Aidha, chini ya Sheria ya Kanuni ya Adhabu kifungu cha 151, mwanamke yeyote ambaye atapatikana na hatia ya kosa la kutoa mimba atahukumiwa kifungo cha miaka saba jela.
Licha ya mazingira hayo yayozunguka suala hilo, zoezi hilo limekuwa likishamiri katika mazingira mabovu na kuhatarisha maisha ya wanawake.
Utoaji hufanywa na watu wasiokuwa na taaluma, wakiwamo waganga wa kienyeji, wakunga wa vichochoroni au matabibu na wauguzi wasio wabobezi.
Mijini mimba huchokonolewa kwenye nyumba za wageni, na maeneo ya vijijini kazi hiyo hufanywa vichakani au porini. Kuna wakati utoaji mimba hufanyika vyooni au kwenye majengo ya shule, mara nyingine katika mazingira ya giza.
Aidha, utoaji huo huweza kuhusisha vifaa vichafu kama spoki za baiskeli na vyuma vya mishikaki vyenye kutu, miti ya mihogo, mabomba ya majani ya migomba na mitidawa ya aina mbalimbali huingizwa kwenye kizazi na kusababisha vifo, maambukizi ya magonjwa hatari, ulemavu na ugumba.
UTOAJI MIMBA USIOSALAMA
Kama hivyo ndivyo hali ilivyo, ni kwanini wadau wa masuala ya kijamii wakiwamo serikali, wataaluma wa afya, wanawake ambao ni waathirika wakuu, viongozi wa dini, wanasheria na washauri nasaha wasianzishe mijadala ya kuzungumzia suala la utoaji mimba na kutoa mwelekeo?
Mapema wiki hii, taasisi ya kimataifa ya Pathfinder iliwakutanisha wanahabari pamoja mabingwa wa magonjwa ya wanawake na masuala ya afya ya uzazi, kujadili kitisho lililoko kwenye utoaji mimba na jinsi inavyochangia kuua wanawake.
Katika mjadala huo ilibainika kuwa utoaji mimba usio salama husababisha wanawake karibu 1,500 wakiwamo mabinti na wanafunzi kufa kila mwaka hapa nchini.
“Takwimu hizi ni vifo vilivyorekodiwa, pengine baada ya wagonjwa kufikishwa na kufariki wakiwa hospitalini. Hivi wale waliofia majumbani au kwa waganga wa kienyeji ni wangapi? Inawezekana idadi hiyo ni kubwa maradufu,” anasema Keneth Simbaya, mwanahabari na mshauri wa masula ya afya na haki ya uzazi salama.
Anasema wanawake 7,900 hufa kila mwaka nchini kutokana na matatizo ya uzazi na asilimia 18 ambao ni zaidi ya wanawake 1,400 vifo vyao vinatokana na utoaji mimba usio salama.
Ndiyo maana wanahabari na wataalamu wa uzazi wakiwamo kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na Pathfinder, wanashauri kuwe na mjadala wa kitaifa kuhusu utoaji wa mimba na maamuzi yafikiwe ili kuokoa maisha ya wanawake na watoto wengi wanaoangamia kutoka na ukimya unaoletwa na kukosa huduma.
“Suala ya utoaji mimba lina mtizamo hasi kwamba ni dhambi ya kuua. Lakini haizungumzi kuwa kubeba mimba kunahusu mwili, afya na saikolojia (akili) ya mwanamke. Kwa hiyo jamii isimzungumzie mwanamke huyu impe nafasi kujadili na kuamua nini kifanyike kuhusu tatizo hilo,” anashauri Keneth Simbaya,mwanahabari na mshauri wa afya na haki ya uzazi salama.
Anasisitiza kuwa ili kuondoa tatizo hilo serikali na wadau wahakikishe kuwa huduma na haki ya afya ya uzazi zinapatikana ili wanawake wakutane na wataalamu, washauriwe ama wahudumiwe kuepusha vifo vya wazazi vinavyoweza kuepukika.
Anaongeza kuwa wanawake hukimbilia kutoa mimba mafichoni kwa vile hakuna huduma wala wataalamu wa kuwashauri cha kufanya inapotokea kuwa wamebaba mimba wasizozihitaji. Lakini pia wanahofia sheria inayowahukumu kwa tendo hilo.
Anasema zipo mimba zinazopatikana kwa kubakwa na wazazi, kuvamiwa na kubakwa na majambazi au za mabinti wadogo mfano wa miaka 10 ambazo huacha maswali mengi na kuhitaji maamuzi.
Akizungumzia suala hilo Naibu Mkurugenzi wa Pathfinder Tanzania, Dk.Pacius Mapunda, anaongeza kuwa mimba hizo zitakuwa na athari kubwa kwa mhusika. Anafafanua kuwa iwapo mama hakuridhika na hali hiyo ya ujauzito hawezi kuukubali na ataathirika kisaikolojia na kimwili pamoja na mtoto aliye tumboni. Kwa maneno mengine hatakubali kuilea mimba asiyoipenda.
Rais wa Chama cha Madaktari wa Wanawake na Afya ya Uzazi, Profesa Andrea Pembe, akizungumza katika mkutano huo, alisema licha ya suala hilo kutozungumzwa hadharani, hali ni mbaya na kwamba dawa kama misoprostol na mifepriston zinatumika na nyingine wanatumia wajawazito licha ya kwamba hazijasajiliwa nchini.
Anasema misoprostol imesajailiwa na inatumika kuzuia damu nyingi kutoka baada ya kujifungua ama kuongeza uchungu, lakini wapo wanaoitumia kutoa mimba bila kujali ina muda gani.
Anaonya kuwa dawa hiyo inatakiwa itumike kwa maelekezo ya daktari lakini hutumiwa kienyeji na kusababisha athari nyingi vikiwamo vifo na maambukizi. Anaeleza kuwa inaweza kutoa mimba ya siku 49.
Akifafanua zaidi, Profesa Pembe anaeleza kuwa misoprostol inaweza isitoe mimba yote na kusababisha sehemu nyingine kubaki tumboni na kuhitaji kusafishwa.
Profesa Pembe ambaye ni mtaalamu wa magonjwa ya wanawake na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili, MUHAS, anasema Mifepriston haijasaliwa nchini lakini inapatikana na inatumiwa kutoa mimba.
Anasema utafiti uliofanyika mwaka 2013 ukihusisha , MUHAS, Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Tiba za Binadamu (NIMRI) na watafiti wa Marekani, ulibaini kuwa tatizo ni kubwa mijini na vijijini.
Anasisitiza kuwa kila mwanamke anapenda kuwa na mimba na kupata watoto na iwapo hataki mimba na anataka kuiharibu ni vigumu kumkataza.
ATHARI
Utoaji mimba usio salama ni sababu ya pili inayochangia vifo vingi vya wanawake vinavyohusisha uzazi. Sababu ya kwanza ni kutoka damu nyingi kupindukia wakati wa kujifungua, kwa mujibu wa Profesa Pembe.
Anaeleza kuwa mimba inapotolewa ‘kienyeji’ sehemu nyingine hubakia kwenye kizazi na kusababisha maambukizi hatari. “Hii inatokea kama aliyefanyiwa hivyo hatasafishwa kizazi kitaalamu.”
Vitu vyenye ncha kali vinavyotumiwa, anaeleza zaidi, hutoboa kizazi hata na utumbo mpana unaohusika na haja kubwa na kuleta hatari ya kinyesi kusambaa na kusababisha maambukizi na vifo. Kutoboa kizazi kunasababisha majeraha kwenye mfuko wa uzazi ambao ili kuokoa maisha inavbidi uondolewe.
Profesa Pembe anasema utafiti uliofanyika katika Hospitali ya Muhimbili mwaka 2011 ulibaini kuwa wanawake 155 walifarika kwa matatizo ya uzazi. Kati yao 23 walikufa kutoka na utoaji mimba usio salama.
Anatoa takwimu nyingine kuwa kati ya wanawake 35 waliotolewa mimba kwenye mazingira duni, saba walikuwa wametobolewa utumbo wa chakula na wengine watatu walifariki.
Anaeleza kuwa kutolewa mimba kusiko salama husababisha damu nyingi kupotea ama mara moja au kidogo kidogo na kusababisha ‘shock’ na baadaye vifo.
Anafafanua kuwa matatizo mengine yanayoambatana na utoaji mimba usiosalama ni pamoja na kupata makovu kwenye kizazi yanayoleta ugumba, kupanuliwa mdomo wa uzazi na kusababisha mimba kutoka mara kwa mara.
MAMBO YA KUJADILIWA
Wakichangia suala hilo wanahabari kutoka vyombo mbalimbali walitaka kuwe na mijadala ya wazi ya utoaji mimba na wanawake washirikishwe kikamilifu kutoa maoni yao.
Suala hilo lijadiliwe kwa uwazi bila kificho mapendekezo na nini kifanyike yatolewe na yafanyiwe kazi.
Wanataka pia sheria iangaliwe. Tanzania haina sheria ya kutoa mimba, lakini vipo vifungu vya Kanuni ya Adhabu vinavyoharamisha utoaji mimba.
Sura ya 16 ya kanuni hizo vifungu vinavyoanzia 150 hadi 152 vinazungumzia adhabu ya mwanamke aliyetoa mimba, aliyeitoa na aliyesaidia kufanikisha utoaji mimba.
Inaeleza kuwa anayetoa, mara nyingi ni dakatari, atafungwa miaka 14, mwanamke anayetolewa atatupwa gerezani miaka saba wakati aliyesaidia kufanikisha utoaji huo atahukumiwa miaka mitatu jela.
Wanahabari wanaona kuwa sheria hiyo inawafanya madaktari kuogopa kusaidia walioharibu mimba na hata wanawake wahofu kuulizia huduma za utoaji mimba na kusababisha wakimbilie maeneo yasiyo salama.
Hata hivyo waandishi walikubaliana kuwa kanuni ya adhabu haikatazi moja kwa moja utoaji mimba kwa kuwa inaruhusiwa iondolewe iwapo inahatarisha maisha ya mama na si vinginevyo.
MIMBA ZENYE MIGOGORO
Washiriki wanapendekeza kanuni ya adhabu itizame ujauzito wenye migogoro kama ule wa kubakwa na mzazi, vichaa wanaovizia wanawake, viongozi wa kidini na mimba zinazopatikana baada ya kuvamiwa na kubakwa majambazi.
Kadhalika sheria hiyo iangalie namna ya kuwasaidia wanawake wanaoishi na VVU ambao hawana kipato pia ni wagonjwa, lakini wamejikuta na ujauzito na wasingependa kupata watoto.
Pamoja na eneo hilo, wana kongamano walishauri kanuni ya adhabu ione namna ya kuruhusu iwapo mimba ina hitilafu kwa mfano kiumbe kilichoko tumboni kina upungufu na kasoro za kimaumbile ili kuwaepusha wenye kujifungua viumbe vya ajabu.
Kwa upande mwingine, wanasemina walishauri sheria iangalie jinsi ya kuwasaidia watu wenye ulemavu, hasa wa akili, ambao hubakwa na kupewa ujauzito.
Lakini pia wanapendekeza sheria iruhusu wanawake wawe na haki ya kuzungumzia ujauzito walionao iwapo wanapenda ama wasingependa kuendelea na mimba hizo mpaka mwisho.
Serikali iruhusu wafanyiwe uchunguzi wakukutana na watalaamu kwenye kliniki, wapate huduma pamoja na ushauri nasaha na wasaidiwe kufanya kile wanachokusudia.










