Ingawa ilifungwa na kuondolewa kwenye michuano hiyo, lakini najiuliza kwanini Yanga haikucheza soka kama lile katika mechi ya kwanza Uwanja wa Taifa?
Pengine soka kama lile wangecheza Uwanja wa Taifa, lingeamsha hamasa kubwa kwa wachezaji na kupata ushindi mnono nyumbani. Haikuwa hivyo, Yanga ilishtuka na kujifunika shuka ugenini wakati tayari asubuhi ilishachomoza.
Yanga ilikuwa na uwezo mkubwa wa kushinda nyumbani kwenye mechi ya kwanza kama ingetandaza kandanda tuliloliona ikicheza Misri.
Ilikuwa na uwezo wa kumaliza biashara, huku nyumbani na kwenda kumaliza mahesabu nchini Misri.Lakini kosa kubwa ililofanya ni kucheza kwa woga kwenye mechi ya kwanza nyumbani na kuruhusu sare ya bao 1-1.
Mechi ya kwanza Yanga ilihitaji ushindi mkubwa ili kujiweke katika mazingira mazuri ya kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.Kilichoonekana mbele ya mashabiki wake kwamba Yanga ilionekana kama iko ugenini.
Ilionekana kucheza kwa tahadhari sana, ikiwa nyuma muda mwingi na kushambulia kwa kushtukiza.Uchezaji wa Yanga ulifanana sana na Al Ahly ambao wao walikuwa wakiitafuta sare kwa udi na uvumba.
Lakini pia wana tabia hata kama wakifungwa magoli mawili au matatu, wanasaka bao moja tu la ugenini ili liwarahisishie kazi.
Ahly hawakuonekana kuwa na haraka na walicheza mpira wa taratibu na pasi nyingi fup, wakiwa na dhamira ya kupoteza muda ili mechi hiyo iishe kwa sare.
Kilichoonekana kwa wawakilishi wetu ni kwamba walicheza kwa kuiogopa Al Ahly.Yanga nao wakaingia kwenye mtengo wa wapinzani wao wa kukaa nyuma zaidi na kushambulia kwa nadra.
Ilifika wakati hata mashabiki wa Yanga walikuwa wakiwapigia kelele wachezaji wao kukaa nyuma zaidi na kupigiana pasi fupi fupi, kana kwamba nao walihitaji sare kwenye mechi hiyo.Wakati mwingine walikuwa wakiwasaidia Al Ahly hata kupoteza muda.
Hali ilikuwa tofauti kule Misri, ilicheza kwa kiwango cha hali ya juu kiasi cha kuwapa wakati mgumu wachezaji, viongozi, benchi la ufundi na mashabiki wa Al Ahly.Tatizo kubwa lilibaki pale pale kuwa ilikuwa ikicheza ugenini.
Ilitakiwa icheze vile nyumbani na sina shaka kuwa wangewachangaya kabisa Al Ahly na kushinda mechi kwa magoli ambayo yangewarahisishia kazi mjini Cairo.Mara nyingi kwenye michuano hii timu hushinda nyumbani na ugenini hitafuta sare.
Ingeweza kufanya kama Simba mwaka 2012 kwenye Kombe la Shirikisho ilipoifunga ES Setif mabao 2-0 nchini, lakini pamoja na kufungwa mabao 3-1 nchini Algeria, ilifuzu kwa bao la ugenini.
Lilikuwa bao la dakika za mwisho la Emmanuel Okwi wakati huo Simba ilikuwa imeshafungwa mabao 3-0, lakini bao hilo lilikuwa na maana zaidi kuliko yote yaliyofungwa kwenye mechi hiyo.Kwenye mechi hiyo, ndipo ilipoonekana faida ya kushinda nyumbani, pamoja na goli la ugenini.
Yanga ingecheza soka lile nyumbani na kushinda mabao 3-1, hata kama ingefungwa idadi ile ya magoli, ingesonga mbele.
Na kama ingeshinda mabao 2-1 timu zilikuwa zinakwenda kwenye mikwaju ya penalti.
Goli la ugenini lililofungwa na Donald Ngoma lingekuwa muhimu na la maana sana kama Yanga ingekuwa imeshinda kwenye mechi ya kwanza Dar es Salaam.
Nadhani hilo sasa litakuwa somo kwa benchi la ufundi na wachezaji wa timu hiyo, kwa sababu bado inaendelea kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Sagrada Esperanca mwezi Mei.
Kwa sababu mechi ya kwanza inaanzia Tanzania, Yanga inatakiwa imalize ufundi wake wote wa kutandaza kabumbu na ujuzi wa kufunga magoli hapa hapa, ili kujiwekea mazingira mazuri ugenini.
Mwaka 1993 ilipofanikiwa kufika fainali ya Kombe la Shirikisho ilikuwa inahakikisha inashinda nyumbani kwa idadi nzuri ya magoli, na nyingi ilikuwa ikishinda mabao 3-0 au 3-1.
Rekodi za Yanga dhidi ya Al Ahly
Rekodi za Yanga dhidi ya timu za Al Ahly zinaanzia mwaka 1982 kwa kunyukwa mabao 5-0 mjini Cairo, kabla ya kuambulia sare ya bao 1-1 katika mechi ya marudiano Dar es Salaam.
Mwaka 1988, Yanga ilikutana tena na Al Ahly tena katika Ligi ya Mabingwa na kutoka sare ya bila kufungana na kwenda kufungwa 4-0 katika mechi ya marudiano Cairo.
Mwaka 2009, Yanga ilijikuta ikipata tena kipigo cha mabao 4-0 kutoka kwa Al Ahly. Katika mchezo wa kwanza jijini Cairo Yanga ilifungwa mabao 3-0 na mashabiki wakapata matumaini Yanga ingeing’oa meno Al Ahly, Dar es Salaam kwenye Ligi ya Mabingwa, lakini ikapigwa bao 1-0.
Mwaka 2014, Yanga ikishinda kwa mara ya kwanza dhidi ya timu za Kiarabu Taifa kwa kuifunga Al Ahly bao 1-0, lakini ikafa bao 1-0 nchini Misri na kutolewa kwa mikwaju 4-3 ya penalti, Bahanuzi akikosa penalti ambayo ingewapeleka kwenye hatua ya makundi.
Mwaka huu 2015 zimekutana tena na kutoka sare ya bao 1-1 jijini Dar es Salaam na Yanga ikafungwa mabao 2-1 nchini Misri.










