MAFURIKO WILAYA 5 ZA MORO Uhai wa watu na mifugo watwaliwa

05May 2016
Ashton Balaigwa
Nipashe
MAFURIKO WILAYA 5 ZA MORO Uhai wa watu na mifugo watwaliwa

WAKATI Mvua zinaendelea kunyesha nchini ikiwemo katika mkoa wa Morogoro, kuna athari kubwa zinazoendelea kushuhudiwa, zikihusu mali na hali za watu mbalimbali.

Baadhi ya nyumba katika kijiji cha Mambegwa wilayani Kilosa, zikiwa zimezingirwa na maji katika picha tofauti.

Mkoani Morogoro kunashuhudiwa vifo vya watu watano na makazi yao kusambaratishwa. Maeneo hayo ni katika wilaya za Kilosa, Morogoro, Kilombero na Malinyi.

Wilaya nyinginezo zilizobaki zimepata mafuriko bila ya kuleta athari za kwa moja. Mvua za msimu wa Masika zilianza Aprili 14 mwaka huu na ndipo kukashuhudiwa madhara ya vifo, kuharibika mazao, nyumba kuzolewa na maji, pia miundombinu ya barabara na madaraja.

WILAYANI KILOMBERO

Hiyo ndiyo wilaya ya kwanza kuathirika na mvua hizo. Mwanzo wake ulikuwa mto Lumemo uliosababisha vifo vya watu watatu.

Kati ya waliofariki, wapo wanafunzi wawili wa shule ya msingi katika tarafa ya Ifakara na mwanaume mmoja, ambao wote walikuwa wakijaribu kuvuka mto na ndio wakasombwa na maji.

Sakata ilianza kwa mvua kunyesha mfululizo kwa saa nane na kusababisha vifo vya wanafunzi wawili, baada ya mkondo mkuu wa maji ya Mto Lumemo kuchepuka na kuingia katika makazi ya watu.

Mauti yaliwakuta wanafunzi hao, walipojaribu kuogelea katika moja ya madimbwi yanayotokana na mafuriko wakati wakitoka shuleni.

Wanafunzi waliofariki walitambuliwa kwa majina ya Esther Kong’oa(12,) anyesoma darasa la sita katika Shule ya Msingi Ifakara na mwenzake Rehema Lyakalyaka (12), anayesoma darasa la nne katika Shule ya Msingi Mbasa.

Mtu mzima aliyefariki na jina lake halijatambulika, alikumbwa na mauti alipojaribu kuvuka mto Kisawasawa na maji yalimshinda nguvu.

Athari nyingine za Wilaya ya Kilombero ni kuvunjika kwa daraja la Mto Njokomoni, katika Kata ya Mang’ula na ikasababisha wakazi wa wilaya za Malinyi na Ulanga wanaotumia barabara ya Kidatu – Ifakara kukaa zaidi ya saa 24 wakisubiri matengenezo, kurejesha mawasiliano.

Athari nyingine ni nyumba 36 zenye kaya 98 na wakazi 373, pamoja na mashamba 60 yaliyoharibiwa na mafuriko hayo.

Hata hivyo, kuna taarifa nyingine za kusombwa kwa nyumba tano mmliki wake anayedaiwa ni kutoka jamii ya kifugaji.

Ni hasara iliyoendana na vifo vya ndama watano, mbuzi 20 na kuku 28 katika kitongoji cha Bwawani, Kata ya Kiberege.

Mmiliki wa nyumba hizo pamoja na mifugo hiyo Ngambusu Kazimoto, anasema wakati akiwa usingizini majira ya saa 8.00 usiku, ndipo aliposikia mifugo inapiga kelele na alipotoka nje, aliishuhudia ikisombwa na sambamba na nyumba zake nyingine zikibomoka.

TISHIO LA KIVUKO

Ni mvua zilizoleta tishio kubwa na kusitishwa kwa huduma ya uvushaji abiria na mizigo katika Mto Kilombero, unaounganisha wilaya tatu za Malinyi, Kilombero na Ulanga. Hiyo ni kutokana na maji kuongezeka kasi.

Mkuu wa Kivuko cha Mto Kilombero, Mhandisi Fadhil Haroub, anasema maji yameongezeka katika mto huo kufikia ujazo wa mita 60 na endapo yataongezeka zaidi, watalazimika kusitisha huduma ya uvushaji kwa kutumia kivuko hicho.

Haroub anasema kina cha juu cha maji kichofanya kivuko hicho kishindwe kuendelea na kasi ni mita 90. Hiyo ni kwa sababu kivuko kinakosa maegesho ya kubeba na kushusha abiria na mizigo.

BWAWA KIDATU

Kwa upande wa bwawa la kufua umeme la Kidatu, linaelezwa kuvuka kiwango chake cha kawaida cha mita 450 za ujazo, kutoka usawa wa bahari.

Hilo ni jambo linaloelezwa kuhatarisha miundombinu ya bwawa hilo, hali inayowaathiri wananchi wanaoshughulika na uvuvi na kilimo, kando ya Mto Ruaha Mkuu.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (Tanesco), Mhandisi Felchecim Mramba, anatahadharisha kwamba, iwapo maji hayo hayatadhibitiwa, yakkuwa chanzo cha hasara kubwa katika kituo hicho cha kuzalisha umeme.

Anaeleza manufaa ya umeme unaotumia maji, kuwa una manufaa makubwa, ikiwemo kutunzwa kupitia maji yaliyopo kwenye mabwawa jirani, pia ni nafuu katika gharama za uendeshaji, kulinganisha na vyanzo vinginevyo, ikiwemo gesi.

Kwa mujibu wa Mhandisi Mramba, hata mashine moja inapoharibika, bado zinginezo zinaendelea kuzalisha umeme.

WILAYA YA KILOSA

Wilaya hiyo ilikumbwa na mafuriko tarehe 23 ya mwezi uliopita na madhara ya kwanza yakashuhudiwa katika katika Kata ya Tindiga, kupitia vijiji vya Tindiga A na B.

Pia ushuhuda huo uko katika Kijiji cha Changarawe kilichopo katika Kata ya Masanze, kijiji cha Mambegwa kilichopo katika Kata ya Msowero.

Serikali ya wilaya inaeleza sababu ya kuwapo mafuriko hayo kuwa ni kufanyika kwa shughuli za kilimo karibu na kingo za mito ya Mkondoa, Miyombo na Msowero, zinazofanya mito hiyo kujaa mchanga na kubadilisha mwelekeo wa maji kuingia kwenye makazi ya watu.

Kaya zilizoathiriwa na mafuriko jumla ni 1,238 zenye idadi ya watu 4,765, huku kuna nyumba 1,120 zikiathiriwa na 144 zikibomoka kutokana na athari za mafuriko hayo.

Licha ya madhara hayo, pia mafuriko yamesababisha uharibifu mkubwa wa miundombinu ya barabara,mashamba na huduma za kijamii.

Vilivyoharibiwa ni pamoja na visima 18 vya maji. Ni jambo lililosababisha kaya 1,238 kukosa maji safi na salama katika kata za Tindiga, Msowero na Masanze, pamoja na mashimo ya vyoo kujaa na kusambaa uchafu.

Athari ni pamoja na kuharibiwa kwa miundombinu ya Barabara ya Kilosa – Mikumi; barabara ya Kilosa –Rudewa; na Barabara ya Zombo –Nyali –Madudumizi;Ulaya-Kisanga.

Miundombinu iliyoathirika ni ya Shule ya Sekondari Tindiga, Zahanati na shule ya msingi kutopitika, huku vivuko vingi vikichukuliwa na maji.

WILAYA YA MOROGORO

Wilaya hiyo ina Halmashauri mbili, ambazo ni Manispaa ya Morogoro Morogoro Vijijini, zinazounda wilaya hiyo.

Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro ndio iliyokumbwa na janga la mafuriko, yaliyotokana na mvua kunyesha siku ya Mei 23, 2016 na yalivikumba vijiji 14 na vifo vya watu wawili, akiwemo mtoto na dereva wa gari dogo.

Vijiji hivyo vilivyokumbwa na mafuriko hayo ni Magogoni, Kiganila, Bwila Juu,Bwila Chini, Kiburumo ambavyo vyote ni kutoka Kata ya Selembala.

Katika kata ya Mvuha, kuna vijiji vilivyokumbwa na mafuriko ambavyo ni Mvua, Msonge, Dala, Kongwa, Tulo na Lukulunge.

Vingine ni Tununguo na Kisanga Stendi, ambavyo viko katika Kata ya Tununguo, Mkulazi katika Kata ya Mkulazi na Kisanga, ambako kuna jumla ya wakazi 8,795 wanaotokea katika kaya 1,759.

Mafuriko katika Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro Vijijini, yameleta madhara makubwa ikiwemo vifo vya watu wawili, nyumba 135 kubomoka na mashamba yenye mazao kiasi cha hekta 2,305.8 yameharibiwa na maji na vyakula vilivyokuwa ghalani, navyo hakikusalimika.

Chanzo cha kifo katika Mto Ngerengere, kinatokana na dereva wa gari anayedaiwa mkazi wa Ngerengere, alikuwa akivuka na kuzama na gari, kasha akasombwa na maji.

Jitihada za kumuokoa zilifanyika pasipo mafanikio, kwani alikutwa ameshafariki.

Katika tukio lingine, mtoto anayekisiwa kuwa na umri wa miaka 10 na jina lake halikufahamika, alizama kwenye maji ya mto wa mvua baada ya kivuko cha daraja la Mto Mvuha kukatika.

Inaelezwa mtoto huyo alipokuwa na mama yake wakivuka mto, kivuko kilikatika na walianguka na mama yake alifanikiwa kujiokoa, mtoto akazama.

WILAYA YA MALINYI

Wilaya ya Malinyi ilikumbwa na mafuriko baada ya mvua zilizonyesha kuanzia tarehe 10 na kudumu kwa siku 16, hali iliyoenda na athari nzito kwenye miundombinu hiyo, ikiwemo kilomita 94 za barabara 94.

Sehemu zilizothirika ni kati ya Lupilo – Malinyi – Kilosa Kwa Mpepo, wakati barabara ya kutoka Miembeni – Malinyi Mjini nayo imeharibiwa vibaya.

Barabara nyingine zilizopata hitilafu ni kati ya Malinyi Mjini –Igawa, Tanga – Biro, Lugala –Misegese na barabara ndogo zilizoko Malinyi.

Madhara mengine ni kuzingirwa kwa maji Shule ya Msingi Ngombo na imesababisha ifungwe.

Pia kuna hekta 6000 za mashamba ya mpunga, mahindi na ufuta katika vijiji vya Usangule, Ngoheranga na Biro yamesombwa na maji.

SAUTI YA RC

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Steven Kebwe, anakiri kutokea kwa vifo vya watu watano kutokana na mafuriko yaliyosababishwa na mvua zilizonyesha katika wilaya zote za mkoa wake.

Anasema kuwa, baada ya kupata taarifa hizo, uongizi wa mkoa kwa kushirikiana na wilaya, ulichukua hatua kadhaa.

Hiyo ni pamoja na kuagiza helikopta, kusaidia ukaguzi wa maeneo yaliyokumbwa na mafuriko, kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi ili kuona hali halisi na madhara yaliyopatikana na tamwimu zake.

Dk, Kebwe anasema kuwa, baada ya kushuhudia hali halisi, ofisi hiyo iliwasiliana na Ofisi ya Waziri Mkuu Idara ya Maafa, ili kupata misaada ya kukoka maisha ya waliodhurika.

Anasema wakati wanasubiri misaada hiyo, tayari ofisi yake imewasiliana na wadau mbalimbali wilayani, ambao wameanza kusaidia vyakula, dawa na sehemu za kuhifadhi waathirika wa mnafuriko.

Kwa mujibu wa Dk. Kebwe, tayari kumeshaundwa kamati ya kufuatilia michango ya mahitaji ya wahanga wa mafuriko katika kila wilaya zilizokumbwa na mafuriko.

Ombi lake kwa wadau, ni kwamna waendelee kusaidia kutoa vyakula na misaada ya kibinadamu, kwa ajili ya kuwapatia waathirika.

Anasema Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imeahidi kutoa dawa za kutosha kukabili magonjwa ya mlipuko.

Dk. Kebwe anasema miundombinu ya madaraja na barabara zilizoharibika vibaya zinashindwa kupitika, hivyo Serikali imeanza jitihada za kurudisha miundombinu hiyo.

ULANGA,GAIRO NA MVOMERO

Wilaya hizo pamoja na kupata mafuriko, hakuna madhara makubwa ya hali na mali, inagawaje timu ya maafa inaenbdelea kufanya utafiti.