Ziara ya Rwanda ni kuua ndege wawili kwa jiwe moja

24Apr 2016
J.M. Kibasso
Nipashe Jumapili
Ziara ya Rwanda ni kuua ndege wawili kwa jiwe moja

RAIS John Magufuli, alifanya ziara ya kwanza ya kikazi nje ya nchi kwa kutembelea Rwanda ikiwa ni siku 153 tangu alipoapishwa kushika wadhifa wa urais na kuingilia Ikulu Novemba mwaka jana.

Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na Rais wa Rwanda Mhe. Paul Kagame wakikata utepe kwa pamoja kuashiria uzinduzi rasmi wa daraja la kimataifa la Rusumo

Waswahili wana msemo kwamba “hayawi hayawi sasa yamekuwa’ kwa mujibu wa taarifa kutoka kitengo cha mawasiliano Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa ilisema, ziara hiyo ilitokana na mwaliko wa Rais wa Rwanda, Paul Kagame.

Akiwa nchini Rwanda pamoja na mwenyeji wake walifungua daraja la kimataifa la Rusumo na kituo cha mpakani, ambavyo vilielezwa ni muhimu kwa maendeleo chini ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Rais Magufuli, alihitimisha ziara yake jijini Kigali ambako walifanya mazungumzo ya faragha na mwenyeji wake na mara baada ya makubaliano walikwenda kuweka shada la maua ya kumbukumbu ya mauaji ya kimbari yaliyotokea mwaka 1994 nchini Rwanda.

Turejee kwenye hoja ya makala ya leo inayohusu hasa ziara ya kwanza ya Rais nje ya nchi ikiwa ni siku 153 tangu alipoapishwa kushika wadhifa huo. Mengi yalisemwa na kujadiliwa kwenye vyombo mbali mbali vya habari kuhusu mtizamo wa serikali ya awamu ya tano katika mahusiano na kidiplomasia ya nje.

kama ilivyo ada, marais wengi wa Kiafrika mara tu baada ya kuapishwa, huwachukua siku kati ya 10 na 30 tayari wameanza safari za kujitambulisha nje. Hatua ya Rais Magufuli kuchukua siku 153 bila ya kusafiri nje ya nchi imetafisiriwa kuwa ni uzalendo uliotukuka wenye kujali nchi na watu wake.

Hakuna jambo lisililokuwa na mwisho wake. Hatimaye Rais Magufuli amefungua mlango na kutoka nje Pamoja na majukumu mengine imeelezwa kwamba safari yake aliitumika kufanikisha mambo mawili makubwa.

Mosi, kutembelea nchi jirani ambayo pia ni mwanachama wa EAC pili, kurudisha imani ya wananchi wa pande hizi yaliyoanza kufifia. Hii ndiyo maana nimesema ameua ndege wawili kwa jiwe moja. Katika vitabu vitakatifu tumeelekezwa kuwathamini na kuwapenda majirani zetu.

Rwanda na Tanzania ni majirani licha ya kuwa nchi hizi zinaunda jumuiya ya EAC. Rais Magufuli alitimiza moja ya nguzo kuu katika maisha ya binadamu ambao ni utu, uungwana na kuwathamini majirani zako.

Safari hii ya Rais Magufuli inaelezwa ilifufua matumaini mapya ya mahusiano kati ya nchi hizi mbili baada ya kuarifiwa kwamba Rais Paul Kagame na Rais mstaafu Jakaya Kikwete walitofautiana kimazungumzo. Inasadikika kuwa mataifa haya yalianza kujitayarisha kijeshi kwa lolote ambalo lingetokea.

Kwa mazingira hayo, ziara hii imesaidia kuwaunganisha wananchi wa mataifa haya mawili na kurejesha undugu na urafiki kama ilivyokuwepo hapo nyuma. Sambamba na hilo, ziara ya Rais Magufuli nchini Rwanda inasemekana imepangua majaribio Kenya, Rwanda na Uganda ambazo ni miongoni mwa wanachama wa EAC kutaka kuzitenga Tanzania na Burundi kwenye maamuzi ya misingi ya jumuiya hiyo.

Itakumbukwa nchi hizi tatu ziliwahi kutamka kinaga-ubaga kwamba wanaanza ushirika upya wenye kasi katika kiuchumi. Baadaye tulishuhudia nchi hizi zikiomba mkopo wa kujenga reli ya kisasa kutoka Mombasa kwenda Kigali na Kampala.

Pia Kenya na Uganda walikubaliana kujenga bomba la mafuta kutoka Kampala hadi Lamu (Kenya) Tofauti na ilivyokuwa ikifikiriwa, wadau wengi wa siasa walitegemea ziara ya Rais Magufuli ya kwanza nje ya nchi angeanzia ughaibuni hasa nchini Marekani.

Hii ni kwasababu ya ukweli kwamba Rais mstaafu Kikwete aliacha mahusiano mazuri ya kidiplomasia baina ya nchi hizi mbili. Mbali na mahusiano mazuri ya kidiplomasia pia ulijitokeza msuguano kati ya Tanzania na Shirika la Changamoto za Milenia la Marekani (MCC), baada ya shirika hilo kuinyima Tanzania misaada wa Dola milioni 472 sawa na Shilingi trilioni moja na ushee.

Hivyo wengi walitarajia ziara yake ya kwanza angeitumia kwenda kuongea na Marekani. Hata hivyo, Rais Magufuli hakuonyesha kusikitishwa na maamuzi hayo ya (MCC), bali aliamua kufuata nyayo za mwalimu Nyerere aliyeapa kwamba hawezi kugeuka

“jiwe” kuangalia nyuma kuwapigia magoti Wazungu eti kwasababu ya kupewa misaada. Wachambuzi wa mambo ya siasa wameitafsiri uamuzi wa Rais kama ni wa kijasiri sawia na alivyokuwa Baba wa Taifa Julius Nyerere, ni mara chache marais wa Kiafrika kufikia maamuzi magumu kama hayo.

Maadamu Rais Magufuli sasa amefungua mlango wa kusafiri nje ya nchi, hakuna ubaya kwenda kuimarisha mahusiano na nchi hizi za Magharibi.

Watanzania wako nyuma yake, hatuwezi tukabweteka tukadhani eti makusanyo ya ndani yanaweza kukidhi mahitaji yetu tukasimama wenyewe bila ya misaada kutoka mataifa yaliyoendelea. Tuko tayari kupokea misaada kutoka nchi hizo lakini kusiwepo na masharti ya kuingilia mambo yetu ya ndani.

Hata hivyo ingawaje bado tu wachanga, lakini Rais Magufuli amethubutu kutufungua fikra kwamba tunaweza kusimama wenyewe kamawananchi watakusanya nguvu zao kwa pamoja kama taifa moja.

Wananchi wengi waliokuwa wakifuatilia ziara ya hiyo, waliafiki uamuzi wake wa kuanza ziara katika nchi ya jirani. Wamemwomba ziara zitakazofuata azungukie mataifa ya kiafrika.

Tanzania imekuwa ikisifika sana katika mataifa ya nje. Kwa bahati nzuri tumempata Rais ambaye ameonyesha dhamira ya kuirudisha Tanzania katika enzi za miaka ya 60s. Tumpe nguvu ili Tanzania iwe kiranja wa (EAC) na kwenye Umoja wa Afrika (AU) Mawasiliano :0713-399004 / 0767- 399004, jmkibasso@gmail.com