Bomoa bomoa Zanzibar izingatie haki za binadamu

24Apr 2016
Mwinyi Sadallah
Nipashe Jumapili
Bomoa bomoa Zanzibar izingatie haki za binadamu

MAFURIKO yanayotokana na mvua zinazonyesha kila mwaka yamekuwa tatizo sugu na linaloathiri Wazanzibari wengi, huku wengine wakilazimika kuomba na kupata hifadhi za muda shuleni ama sehemu za umma.

Changamoto hii inawaumiza zaidi wanaoishi kwenye mikondo ya mito kwani mvua zikinyesha hubadilisha mikondo ya mito na maji hubadili mielekeo na kuingia ndani ya nyumba.

Mafuriko hayo husababisha upotevu wa maisha, uharibifu wa miundombinu na mali. Wanafunzi ni miongoni mwa waathirika wakubwa wa tatizo hilo.

Ni kwa sababu wanakwama kuendelea na masomo kwa muda unaotakiwa kutokana na kukosa makazi, kupoteza vifaa na mahitaji muhimu ya shule kila mafuriko yanapotokea. Wasomi hao maendeleo yao hurudi nyuma wakati wenzao wakiendelea na masomo waathirika hawa hubakia kwa muda katika kambi za kuhifadhi waliopata mafuriko pamoja na familia zao.

Majengo ya Shule ya Mwanakwerekwe C, hapa Zanzibar yamekuwa maarufu kutumika kwa muda kuwa kambi za kutunza waathirika wa mafuriko kila mvua zinaponyesha na mafuriko kutokea kila mwaka.

Hata hivyo, wanafunzi wanaosoma shuleni hapo wanakuwa na wakati mgumu pale yanapotumiwa na waathirika wa mafuriko na kulazimika kuhamishiwa katika shule nyingine kwa muda kupisha kambi ya mafuriko.

Familia nyingi zinaathirika kutokana na kupokea waathirika wa mafuriko na kuiishi nao hali inayosababisha kuongezeka kwa matumizi kwenye familia na kuvuruga mfumo wa maisha ndani ya kaya.

Mbali na matatizo hayo mafuriko hayo ni kichocheo cha kipindupindu na kulifanya kuwa tatizo sugu kutokana na maji ya mafuriko kuchaganyikana na maji taka ya vyooni ambayo hupelekwa katika makazi ya wananchi.

Idadi kubwa ya wananchi waliojenga katika mikondo ya maji na karibu na mito waliokosa viwanja halali vya kupima kutokana na urasimu wa upatikanaji wa viwanja unaofanywa na baadhi ya viongozi na watendaji.

Tatizo la rushwa limeathiri kwa kiwango kikubwa na kukwamisha upatikanaji wa viwanja vya makazi kwa Wazanzibari na viwanja vingi vinavyopimwa katika miji mipya mathalani, Chukwani, Mbweni, Tunguu Mombasa kwa Mchina kuwanufaisha vigogo na wenye vipato vya juu huku maombi ya wanyonge yakitupwa nje kwa zaidi miaka 30 bila kufanikiwa.

Urasimu huo pia umechagia ramani ya mipango miji kutozingatiwa kutokana na wananchi wanyonge kulazimika kununua sehemu za mashamba ya watu na kujenga makazi au kuishi katika maeneo hatarishi.

Alhamisi wiki hii Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alitangaza mpango wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) wa kufanya maamuzi magumu ikiwamo kuvunja nyumba zilizojengwa kinyume na sheria katika mikondo ya maji na mito.

Aliwambia viongozi na watendaji wa wilaya kuwa SMZ italazimika kuchukua hatua hizo baada ya wananchi wengi kujenga nyumba katika maeneo hatarishi na yaliyotengwa kwa ajli ya miradi ya huduma za jamii visiwani humo.

Serikali kuendelea kuachia matumizi mabaya ya ardhi inawezekana ukafika wakati ikakosekana maeneo ya wazi na hata kilimo cha mboga, mathalani kama ilivyotokea katika Wilaya ya Mjini ambayo haina sehemu za mapumziko.

Msimamo wa SMZ kupitia kauli ya Makamu wa Pili wa Rais imefufua matumaini kwa wananchi lakini mpango huo lazima uzingatie utu na misingi ya haki za binadamu kwa kuhakikisha kuwa wanapatiwa viwanja kabla kuvunjiwa.

Hatua ya serikali ya kuwataka viongozi wa wilaya wakiwamo masheha kuanza kufanya uhakiki wa kuziorodhesha nyumba zote zilizojengwa bila ya kibali na katika maeneo yasiyostahiki ndiyo njia pekee ya kuondoa tatizo la mafuriko Zanzibar.

“Tunakusudia kubomoa majengo yaliyojengwa bila ya kibali na kwenye maeneo ya njia za maji ikiwa ni mwanzo wa maamuzi magumu yatakayochukuliwa na serikali ”.anasema Makamu wa Pili wa Rais. Anasema kuanzia sasa hakuna sheha atakayeruhusiwa kutoa, kuuza au kukata viwanja kwa ajili ya ujenzi wa nyumba jukumu ambalo liko chini ya Wizara ya Ardhi, Maji Nishati na Mazingira.

Pamoja na mpango huo wa SMZ inapaswa pia kuchukua hatua kwa viongozi wake na watendaji waliohusika kugawa na kuuza viwanja katika maeneo yasioruhusiwa badala ya kuvunja bila ya kuwaadhibu wahusika.

Hatua ya serikali kuwashughulikia kwa mujibu wa sheria viongozi waliohusika na kugawa au kuuza viwanja katika maeneo yasiyoruhusiwa pamoja na kushindwa kusimamia majukumu yao hitakuwa fundisho kubwa kwa viongozi na watendaji katika kuzimamia misingi ya uwajibikaji wa pamoaja.

Ni jambo la kushangaza watu wanafikia kujenga nyumba za makazi katika vyanzo vya maji huku serikali ikiendelea kuwalipa mishahara viongozi na watendaji dhamaza wakibakia ofisini na kuhatarisha maisha ya watu.

Uamuzi wa SMZ wa kuvunja nyumba zilizojengwa maeneo hatarishi unapaswa pia kuzingatia utu na ubinadamu ikiwamo kuwapatia viwanja wananchi hao kabla ya kuanza kubomoa na kutoa muda wa kutosha wa kuhamisha mali pamoja na serikali kuondoa urasimu wa upatikanaji wa Viwanja.

Mpango wa serikali wa kupima viwanja 380 mgao wake ufanyike kwa umakini ili wananchi wanyonge waliuojenga mabondeni na katika vyanzo vya maji wanufaike badala ya viwanja hivyo historia kujiruduia na kuwanufaisha vigogo na watu wenye kipato cha juu Zanzibar.