ama mitumbwi na hujikuta wakikataa na kuacha kazi kwa sababu ya mazingira hayo wanayoyaona kuwa ni magumu kwao,”alisema Mwasamila.

Mwasamila aliendelea kusema kuwa, sekta ya elimu katika wilaya hiyo inakabiliwa na changamoto nyingi ingawawanajitahidi kukabiliana nazo lakini bado hali hairidhishi. Kuhusu suala la usafiri hali hii inahatarisha maisha ya watoto wanaovuka kwamitumbwi wakiwa wamejazana. Kwa kutambua changamoto hizikuna haja ya kuwasaidia watoto hawa ikiwamo kuwatafutia usafiri ama kuwajengea shule katika maeneo yao ili wasivuke maji.

Naye mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, George Nyamaha alisema wilaya yao inakabiliwa na tatizo la ukosefu wa walimu wanawake hasa katika shule za msingi, pia ukosefu wa shule za sekondari katika visiwa vidogo unaowalazimisha wanafunzi wengi kusafiri kwa kutumia mitumbwi inayosababisha wanafunzi wachelewe kufika shuleni. Hii inasababisha kiwango cha ufaulu kushuka.

Alitolea maoni mgawanyo wa fedha za elimu bila malipo usiwe na vigezo vinavyofanana kwani gharama zinatofautiana kati ya sehemu moja na nyingine hivyo serekali kuu inatakiwa kufanya tathmini katika eneo na kutoa kiwango kinachooana na hali halisi ilivyo.

Nini kifanyike?
Kinachotakiwa ni kuwatafutia na kuwapangia walimu watakaoweza kuishi na kufanya kazi katika mazingira hayo pia wananchi watoe ushirikiano kwa walimu hao endapo wakipangwa

“Walimu hao wanatakiwa kuwekewa mazingira mazuri ya kuvutia ikiwamo kuwalipa mishahara inayotofautiana na walimu wengine wasioishi katika mazingira magumu.Hii inaweza kuwahamasisha walimu wawe na moyo wakujituma hata kufanya kazi katika mazingira husika” alisema.

Nyamaha anasema, katika kutatua tatizo la ukosefu wa shule za sekondari katika visiwa hivyo, Serikali na wananchi wanatakiwa kutoa ushirikiano ikiwamo kuchangia ujenzi wa shule katika maeneo yao ili kuyanusuru maisha ya watoto wasilazimike kuvuka kwenda upande mwingine kufuata shule

Changamoto ya madawati
.
Naye mkuu wa wilaya hiyo, Joseph Mkirikiti alizungumzia tatizo la upungufu wa madawati katika wilaya hiyo, alisema pamoja na mwitikio wa wananchi ambao wameitikia wito na kuanza kuangusha miti na mbao kwa ajili ya kutengeneza madawati.

“Bado kuna upungufu mkubwa wa madawati kisiwani humo kwa sababu ya kuwapo wanafunzi zaidi ya 100,000, huku mahitaji halisi ya madawati ni 52,437 na yaliyopo ni 20,276 na yaliyotengenezwa kwa nguvu za wananchi hadi sasa ni 3,216 hivyo idadi iliyopo hadi sasa ni 20,276. Na upungufu wa sasa ni 10,721,”alisema Mkirikiti”.

Anasema jitihada zimefanyika za kutafuta wadhamini mbalimbali na tayari kampuni ya Tigoimewapatia madawati 200, Tanesco wachangia Sh.1,430 na wakandarasi wa ndani wametoa Sh. 1,750,000.Wakuu wa Idara na watumishi Sh.4,000,000 na wadau wengine Sh. 5,576,000. Halmashauri haina fedha lakini imejitahidi kulipa Sh.50,000,000 na Mfuko wa Jimbo Sh 10,000,000 “Alisema Mkirikiti.

Mafanikio

Kwa upande wake Ofisa Elimu Msingi wilaya ya Ukerewe, Reginald Richard alieleza kuwa “Pamoja na changamoto hizo wilaya imeendelea kufanya vizuri katika mitihani ya kuhitimu elimu ya msingi mfano mwaka 2014 wilaya ilishika nafasi ya kwanza kimkoa na nafasi ya kumi na tatu Kitaifa na mwaka 2015 ilishika nafasi ya kwanza kimkoa na nafasi ya tano Kitaifa”.