Na ndiyo maana wala si ajabu kuona taarifa za baadhi ya vyombo vya habari kuripoti Simba kumsajili Jamal Mnyate kutoka Mwadui FC.
Kama Mnyate atakuwa amesajiliwa na klabu hiyo, naye ataingia kwenye orodha ya wachezaji waliosajiliwa na klabu baada ya kuifunga.
Mei 8 mwaka huu, Mnyate alipofunga bao pekee dhidi ya Simba katika mechi ya Ligi Kuu Bara akiwa Mwadui.
Wafuatao ni wachezaji waliosajiliwa na klabu baada ya kuzifunga.
1. Hussein Javu
Mshambuliaji Hussein Javu ambaye sasa anaichezea Mtibwa Sugar.Ligi Kuu ya 2012/13 alipokuwa na timu hiyo alifunga mabao mawili Mtibwa ilipoichapa Yanga mabao 3-0 kwenye Uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro.
Javu alifunga magoli hayo dakika ya 45 na 77, mechi iliyochezwa Septemba 19, 2012.Baada ya mechi hii, Yanga iliamua kumsajili, lakini muda mrefu aliishia benchi kabla ya kuamua kurejea kwenye timu yake ya zamani alipomaliza mkataba wake wa misimu miwili.
2. Didier Kavumbagu
Ndiye mchezaji anayeongoza kwa kusajiliwa na timu alizozifunga.Mrundi huyu awali alisajiliwa na Yanga mwaka 2012, akitoka Atletico Olympic ya Burundi.
Kusajiliwa kwake kulitokana na kufunga magoli mawili yaliyoifanya Yanga kuchapwa mabao 2-0 na Atletico kwenye mechi ya kwanza ya Kombe la Kagame, ingawa watoto hao wa Jangwani walitwaa ubingwa.
Baada ya hapo Yanga ilimsajili kwa mkataba wa miaka miwili hadi ulipomalizika mwaka 2014.Akiwa Yanga, Kavumbagu alifunga magoli mechi zote mbili msimu wa 2013/14 dhidi ya Azam FC.
Septemba 22, 2013 mechi ya mzunguko wa kwanza alifunga goli moja, Yanga ikilala mabao 3-2 dhidi ya Azam, lakini Machi 19, 2014 alifunga goli lililoisaidia Yanga kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Azam.
Kuona jinsi anavyowafunga, Azam walitupa ndoano na kusajili mwaka 2014, mara tu alipomaliza mkataba wake na Yanga.
3. Hamisi Kiiza
Alisajiliwa na Simba msimu ulioisha wa Ligi Kuu na kuwafungia magoli 19.
Ingawa hakucheza Ligi Kuu msimu wa 2014/15, lakini kilichochangia zaidi Simba kumsajili kile kitendo cha kuwafunga mara kwa mara akiwa Yanga.
Alianza kuwafunga Mei 18, 2013, akifunga bao moja Yanga ikinyoosha Simba ambao 2-0 Ligi Kuu msimu wa 2012/13.
Oktoba 20, 2013, alifunga magoli mawili, Yanga ikitoka sare ya mabao 3-3 dhidi ya Simba ligi ya msimu wa 2013/14.
Baada ya kuachwa na Yanga na kukaa msimu mzima nyumbani, Simba ikaamua kumsajili kutokana na historia ya kuwafunga.
4. Paul Nonga
Ni mshambuliaji wa zamani wa timu za JKT Oljoro, Mbeya City na Mwadui FC.
Kwa sasa anaichezea Yanga. Unajua kwa nini alisajiliwa na timu hiyo?
Mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu, Yanga ilikwenda kwenye Uwanja wa Kambarage Shinyanga na kuambulia sare ya mabao 2-2 dhidi ya Mwadui.
Pamoja na kuwanyanyasa mabeki wa Yanga, lakini Paul Nonga alipachika moja ya mabao na ndicho kilichowafanya Yanga kumsajili wakati wa kipindi cha dirisha dogo.
5. Malimi Busungu
Mshambuliaji huyu alipata ulaji Yanga baada ya kuwafunga goli Machi 29, 2014 kwenye mechi ya Ligi Kuu msimu wa 2014/15 na kuifanya timu aliyokuwa akiichezea, Mgambo Shooting kushinda kwa mabao 2-1.
Hii ilichangia kwa kiasi kikubwa kusajiliwa msimu uliomalizika wa Ligi Kuu.Hata hivyo tangu atue Yanga, straika huyu hana namba ya kudumu kwenye kikosi hicho.










