Inaelezwa kwamba, biashara za vyakula zinazoendeshwa katika mazingira hatarishi ni tatizo kubwa. Kwa kipindupindu ambacho kimeshamabukiza watu 3448 na kuua 57.
Uamuzi wa serikali kupiga marufuku biashara za vyakula na vimiminika katika mazingira hatarishi, umesababisha migahawa na maduka ya chipsi kutoweka, hali iliyoendana na sehemu kubwa ya ajira katika sekta isiyo rasmi Zanzibar kusimama.
Serikali inaeleza kwamba imeshabaini kuwapo mazingira hatarishi kwa afya ya Wazazibari na ameagiza kufungwa biashara, kwani zimekuwa zikifanyika katika mazingira yasiyo rafiki, jambo linalosababisha wilaya 11 za Visiwa vya Unguja na Pemba.
WAFANYABIASHARA
Juma Mussa Ali, ni mfanyabiashara wa chipsi katika eneo la Darajani, anasema kuwa biashara yake ilikuwa ikimuingizia Sh. 300,000 kwa siku, kutokana na kuuza chipsi na urojo.
Anasema kiasi kilimuwezesha kuwalipa mishahara wafanyakazi wake wanane, ambao kwa sawa kusimama biashara kuendeleza ajira yake.
Juma anasema kulikuwapo wananufaika na mradi huo waliokuwa wakimuuzia chapati, maandazi, bajia na kachori kila siku.
Kwa upande wake, Said Hassan Bakar, ambaye ni mfanyabiashara wa chipsi katika eneo la Jang’ombe, anasema tangu serikali ipige marufuku biashara za chips, amekuwa akishindwa kumudu mahitaji ya familia yenye watoto 12 na wake wawili.
“Hatujafahamu lini serikali itaruhusu, ili tuendelee na biashara zetu, kwa sababu maisha yamekuwa magumu. Serikali ituangalie, kwani tunaumia,” anasema Bakari.
Makame Kombo Shaame, ni mfanyabiasha wa viazi na vitunguu katika soko la Darajani, anayesema tangu serikali kupiga marufuku migahawa na maduka ya chipsi, maisha yamekuwa magumu.
Anasema kwa siku aliuza gunia mbili za viazi na vitunguu gunia moja, lakini biashara imekuwa ngumu tangu wamiliki wa migahawa na chipsi kusitisha biashara zao Zanzibar.
“Tumebakiwa na wateja wachache wa mahitaji ya nyumbani soko letu la chipsi na migahawa limekufa, wakati ndiyo tegemeo kubwa,” anasema Pandu Said Hassan, mfanyabiasha kutoka wa Soko la Mwanakwerekwe.
Mmiliki wa Mgahawa wa Turutara, Munir Zakaria, anasema wafanyakazi watatu na vibarua watatu hawana ajira sasa, baada ya kufunga mgahawa wake. Ajira yao kwa mwezi ni Sh. 200,000.
Mamalishe Mwanahija Juma Saleh, anayefanya biashara katika Mtaa wa Darajani, Unguja anasema uuzaji chakula ndiyo ilikuwa unamsadia pato la kila siku na gharama za kujielimisha.
Anasema asilimia 90 ya biashara ya chakula katika mtaa huo, inafanywa na wanawake ambao kwa sehemu kubwa ni wajane na wanaolea yatima.
Kwa mujibu wa Mwanahija katika maisha yake, amekuwa akienda asubuhi masomoni na jioni anajiunga katika biashara ya chakula mtaa wa Darajani, ambayo ina maana kubwa kwa maisha ya familia yake.
“Kufa hatufi lakini chamoto tunakiona! Maisha yamekuwa magumu, tunaomba serikali ituagalie kwa macho ya huruma,” analalama Zuwena Hasaan, mkazi wa mtaa wa Mikunguni, Unguja.
“Nilikuwa nauza kilo 200 za nyama kwa siku, lakini sasa nauza mpaka kilo 100, kwa sababu wateja wangu wamepungua tangu serikali kupiga marufuku biashara ya vyakula.” anaeleza Amour Iddi wa Soko Kuu la Darajani Unguja.
Salehe Masoud, ambaye wateja wake wengi ni wakaanga samaki mitaani kwa kiasi kikubwa wamepungua.
“Nimebakiwa na wateja wa mahitaji ya nyumbani, biashara kwa kiasi kikubwa imeanguka, hatuna wateja wa uhakika,” anasema Masoud, anayelalamika kwamba kipato chake klimeshuka kutoka Sh. 350,000 hadi Sh.150000.
KAULI YA SERIKALI
Mkurugenzi wa Kinga Wizara ya Afya Zanzibar, Dk. Mohamed Dahoma, anasema serikali imepiga marufuku biashara za vyakula katika mazingira hatarishi, baada ya kipindupindu kudumu Zanzibar kwa miezi saba.
Dk. Dahoma anasema baada ya kufanya ukaguzi, waligundua kuna migahawa inayotoa huduma bila ya kuwa na wafanyakazi waliopimwa afya na hakuna huduma za vyoo.
Anasema biashara nyingi zilikuwa zikifanyika bila ya kuzingatia usafi na kanuni za afya, jambo lisilokubalika kwa mujibu wa sheria na kanuni za afya.
Mkurugenzi huyo anasema maambukizi ya kipindupindu yamepungua kutoka wagonjwa 192 hadi 164, tangu serikali ilipopiga marufuku biashara za vyakula katika maeneo hatarishi.
‘Vifo vimepungua kwa aslimia 50, lakini bado kuna changamoto kubwa. Mvua zinazoendelea kunyesha kutokana na mazingira yetu bado kuwa sio ya kuridhisha,” ansema Dk. Dahoma.
Anaongeza kwamba ukaguzi walioufanya katika nyumba 303, wamebaini nyumba 150 zilikuwa hazina huduma za vyoo na aslimia 51 hazikuwa karo za kuhifadhi maji machafu.
Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa ya Zanzibar, Aboud Hassan Serenge, anaiasa jamii kubadilika kwa kutii kanuni za usafi, ili kila mwanachi afanikishe mkakati wa kutokomeza kipindupindu.
Serenge anasema kuna mabadiliko ya mlo wa watu wengi waliokuwa wateja wa migahawa iliyopigwa marufuku na kwenye mauzo ya chipsi, sasa wanahamia madukani kununua biskuti, maji na soda.
Anasema hata shule, wanafunzi wa madarasa ya kwanza hadi la tatu wamesimamishwa masomo kuangalia hali ya kipindupindu inavyoendelea.










