miradi ya uzalishaji na usambazaji nishati ya umeme, madaraja, mabomba ya miradi ya maji, gesi na mingine.
Ni kutokana na umuhimu wa sekta hii si ajabu baadhi ya watalaamu wa uchumi hutumia idadi na thamani ya utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa miundombinu katika kupima ukuaji au uimara wa uchumi wanchi husika.
“Nchi ambayo uchumi wake ni duni haiwezi kutekeleza miradi mikubwa ya ujenzi wa miundo mbinu ya ukubwa na thamani kama ya daraja la Mwalimu Nyerere linonalounganisha Kigamboni na Jiji la Dar es Salaam au miradi mikubwa kama ule unaotarajiwa kuanza kutekelezwa hivi karibuni wa barabara ya njia sita ya Dar es Salaam hadi Chalinze, anaeleza Profesa wa uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ambaye hata hivyo, hataki jina lake kutajwa na kuongeza:
“Hivyo sekta ya ujenzi sio tu ni kielelezo cha uimara wa uchumi na kasi ya maendeleo inayopigwa na nchi husika, lakini ni eneo ambalo kama serikali husika inakuwa makini ni sekta inayopaswa kutumiwa kuimarisha uchumi wa wananchi wa nchi hiyo kwa kuhakikisha asilimia kubwa ya miradi ya ujenzi inatekelezwa na makampuni ya ukandarasi ya wazalendo.”
Nikutokana umuhimu wa sekta ya ujenzi na haja ya makandarasi wazalendo kupata mgawo stahili na wa haki katika soko la miradi ya ujenzi inayotekelezwa nchini, hivi karibuni Chama cha Makandarasi Wazalendo yaani Association of Citizen Contractors Tanzania (ACCT), katika mkutano wake wa mwaka uliofanyika mjini Dodoma kilieleza nia na mikakati yake ya kuanzisha benki maalum kwa ajili ya makandarasi wazalendo ambayo itaitwa Wajenzi Benki.
“Msukumo wa kuanzisha benki hii ambayo licha ya kutoa huduma zingine za kibenki kwa wateja wa aina tofauti na makandarasi wa ujenzi, lakini itakuwa na huduma maalum kwa makandarasi wazalendo ulikuja kutokana na benki zilizoko kutokutaka kujua ni aina ya huduma gani makandarasi wanataka na kwa mazingira tofauti na wateja wengine,” anasema Mwenyekiti wa ACCT, mhandisi Milton Nyerere na kuongeza:
“Tukiwa hatuna nguvu kubwa ya kupaza sauti zetu ili mabenki haya yatuelewe tulijikuta hatuna njia mbadala bali kuja na mkakati huu ili kwa umoja wetu na wadau wetu tuanzishe benki itakayokuwa tayari kujua mahitaji yetu na kukidhi mahitaji yetu, hivyo kuwezesha sekta hii ya makandarasi wa ndani kukua na kuchangia kikamilifu juhudi za kupambana na umaskini.”
Mhandisi Nyerere liuambia mkutano huo uliojumuisha makampuni yenye wanachama wa ACCT 80 na wanachama washiriki 20 kuwa tayari hatua kubwa imekwishapigwa na ACCT baada ya mshauri mwelekezi kukamilisha upembuzi yakinifu na kuukabidi kwa uongozi wa chama kwa utekelezaji wa kuanzisha benki hiyo.
“Tayari mtaalamu mwelekezi wa mradi huu kaleta ripoti juu ya nini kinatakiwa na kifanyike vipi ili mradi wa benki uanze. ACCT tumejipanga kutekeleza mradi huu kutokana na sera ya benki ziliziko na namna zinavyowatendea makandarasi wazalendo ndivyo sivyo, ” alisema Mhandisi Nyerere.
Anatoa mfano ni kwa kiasi gani benki za biashara hazitoi ushirikiano kwa kampuni za makandarasi wazalendo na kwamba ACCT wanapoomba mkopo benki kwa ajili ya kutekeleza mradi wa mteja, benki hizo huwa hazijali mradi unaanza lini na huwa zinatoa fedha pale zinapojisikia bila kujali mkandarasi alishatimiza masharti muda mrefu uliopita.
Kutokana na hali hiyo, anasema mkandarasi aliyeomba mkopo hujikuta yupo katikati ya kabali mbili, ile ya mteja anayetaka mradi wake uanze na benki inayopiga danadana utoaji mkopo na kama mkopo utakuwa umetoka basi atakuwa na kabali ya kudaiwa riba hata kama mteje atakuwa hajamlipa mkandarasi stahili yake ya malipo.
“Utumwa huu wa kukabwa sehemu mbili kwa mara moja tunaukataa kwa kuleta Wajenzi Benki na tayari tumeshapata ishara za kuungwa mkono na wapenda maendeleo na kuna kila dalili kuwa tupo sawa kwa wazo hili,” anabainisha Mhandisi Nyerere.
Katika juhudi za kuwakwamua makandarasi wazalendo nchini kuepuka gharama na usumbufu wa kupindukia wanapotaka dhamana za kuombea zabuni au dhamana za malipo ya wali Bodi ya Usajili wa Makandarasi nchini (CRB) kupitia mfuko wa kusaidia wakandarasi (Contractors Assistance Fund –CAF) imetoa Sh. bilioni 10 kama mikopo ya dhamana hizo kwa makampuni hayo kati ya mwaka 2002 mfuko ulipoanzishwa hadi mwaka huu.
Taarifa hizi ambazo ni faraja kubwa makampuni ya kandarasi ya ujenzi hasa madogo madogo imetolewa wakati ACCT kwa kutambua umuhimu wa mikopo nafuu kwa ukuaji wa sekta ya ukandarasi na hasa makampuni ya ndani.
Kwa mujibu wa Kaimu Msajili wa CRB, Robhen Nkori, mfuko huo kwa kiasi kikubwa umeweza kutekeleza jukumu lake muhimu la kuanzishwa kwake kutokana na kuwasaidia wakandarasi wazawa katika muda na mazingira mwafaka.
“Kabla ya kuanzishwa CAF lilikuwa jambo la kawaida kwa kampuni za wazalendo kushindwa kugombea zabuni kubwa na ndogo kwa kuwa tu kampuni hizo hazikuwa na dhamana ya kuombea zabuni hizo. Mbaya zaidil ilikuwa jambo la kawaida kwa kampuni hizi licha ya kushinda zabuni kushindwa kutekeleza miradi hiyo kwa kukosa dhamana za kuweka kinga ya malipo ya awali kutoka kwa wateja wao. Sasa hilo jambo ni historia hapa nchini kwani mfuko umefanya kazi nzuri sana,” anaeleza Nkori.
Kwa mujibu wa Nkori, licha ya kutoa dhamana kwa makandarasi wa ndani na hivyo kuokoa zabuni za makandarasi hao, lakini mfuko umetekeleza jukumu jingine muhimu zaidi la kuwakinga makandarasi hao na masharti magumu ya kupata dhamana hizo hizo kutoka katika mabenki ya biashara.
“Mabenki ya bishara yana huduma hii ya kutoa dhamana kwa zabuni na hata malipo ya awali, lakini masharti yake hayapo katika namna bora ya kuwahudumia wazalendo hawa. Hivyo kuwapo kwa mfuko huu kumeyaepushia makampuni haya kutekeleza masharti magumu na hasi kutoka katika mabenki haya,” anasema Nkori.
Kwa kujua umuhimu wa umoja katika jambo lolote, Kaimu Msajili huyo wa CRB anaitaka ACCT kujikita katika kuyavuta makampuni zaidi ya ukandarasi yanayomilikiwa na wazalendo kujiunga na ACCT ili chama kiwe na nguvu zaidi na hivyo kuwawakilisha wazalendo kwa kiwango bora zaidi.
“Sina budi kuwapa hongera kwa kuanza kupanga kufanya mambo makubwa kama kuwa na Wajenzi Benki. La muhimu sana hapa ninalo shauri ni kwa chama sasa kuanzisha mradi wa kuleta wanachama zaidi ili katika makandarasi wazalendo 7,000 walau nusu yake wawe wanachama wa ACCT,” anashauri Nkori.
Katika juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano kuisaidia sekta ya ujenzi na hasa makandarasi kwa kipindi cha miezi tisa iliyopita yaani kuanzia Julai 2015 hadi Machi mwaka huu, zaidi ya Sh. trilioni 1.2 zimelipwa kwa makandarasi waliokuwa wakiidai serikali malimbikizo ya madeni kutokana na kutekeleza miradi mbalimbali ya ujenzi nchini.
Katika fedha hizo Sh. bilioni 605.35 zililipwa na Wizara ya Ujenzi kupitia Hazina huku Sh. bilioni 462.123 zikiwa zimelipwa na Bodi ya Mfuko wa Barabara.
“Malipo haya kwa makandarasi yamenufaisha makampuni yote ya ukandarasi yawe ya kigeni au ya wazalendo na lengo kubwa ni kutoa ishara kwenu kuwa serikali hii ya awamu ya tano kwanza haitaki kuwakopa makandarasi na pili inataka kutoa mchango wake kikamilifu kwa ukuaji wa sekta ya ukandarasi na hasa makandarasi wazalendo,” anabainisha Mhandisi Joseph Nyamhanga, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi anayesimamia sekta ya Ujenzi.
Mhandisi Nyamhanga anasema licha ya kulipa madeni hayo, Serikali ya Awamu ya Tano imejiwekea mikakati ya kuona kuwa miradi yote ya ujenzi inayotekelezwa nchini na ambayo inagharamiwa na fedha za walipa kodi Watanzania kuanzia sasa itatengwa mahsusi kutekelezwa na kampuni za ndani tu.
“Hatuoni shida kuitenga miradi hii maalum kwa makampuni ya ndani il mradi tu yakidhi vigezo vya kisheria na utalaamu kwani serikali hii ipo kwa ajili ya Watanzania na kwa kuitenga miradi hii kwa kampuni za ndani tutakuwa tunajenga mazingira ya kukuza uwezo wa kampuni zetu kifedha na kitaalamu na pia kuchochea maendeleo ya kiuchumi kwa nchi kwani mkandarasi wa ndani akipata fedha hizo anawekeza hapa hapa,” anaongeza Nyamhanga.










