Barabara Dar hii sasa kero,kuongeza umaskini

24Apr 2016
Salome Kitomari
Nipashe Jumapili
Barabara Dar hii sasa kero,kuongeza umaskini

MVUA zinazoendelea kunyesha maeneo mbalimbali nchini zimeathiri miundombinu dhaifu iliyoko Dar es Salaam ambayo ina mashimo makubwa kwa madogo yaliyojitokeza baada ya wiki nne za mvua.

mkuu wa mkoa wa Dar es Saalam paul makonda akiangalia uharibifu wa barabara

Kabla ya baraka hiyo kuanza baadhi ya barabara zilikuwa na mashimo ambayo moja kwa moja hayajachangiwa na mvua bali miundombinu iliyojengwa chini ya kiwango.

Mbaya zaidi barabara nyingine hazijafikisha miezi sita tangu kuwekewa lami, lakini zimemeguka kama ambazo zilitengenezwa miongo kadhaa iliyopita jambo ambalo linatia shaka na uwezo wa makandarasi wanaopewa kazi hizo.

Asilimia kubwa ya barabara za jiji hasa zinazosimamiwa na Manispaa zina mashimo makubwa kwa madogo mengine yapo katikati na kuwa chanzo cha ajali. Mathalani, Mwenge kwenye kona ya kituo cha mafuta cha Puma kuelekea Lugalo kuna korongo kubwa ambalo hata ajali ikitokea hakuna utetezi.

Yapo mengi ya kujiuliza kuhusu ujenzi wa barabara hizi kama utoaji wa zabuni husika hufuata vigezo vyote au ipo namna nyingine kwani kama tumeamua kutumia mabilioni ya fedha kujenga barabara kwa kiwango cha lami iweje iharibike chini ya miezi sita?

Kwa kawaida mnunuzi wa bidhaa anaponunua bidhaa au huduma matarajio yake ni kwamba alichonunua kitadumu kwa miaka kadhaa na siyo kutoa fedha kila wakati na kuendelea kununua mali nyingine kwani ni kuendeleza umaskini ambao unaletwa na kukwama kufanyakazi zisizo na manufaa kwa wananchi.

Hivyo hivyo, kwa ujenzi wa barabara kama hautakuwa wa viwango ni kuendeleza umaskani kwani hakuna asiyejua kuwa kandarasi zake zinatumia mabilioni hivyo ni lazima kuwa na barabara imara zitakazodumu muda mrefu.

Ujenzi chini ya kiwango umekuwa chanzo cha ajali nyingi zilizopoteza maisha, kuleta ulemavu , kusababisha uharibufu wa miundombinu kama madaraja, nguzo za umeme na kuharibu mali yakiwamo magari.

Barabara nyingine ni nyembamba kupindukia kiasi kwamba gari kubwa na dogo haziwezi kupishana na inapotokea ajali taabu huzidi zaidi na kuendeleza majanga yasiyo ya lazima. Mifano ni barabara ya Morogoro ambayo imefinywa ili kujenga njia ya mwendo kasi.

Hali ni mbaya zaidi kwenye kona inakuwa vigumu kupishana sehemu hizo. Mathalani , barabara ya kutoka Sayansi hadi baa ya Hongera nyuma ya Chuo cha Ustawi wa Jamii, nyingine kutoka kona ya Brajec hadi nyumba za Mawaziri, kadhalika eneo la Zantel kupitia kwa nyumbani kwa Rais mstaafu hadi karibu na Shule Kuu ya Uandishi wa Habari ni mashimo makubwa na zinamengenyuka kila siku.

Cha kusikitisha zaidi baadhi ya barabara hazina miezi sita tangu zitengenezwe na zimeharibika kiasi cha kuwa kero kwa watumiaji wote kuanzia watembea kwa miguu, wenye magari , daladala na pikipiki na mbaya zaidi maji yametuama na kuzigeuza kuwa makaro ya maji taka.

Mbaya zaidi ubovu na udhaifu wa miundombinu huenda sambamba na ile ya majitaka ambayo kipindi cha mvua hufumuka na kusambaa kwenye makazi ya watu na hakuna hatua za haraka zinazochukuliwa kurekebisha.

Ipo haja kwa Manispaa zetu kujitathimini juu ya viwango vya ujenzi wa miundombinu yake, wanatoe zabuni kwa wenye uwezo na mkandarasi apewe kazi kitaalamu na kitaaluma na isiwe ni kujuana ama kupeana asilimia 10.

Ni aibu kwa Dar kuwa na miundombinu dhaifu kila wakati huku barabara zilizojengwa na Wakala wa Barabara (Tanroads) zikiwa katika hali nzuri kwa kipindi chote cha mwaka.

Kadhalika kudumu kwa muda mrefu. Kinachofanywa na Manispaa ni kuendelea kuogelea katika lindi la umaskini kwa kila mwaka kutenga fedha za kukarabati barabara ambazo hata zikijengwa hazijamalizi miezi sita tangu kutengenezwa, fedha ambayo ingetumika kurekebisha miundombinu ya maeneo mengine.

Hii ni sawa na kupiga hatua moja mbele na kurudi hatua nane, kila mwaka ni matengenezo ya barabara ambazo kila baada ya muda mfupi zinatengenezwa tena, jambo ambalo linaonyesha hapo ndipo kuna kichaka cha watu kuoiga hela za wavuja jasho.

Tunaiomba serikali kuchukua hatua madhubuti kusimamia na kukataa ubabaishaji wa usimamizi wa miundombinj ya Jiji, leo ukipata barabara za Maniaspaa ni ajbu tupu jambo ambalo linatia shakanuwezo wao na kurejesha umuhimu wa Tanroads kupewa kazi ya kusimamia barabara zote.

Ni heri kujenga chache ambazo zitadumu kuliko nyingi ambazo kila baada ya muda mfupi zinahitaji matengenezo kiasi kwamba fedha ya matengenezo izingetumiwa kujenga barabara nyingine.

Tunahitaji kuwa nchi ianyojitegemea hatuwezi kufikia hilo iwapo tutaendelea na ujenzi huu usio na tija yoyote. Mungu ibariki Tanzania Mungu ibariki Afrika