Dar ipanuliwe kuinua uchumi-2

24Apr 2016
Ibrahim Mkamba
Nipashe Jumapili
Dar ipanuliwe kuinua uchumi-2

BAADA ya makala ya wiki iliyopita kuhusu ushauri wa namna ya kupunguza msongamano wa Dar es Salaam, yalijitokeza matukio mawili makubwa ya uzinduzi wa barabara ya kwanza ya juu,

jiji la dar es salaam

maarufu kama ya daraja au ya ghorofa (flyover) eneo la TAZARA na pili ni daraja la Mwalimu Julius Nyerere linalounganisha Kigamboni na sehemu nyingine ya Dar, uzinduzi huo ulifanywa na Rais John Magufuli.

Nizungumzie kuhusu daraja la Kigamboni, hakuna ubishi kwamba kama kuna watu wamechangia sana mafanikio ya mradi huo mkubwa ni Rais wakati huo akiwa Waziri wa Ujenzi wakati wa ujenzi wa daraja hilo na Dk. Ramadhan Dau, aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), wakati huo ambaye kwa sasa ameteuliwa kuwa Balozi.

Kwa bahati mbaya Dk. Dau alisahaulika kwenye ratiba lakini Rais, akamkumbuka na kumpa nafasi ya kuongea. Katika hali ya kawaida watu wanaofanikisha mambo makubwa ya nchi hupewa heshima inayostahili.

Watu hawa hawapaswi kudharauliwa.Wengine muhimu waliofanikisha kazi NSSF na waajiri wanaowasilisha michango kwa mfuko huo. Hao ndiyo walioingiza kiasi cha pesa cha asilimia 60 kutoka NSSF kufanikisha mradi huo.

Asilimia 40 imetolewa na serikalini. Kuhusu jina lililopendekezwa na Rais, ni vizuri jina hilo lieleze ni Nyerere yupi aliyekusudiwa. Ukisema Daraja la Nyerere, Makongoro, Madaraka na Nyerere yeyote yule, wa ukoo wa Rais wa kwanza au asiye wa ukoo huo ataonekana amekusudiwa yeye.

ukisema Daraja la Mwalimu Nyerere, walimu Nyerere wa leo ni wengi, watadai ni wao. Kukata mzizi wa fitna ni vizuri likaitwa daraja la Mwalimu Julius Nyerere. Itakuwa vigumu kumpata mtu mwingine wa majina yote hayo na hivyo jina hilo kuwa moja kwa moja likimhusu baba wa taifa.

Tukiendelea na mjadala wa msongamano, hizi barabara za ghorofa na daraja la Mwalimu Julius Nyerere si ufumbuzi wa kudumu wa msongamano. Ni wa muda mfupi. Ufumbuzi huu utafanya kazi vizuri ukiunganishwa na ile mipango ya muda mrefu iliyojadiliwa wiki iliyopita.

Sanjari na hiyo, katika kupunguza usumbufu wa watu, Dar haipaswi kuwa na kituo kimoja cha mabasi iwe kama ilivyo sasa au ikipanuliwa kama ilivyoshauriwa wiki iliyopita. Dar inapaswa iwe na vituo vya mabasi ya mikoani, kama cha Ubungo, visivyopungua sita kwa sasa vya mabasi ya njia zote, kwa mfano Ubungo, Bunju, Mbezi ya Barabara ya Morogoro, Pugu, Temeke na Kibada.

Hii itakuwa njia bora ya kusogeza huduma kwa wananchi, kuwapunguzia usumbufu na kuongeza mapato. Ninasisitiza kwamba kila kituo kiwe na mabasi ya kutoka na kwenda sehemu mikoa yote. Mabasi hayo yagawiwe vituo vya Dar na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) kama inavyofanyika kwa madaladala.

Hebu, tulitazame hili kwa ukweli. Mtu anaishi Kongowe ambayo inafikika kwa njia ya Barabara ya Kilwa. Anatakiwa aende Bunju kuwahi basi la Mwanza, linaloondoka saa 12.00 asubuhi.

Kwa nini abiria huyu aachiwe kwamba kuwahi basi hilo liwe suala lake? Nini wajibu wa viongozi kubuni njia za kuwaondolea watu mateso? Tunapata nini kwa kuwa na kituo kimoja pekee cha mabasi kwa jiji kubwa kama hili? Lengo la kushauri vituo vingi kwa mabasi ya njia zote ni kwamba ukiyagawa kwa ruti kwa mfano Bunju kwa Tanga, Arusha na Moshi, Ubungo kwa Morogoro, Kanda za Kati, Ziwa na Nyanda za Juu Kusini, Kibada kwa Lindi na Mtwara, usumbufu utakuwa palepale kwa sababu wakazi wa Dar es Salaam, husafiri kwenda au kutoka popote bila kujali wanaishi eneo gani jijini.

Kwa mfano, mtu anaweza kuishi Bunju lakini akawa na safari ya Mtwara au mwingine anakaa Mbagala akawa na safari ya Tanga. Ufumbuzi ni kusambaza vituo vya mabasi ya njia zote kotekote Dar.

Naomba wenye mamlaka wautupie macho ushauri huu ambao utekelezaji wake unaweza kuanza hata kesho Jumatatu. Pamoja na kuondoa usumbufu kwa wananchi, mpango huu utaondoa hali ya kufanya magari yasongamane kutoka na kuelekea upande mmoja tu wa kituo kimoja cha mabasi.

Yatatawanyika Naomba nihitimishe mjadala huu kwa kushauri kutazamwa kwa yanayoshauriwa hapa kutoka lile la kujenga uwanja mkubwa wa ndege Bagamoyo (Nipashe Jumapili,6/3/2016), la kulipanua jiji la Dar mpaka karibu na Bagamoyo, karibu na Mlandizi, Masaki Kisarawe na kati ya Shugubweni na Kisiju Mkuranga, kuweka bandari ya nchi kavu kati ya Ruvu na Vigwaza (Nipashe Jumapili, Aprili 17, 2016) na hili la leo la kuwa na vituo vingi vya mabasi ya mikoani Dar. Yote haya yakifanyika kwa mipango ya muda mfupi na muda mrefu, maisha ya watu yatarahisishwa na uchumi utainuka.